DONDOO ULAYA

DONDOO ULAYA

573
0
KUSHIRIKI

jorge-mendes-agent-ronaldo_3472788MENDES APELEKA WATATU MILAN

MILAN, Italia

KWA mujibu wa mtandao wa SkySports, wakala Jorge Mendes, amekutana na wakurugenzi wa klabu ya AC Milan, Marco Fassone na Massimiliano Mirabelli, katika kisiwa cha Sardinia juzi Jumanne kwa ajili ya kujadili dili za wachezaji watatu.

Imedaiwa kuwa, Mendes alienda na majina ya wachezaji hawa ambao alidhani huenda Milan ingevutiwa kuwa nao msimu ujao: Diego Costa (Chelsea), Renato Sanches (Bayern Munich) na Radamel Falcao (Monaco).

Man Utd bado yamuota Matic

MANCHESTER, England

MASHETANI wekundu, Manchester United bado wanafikiria kumsajili kiungo wa Chelsea, Nemanja Matic.

United ambao hadi sasa wameshazinasa saini za nyota wawili, wanataka kumpata na kiungo mkabaji mmoja, ambapo Matic mwenye umri wa miaka 28 na mwenye thamani ya pauni milioni 40 ameivutia timu hiyo.

PSG huwaambii kitu kwa Neymar

PARIS, Ufaransa

KLABU ya Paris St-Germain bado ina matumaini ya kumaliza dili la kumsajili mshambuliaji wa Barcelona, Neymar kwa dau la pauni milioni 198 ndani ya siku 15.

Mtandao wa L’Equipe wa Ufaransa, umedai kuwa miamba hao wa Ufaransa wana matumaini makubwa ya kumsajili Neymar ambaye hadi sasa anaonekana kuwa na furaha ndani ya klabu yake ya Barca.

Guardiola ajipanga kumbeba Mbappe

MANCHESTER, England

WAKATI tetesi nyingi zikiitaja klabu ya Real Madrid kuwa kwenye mpango mzito wa kumsajili mshambuliaji wa Monaco, Kylian Mbappe, imeonekana Pep Guardiola naye anammezea mate fowadi huyo.

Kocha huyo wa Manchester City alisema kuwa, anaamini timu yake ina nguvu kiuchumi hivyo hatishiwi na Madrid kwenye harakati zake za kumnasa Mbappe.

Nainggolan ‘ajitia kitanzi’ Roma

ROME, Italia

KIUNGO wa klabu ya AS Roma, Radja Nainggolan, amezima tetesi za yeye kutakiwa na Man United, baada ya kuongeza mkataba mpya wa kuitumikia klabu yake hiyo, Sky Sports imetaarifu.

Kiungo huyo alikuwa akihusishwa na tetesi za kuondoka jijini Roma, lakini taarifa za mkataba huo mpya zimefuta fununu zote.

Matias Fernandes aitamani Valencia

VALENCIA, Hispania

TETESI zinadai kuwa kiungo wa klabu ya AC Milan, Matias Fernandez, mwenye umri wa miaka 31, anataka kuikacha timu hiyo na kuhamia Valencia.

Tangu alipotua Milan, Fernandez ambaye alikuwa akifanya vyema na klabu ya Fiorentina, anatamani kuhamisha majeshi yake ndani ya klabu ya Valencia inayoshiriki Ligi Kuu Hispania.

Perez wa Arsenal aitwa Deportivo

MADRID, Hispania

KLABU ya Deportivo imedhamiria kutoa ofa ya euro milioni tisa kumsajili mshambuliaji wao wa zamani, Lucas Perez, aliyesajiliwa na washika mitutu wa jiji la London, Arsenal.

Rais wa klabu hiyo, Tino Fernandez, amesema jambo la kwanza kabla ya msimu mpya kuanza ni kuhakikisha anamchukua Perez ambaye anataka kurudi Hispania kufuatia kipindi kibovu cha kucheza soka England.

Inter kuchukua ‘kimeo’ cha Juve

MILAN, Italia

INTER Milan wapo mbioni kukamilisha dili la kumchukua mchezaji aliyefeli vipimo Juventus, Patrik Schick.

Schick alikuwa mmoja wa wachezaji wa kwanza kununuliwa na Juve katika dirisha la usajili wa majira haya ya kiangazi kutoka Sampdoria, lakini alishindwa kufaulu vipimo na Juve ikaamua kumtema. Hata hivyo, Inter hawataki kupitwa na fursa ya kumsajili mmoja wa wachezaji walioonesha uwezo mkubwa msimu uliopita.

Leeds wamweka Wood sokoni

LONDON, England

KLABU ya Leeds imeonekana kuzitamani pesa za timu za Ligi Kuu England kwa kusema wazi kwamba thamani ya mshambuliaji wao, Chris Wood, ni pauni milioni 20.

Moja ya klabu iliyokuwa ikimtamani Wood ni Huddersfield ambayo imepanda Ligi Kuu msimu huu pamoja na Crystal Palace, Swansea, Stoke, West Ham, West Brom na Southampton.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU