MASTAA WENYE ‘MAHABA’ NA KLABU ZA SIMBA NA YANGA

MASTAA WENYE ‘MAHABA’ NA KLABU ZA SIMBA NA YANGA

1032
0
KUSHIRIKI

NA JESSCA NANGAWE

WAPO mastaa mbalimbali ambao mbali ya kufanya vyema kupitia taaluma zao, lakini wamejikuta wakiwa na mapenzi makubwa na vitu vingine ambavyo vinashaabiana na sanaa zao.

Wasanii wengi wa fani ya muziki duniani kote baadhi yao wamekua na mapenzi na mambo ya soka na michezo mingine na mfano mzuri ni familia ya mwanamuziki tajiri duniani, Jay Z na mkewe Beyonce ambao mbali ya kuwa na hisa na timu pia wamekua mashabiki wakubwa wa timu ya mpira wa kikapu ya Brooklyn Net ya Marekani.

Kwa hapa kwetu tumeshuhudia mastaa mbalimbali wa muziki wakionyesha mahaba yao ya dhati kwa klabu kubwa za soka hapa nchini za Simba na Yanga na mara nyingi tumekua tukikutana nao uwanjani wakiwa na jezi zao tayari kuzisapoti timu wanazozipenda.

ALI KIBA

Staa huyu ambaye anafanya vyema kwenye medali ya burudani kwa sasa ni shabiki mkubwa wa klabu ya Yanga na amekua akimhusudu sana aliyekua kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima.

Mara nyingi Ali Kiba amekua akihudhuria uwanjani na kujichanganya na mashabiki, licha ya kuondoka kwa kiungo huyo msanii huyo aliweza kutoa yake ya moyoni kwa kudai pamoja na Niyonzima kuondoka lakini ataendelea kuwa kipenzi chake na kamwe hawezi kuacha kuishabikia timu ya Yanga.

Vincent Kigosi ‘Ray’

Huyu ni staa wa Bongo Movie ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga na amekua akiisapoti timu hiyo wakati wote timu inapocheza mechi za ligi pamoja za kimataifa.

Ray ameweka wazi mahaba yake kwa timu ya Yanga na kufikia kusisitiza kuwa anatamani mtoto wake aitwaye Jayden kuja kurithi mapenzi ya baba yake kwa kuendelea kuipenda Yanga siku zote.

Jacob Steven ‘JB’

Pamoja na kufanya vizuri kwenye filamu zake, JB amekuwa mwanamichezo mzuri ambapo amekua akishiriki mashindano mbalimbali ya soka.

Mapenzi yake kwa klabu ya Simba yameendelea kuonekana kwani mara nyingi pamoja na kufanya kazi pamoja na Ray, lakini wamekuwa wapinzani wazuri sana linapokuja suala la Simba na Yanga kwa kuwa wamekua timu mbili pinzani.

Katika mechi zinazokutanisha timu hizo JB na Ray wamekua kivutio kikubwa sana uwanjani kwa kuwa wamefikia hata hatua ya kuwekeana dau kwa timu itakayofanya vizuri.

Elizabeth Michael ‘Lulu’

Mrembo Lulu amekua na mapenzi makubwa na Simba licha ya kuonekana uwanjani mara chache.

Linapokuja pambano la Simba na Yanga hutumia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii kutoa tambo zake hata pale timu inapofungwa na mara nyingine amekuwa akionekana uwanjani kuisapoti timu yake.

Irene Uwoya

Staa huyu wa Bongo Movie naye huwa habaki nyuma katika kuisapoti klabu ya Yanga na mara nyingi amekuwa akienda uwanjani kwa ajili ya kuishangilia timu yake akiambatana na mwanaye anayejulikana kwa jina la Krish.

Snura Mushi

Miongoni mwa wanamuziki wanawake wenye mapenzi na Simba ni pamoja na Snura Mushi anayefanya vyema kwa sasa na kibao chake kipya cha ‘Zungusha’ akimshirikisha Christian Bella.

Snura ni shabiki mkubwa sana wa Ibrahim Ajib ambaye kwa sasa ametua Yanga pamoja na Shiza Kichuya aliyempa zawadi ya viatu msimu uliopita baada ya kufanikiwa kuwafunga watani zao Yanga katika mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wema Sepetu

Wema ana mapenzi makubwa sana na Yanga licha ya kutoonekana mara nyingi uwanjani kama ilivyo kwa wasanii wenzake na alikua na upendo mkubwa kwa aliyekua kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima, akidai ni kutokana na uwezo wake anaouonyesha uwanjani.

Alisema amekua na mapenzi makubwa na timu hiyo tangu akiwa mdogo na ataendelea kuisapoti inapokuwa nyumbani hata katika mashindano ya kimataifa.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU