CASSPER NYOVEST MJUKUU WA MANDELA ALIYEKINUKISHA LEADERS CLUB

CASSPER NYOVEST MJUKUU WA MANDELA ALIYEKINUKISHA LEADERS CLUB

322
0
KUSHIRIKI

NA TULINAGWE MALOPA

JULAI 22, mwaka huu, mashabiki wa muziki nchini walipata bonge la burudani katika tamasha la Castle Lite Unlocks, lililofanyika kwenye viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.

Wasanii waliotoa shoo katika tamasha hilo walikuwa ni mkali wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond’, Vanessa Mdee ‘V Money’, kundi la Navy Kenzo na lile la Weusi.

Pia alikuwapo rapa Mmarekani Nayvadius Wilburn ‘Future’ na rapa wa Afrika Kusini, Refiloe Phoolo ‘Cassper Nyovest’.

Kama ilivyokuwa kwa wasanii wengine waliofanya shoo siku hiyo, Cassper alifunika balaa kutokana na umahiri wake katika muziki wa hip hop.

Kwa muda wote aliokuwapo jukwaani, mkali huyo aliimba kwa hisia kali pamoja na kucheza kwa umahiri wa hali ya juu, huku akipewa sapoti na mashabiki waliojitokeza ambao walionekana kuzifahamu vilivyo baadhi ya nyimbo zake tofauti na ilivyotarajiwa.

Kitendo cha ‘wabongo’ kumsapoti kuimba baadhi ya nyimbo zake na kuzicheza kwa ustadi, kilionekana kumpagawisha mno Cassper na kuongeza mzuka, hali iliyoongeza burudani katika tamasha hilo.

Hata Diamond na Future walipopanda jukwaani baadaye, tayari mashabiki walionekana kutojutia kufika kwao Leaders Club kutokana na kile walichokipata kutoka kwa ‘mjukuu’ wa mpigania uhuru wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

 

Cassper Nyovest ni nani?

Cassper Nyovest ambaye jina lake kamili ni Refiloe Maele Pholo, alizaliwa Desemba 16, 1990, mjini Mafikeng, Afrika Kusini, akiwa pia ni mtayarishaji wa muziki. Albamu yake ya kwanza inayojulikana kama “Tsholofelo”, ilizinduliwa Julai 18, mwaka 2014 ambapo kwa sasa amekuwa akifanya muziki wake binafsi kwa mafanikio makubwa.

Maisha yake

Nyovest alikulia huko Montshiwa, Makifeng ambao ni mji mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Magharibi. Alisoma shule ya Sekondari Sol Plaatje na akiwa huko alikuwa ni mwanariadha huku pia akijihusisha na michezo mingine kama soka, mpira wa kikapu na mingineyo. Alianza kuwa rapa alivyokuwa darasa la sita, akiwa na umri wa miaka 12.

Rapa huyo alifeli mitihani ya darasa la 10 na hivyo kuhamia kwa bibi yake huko Potchefstroom. Mwaka uliofuata alipotimiza umri wa miaka 16, aliamua kuacha kusoma.

“Niliwaambia wazazi ni bora nikuze kipaji ninachoamini kitanitoa, kuliko kukipuuzia na kujuta maishani,” alisema wakati fulani katika mahojiano na vyombo vya habari.

Nyovest alihamia jijini Johannesburg mwaka uliofuata na kujiingiza katika tasnia ya muziki kama rapa na mtayarishaji muziki.

Baadaye rapa wa Motswako HHP, alimwona Nyovest akifanya shoo na hivyo kuamua kumshirikisha kwenye wimbo wake wa ‘Wamo Tseba Mtho’ uliopo kwenye albamu yake ya Dumela. Nyovest alianza kuambatana na HHP ndipo alipozidisha umaarufu wake kama msanii.

Pia, ukaribu wake na mkali huyo, ulimwezesha kufahamiana na nyota wa muziki kama Kid Cud, Kendrick Lamar, Nas Talib na Wiz Khalifa.

Mwaka 2014, Nyovest alihusishwa kwenye bifu na marapa wengine wa Afrika Kusini hali iliyowafanya kila mmoja kurekodi nyimbo za kusemana.

Albamu zake

Mwaka 2013, alizindua wimbo wa ‘Gusheshe’ kwa mara ya kwanza kutoka albamu yake ya kwanza ya Tsholofelo ilipokewa vizuri mno na kupigwa mara nyingi katika vituo mbalimbali vya redio huko Afrika Kusini.

Baada ya ‘Gusheshe’, alitoa ‘single’ yake ya pili iliyoitwa ‘Doc Shebeleza’ iliyozidi kumpa mafanikio ambao ulifanikiwa kuchukua nafasi ya nne kwenye chati za muziki nchini humo. Miongoni mwa walioguswa na wimbo huo, ni mkongwe wa muziki Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla, Yvonne Chakachaka.

Wimbo wake wa kwanza wa ‘Tsholofelo’, ulizinduliwa Julai 18, 2014 na kushika nafasi za juu katika chati mbalimbali za muziki ndani ya miezi miwili mfululizo.

Oktoba 2014, Nyovest alishika nafasi ya pili katika tuzo za ‘The Hottest Mc In Afrika’ zilizoandaliwa na MTV Base, akitanguliwa na K.O.

Hata hivyo, rapa huyo alilalamikia ushindi wa K.O kwa madai kuwa ulitokana na ukaribu wake na DJ Vigilante aliyekuwa na bifu naye.

Baada ya hapo, Cassper Nyovest, aliendelea kutesa kwenye muziki kwa kutoa nyimbo kali pamoja na albamu za ukweli zilizomwezesha kutwaa tuzo mbalimbali na kuzoa mashabiki lukuki Afrika Kusini na kila pembe ya dunia.

Huyo ndiye Cassper Nyovest, rapa mahiri Afrika Kusini.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU