ACHA MATIC, HAWA PIA MOURINHO ALIWASAJILI MARA MBILI

ACHA MATIC, HAWA PIA MOURINHO ALIWASAJILI MARA MBILI

782
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

MANCHESTER United wamekamilisha usajili wa kiungo Nemanja Matic kutoka Chelsea, wakitumia kiasi cha pauni milioni 40 kuinasa huduma yake.

Nyota huyo wa kimataifa wa Serbia, ametua Old Trafford na kupewa mkataba wa miaka mitatu, ukiwa ni usajili wa tatu kwa Jose Mourinho baada ya kuwanasa Victor Lindelof na Romelu Lukaku.

“Kufanya kazi na Jose Mourinho ni nafasi ambayo nisingeweza kuipotezea,” ni maneno ya Matic baada ya kukamilisha usajili wake huo.

Matic anaiacha Chelsea ambayo msimu uliopita aliichezea mechi 35 kati ya 38 za Ligi Kuu England na kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa.

“Nimefurahia muda wangu niliokuwa Chelsea na ningependa kuishukuru klabu na mashabiki kwa kuniunga mkono.

“Nasubiri kukutana na wachezaji wenzangu wapya na kuanza mazoezi na timu,” alisema Matic.

Kuondoka kwa nyota huyo Stamford Bridge kulitarajiwa na wengi, hasa baada ya kusajiliwa kwa kiungo Tiemoue Bakayoko, aliyechukuliwa kwa ada ya pauni milioni 40 akitokea Monaco.

Haitakuwa mara ya kwanza kwa Mourinho kufanya kazi na Matic kwani waliwahi kuwa pamoja Stamford Bridge misimu kadhaa iliyopita.

Mwaka 2014, Mourinho ndiye aliyemsajili mchezaji huyo, huku ikielezwa kuwa alitumia kitita cha pauni milioni 21 kufanikisha mpango wake huo.

Hata hivyo, Matic si mchezaji pekee aliyewahi kusajiliwa mara mbili na kocha huyo mwenye heshima kubwa kwenye ulimwengu wa soka.

Maniche

Kiungo huyo alikuwa na Mourinho katika kikosi chja Porto kilichokuwa tishio kuanzia mwaka 2002-04.

Mwaka 2006, Mourinho alimchukua Maniche ambaye kwa kipindi hicho alikuwa Dinamo Moscow kwa mkopo. Hata hivyo, Maniche alilimwa kadi nyekundu katika mchezo wake wa kwanza akiwa na ‘uzi’ wa Blues.

Baadaye, nyota huyo alijikuta akishindwa kujihakikishia namba kwenye kikosi hicho na ndipo alipoamua kurejea Moscow.

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea Inter Milan, Aletico Madrid na FC Koln ya Bundesliga, alistaafu mwaka 2011.

Paulo Ferreira

Ni miongoni mwa mabeki wa kulia waliokuwa wakimvutia Mourinho alipokuwa akiinoa Porto.

Baada ya kuhamia Chelsea, Mourinho alimvuta Mreno mwenzake huyo kwa ada ya pauni milioni 13.

Hata baada ya kuondoka kwa Mourinho aliyetimkia Inter Milan, Ferreira aliichezea Chelsea kwa misimu tisa kabla ya kutundika daluga mwaka 2013.

Michael Essien

Alipokuwa Chelsea, Mourinho alimsajili kiungo huyo aliyekuwa akiichezea Lyon kwa kipindi hicho. Mghana huyo alikuwa sehemu muhimu ya kiungo katika kikosi cha Chelsea kabla ya kuzinguliwa na majeruhi mwaka 2008.

Mourinho alipokwenda Real Madrid, alipendekeza kusajiliwa kwa Essien na hatimaye aliungana tena na mchezaji wake huyo katika msimu wa 2012-13.

Mpaka leo, Mourinho amekuwa akimtaja Essien kuwa mmoja kati ya wachezaji bora aliowahi kuwafundisha.

Mwaka jana, Essien alijiunga na Persib Bandug ya Indonesia anayoichezea hadi sasa, baada ya kukataa ofa ya kukipiga Australia.

Ricardo Calvalho

Baada ya Mourinho kutua Chelsea akitokea Ureno alikokuwa akiinoa Porto, aliiambia Blues kuwa anamhitaji Carvalho kwenye safu ya ulinzi.

Haikuishia hapo, mkufunzi huyo alipotimkia Real Madrid, alimtaka Rais wa mabingwa hao wa La Liga, Florentino Perez, kuhakikisha beki huyo anang’oka Blues na kutua Santiago Bernabeu.

Mwaka 2011, alitangaza ghafla kuachana na majukumu ya timu ya Taifa ya Ureno kwa kile alichokitaja kuwa ni udhalilishwaji aliofanyiwa na staa mwenzake kwenye kikosi hicho, Paulo Bento.
Wawili hao walikorofishana wakiwa mazoezini na ilielezwa kuwa Bento alimtaja Carvalho kuwa chanzo cha ubovu wa safu yao ya ulinzi.

Romelu Lukaku

Mwaka 2013, straika huyo wa kimataifa wa Ubelgiji alirejea Chelsea baada ya kung’ara akiwa na West Brom kwa mkopo.

Ni Mourinho aliyekuwa Chelsea kwa mara yake ya pili, ndiye aliyependekeza kurudishwa kwa Lukaku hasa baada ya Mbelgiji huyo kung’ara akiwa na West Brom kwa mkopo ambapo aliifungia mabao 17.

Hata hivyo, mambo hayakwenda vizuri kwa Lukaku, kwani chini ya Mreno huyo, alicheza mechi mbili pekee na ndipo alipopelekwa Everton kwa mkopo.

Katika majira haya ya kiangazi, Mourinho ametumia pauni milioni 75 kumsajili Lukaku na safari hii wamekutana wakiwa ni waajiriwa wa Manchester United.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU