DUNIA YA MKE WANGU

DUNIA YA MKE WANGU

339
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia

Taarifa hiyo pia ilileta habari ya dunia iliyozidi kutangaza hali ya hatari katika pande zote za dunia. Tayari ugonjwa wa Ebola ulikuwa umeingia katika mabara yote saba. Katika Bara la Asia tayari watu 100 walishakuwa wamepoteza maisha, huku zaidi ya 800 wakiwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo. Barani Ulaya watu 20 walishakuwa wamepoteza maisha na wengine 90 wakigundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

SASA ENDELEA

Taarifa hizo zilizidi kuleta hofu kubwa duniani. Mamlaka husika zilijitahidi kwa kila hali kuweza kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo, lakini hazikuweza kufanikiwa.

Wanasayansi kutoka pande zote za dunia, waliendelea kukutana maabara kuu ya dunia nchini Marekani kujadili njia mbadala ya kuweza kukabiliana na Ebola, huku wakizidi kuhangaika kutafuta dawa ya kutibu ugonjwa huo.

Kamishna wa Shirika la Afya duniani (WHO), Leot Ving, hakupata usingizi aliendelea kuzunguka huku na kule katika nchi mbalimbali kuona anapata ufumbuzi.

Watu walishaanza kuona kama mwisho wa dunia ulikuwa umekaribia, wengi walikesha kwenye nyumba za ibada wakimwomba Mungu awaepushe na Ebola.

Taarifa hiyo ilizidi kumchanganya Kai na kumwogopesha. Lakini alijipa nguvu akiamini ni helr kufa pamoja na mkewe, kuliko kubaki peke yake katika dunia hii.

Lakini alichanganyikiwa baada ya kumpigia simu Julia ili kumjulisha kuwa  tayari alikuwa amefika Ethiopia. Mtandao ulikuwa haupatikani. Muda mwingi simu ilikuwa ikiita na kukatika hata kabla haijapokelewa.

Alijaribu kupiga masaa yote lakini simu haikupatikana. Hakujua ni kwanini wakati jana yake alikuwa ametoka kuongea na Julia. Alizidi kuchanganyikiwa tena kwa kiasi  kikubwa.

Usiku huo alituma taarifa kwenye mtandao wa wanasayansi akiwajulisha kuwa alikuwa nchini Ethiopia na akijiandaa kuingia mji wa Amhara. Chuo chake cha Heath For world kilikuwa cha kwanza kupata taarifa hizo. Wanafunzi wengi walimpinga Kai kwa uamuzi aliouchukua.

Taarifa hiyo ilifika maabara kuu ya dunia. Wanasayansi wengi walilipinga suala hilo. Walipinga kwa sababu Kai alikuwa ni mwanasayansi mkubwa japo alikuwa ni mwanafunzi. Wanasayansi wakubwa kama yeye walitakiwa kulindwa na kujitunza kutokana na uchache wao.

Kai alitoa maelezo kwenye mtandao wa wanasayansi pamoja na akaunti yake ya Twitter akisema kuwa mke wake kipenzi, alikuwa amekwama katika mji wa Amhara.  Alisema madaktari  waliokwenda na mkewe wote wamefariki aliyekuwa amebaki Keneza ni mkewe tu.

Aliongeza kwa kuandika kuwa mke wake ambaye ni Dk. Julia, alifanikisha kuondolewa kwa zaidi ya watoto 10,000 katika Kijiji cha Keneza. Hivyo hawezi kumuacha katika nchi hiyo. Alisema pia safari ya kwenda kumchukua mkewe, itamsaidia kufanya mambo fulani ya kiuchunguzi.

Kiongozi mkuu wa wanasayansi duniani aliuomba umoja wa mataifa kumlinda Kai, akitaka  aruhusiwe kwenda Amahara. Umoja wa mataifa ulitoa taarifa kwa serikali ya nchini Ethiopia ukiitaka  kumlinda Kai.

Umoja wa chama cha wanasayansi cha dunia ulishindwa kumzuia Kai kwa sababu, ulipata taarifa kutoka chuoni kwake kuwa maisha ya Kai yanategemea uwepo wa mkewe.

Wakati huo serikali ya Ethiopia, ilikuwa na hofu kwa sababu, ilikuwa imezembea hadi kupelekea wauguzi na madaktari kadhaa kutoondolewa katika miji iliyokuwa na maambukizi.

Saa kumi jioni magari ya umoja wa mataifa pamoja na ya jeshi la Ethiopia, yalifika katika hoteli aliyofikia Kai. Kai alichungulia dirishani na kukutana na wanajeshi hao.

Alivaa suruali yake ya jinzi pamoja na shati jeupe. Alikaa kwenye kiti na kumuomba Mungu amlinde katika safari hiyo ya kuogofya. Baada ya sala hiyo fupi, alifungua begi lake na kuitoa ile kinga ya virusi vya Ebola, kinga aliyokuwa ameingundua akiwa London baada ya kuota ile ndoto.

Aliinyanyua chupa juu na kuitikisa, aliitazama kwa dakika mbili akiitafakari kwa umakini mkubwa. Bado hakuwa na uthibitisho wa kutosha kuwa dawa hiyo, ilikuwa inaweza kweli kumkinga binadamu asipatwe na virusi vya Ebola. Imani ndogo aliyokuwa nayo, ilikuwa ni ya Kimungu na si ya kisayansi.

Alichukua sindano na kuivuta ile dawa. Akajifunga mpira kwenye mkono wake wa kushoto na kuutafuta mshipa mkubwa. Aliitumbukiza ncha ya sindano kwenye mshipa, akabonyeza sindano ili kuiruhusu dawa kuingia kwenye damu.

Nusu nzima ya dawa, aliingiza kwenye mshipa. Dawa ilianza kutembea kwa kasi kwenye mishipa yote ikienea kwenye mwili wake wote. Yeye kama mwanasayansi, aliiona tofauti ya kimwili iliyojitokeza pindi dawa hiyo ilipokuwa ikisafiri ndani ya damu.

Baada ya hapo alijiweka sawa na kutoka mle chumbani alishuka ngazi, ambapo alielekea nje ya hoteli. Nje alikutana na jeshi la Ethiopia pamoja na watu wa umoja wa mataifa. Baadhi ya watu wa shirika la Afya Duniani (WHO) walikuwepo. Waandishi wa habari wa mashirika mbalimbali wote walijazana wakichukua matukio, huku wakijiandaa kunasa maongezi ya Kai na watu hao.

Viongozi wao pamoja na makamanda wa jeshi walimuomba Kai akae pamoja nao kwa ajili ya mazungumzo mafupi. Lakini Kai alijua nia yao ilikuwa ni kutaka kumzuia asiende Amhara katika kijiji cha Keneza.

“Habari yako Mr. Kai,” aliongea kamanda wa jeshi akiwa pamoja na vongozi wa umoja wa mataifa.

“Kwangu si njema,” alijibu Kai huku akiwapa mkono.

“Mr Kai tunaomba tuzungumze kidogo.”

“Sina muda huo kwa sasa naomba mniache.”

“Mr Kai hali ya kijiji cha Keneza ni mbaya sana. Hakuna binadamu anayeishi huko kwa sasa. Na kama wapo basi wako kwenye hatua mbaya ya kuugua. Virusi vya Ebola vinasambaa kwa njia ya hewa kwa haraka sana, kwa sababu maiti zimezagaa kote.”

“Hilo nalijua, niacheni niende.”

“Mr Kai ukienda huko hautotoka salama. Kumbuka Afrika inakutegemea. Serikali ya Uingereza imetuambia tusikuache uwende Amhara,” alizidi kuongea kamanda huyo wa jeshi.

“Hili ni bara langu na kumbukeni sipendi kuona Waafrika wenzangu wakipoteza maisha. Nikifa mimi ni sawa tu kwa kuwa wengi wamekufa,” alijibu Kai.

“Mr Kai najua unakwenda kumtafuta mkeo lakini amini kuwa mke wako amekwisha kupoteza maisha.”

Kai aliposikia hivyo alikasirika sana, maana maneno hayo yalikuwa mabaya kwake. Mapigo ya moyo wake yaliongezeka ghafla, alihema kwa nguvu. Alimtazama kamanda yule kwa muda mrefu kisha akamjibu.

“Nahisi serikali yako ingekuwa makini mke wangu angekuwa mahali hapa. Niache nikafe na mke wangu.”

Kai aliposema hivyo, alipiga hatua kwenda mbele akitaka kuondoka lile eneo. Lakini jeshi lilimzunguka ili kumzuia asiondoke.

“Mke wangu ndio uhai wangu. akifa yeye lazima na mimi nitakufa, hivyo hamna haja ya kunizuia. Na wala haitowasaidia. Tena ni bora mngeniruhusu ili nikauone mwili wa wake, huenda ninaweza kupata nafasi ya kuishi,” aliongea Kai akitokwa na machozi.

Waandishi wa habari waliendelea kuchukua matukio hayo na kuyarusha moja kwa moja katika vituo vyao vya televisheni duniani kote.

Muda huo huo kiongozi wa wanasayansi alimpigia simu katibu wa umoja wa mataifa, akimtaka mwanafunzi wake aruhusiwe kuingia Amhara. Katibu huyo, alimpigia simu Rais wa Ethiopia Amiton Lakeba, ambaye naye alimpigia Kamanda wa jeshi aliyekuwa na jeshi pale nje ya hoteli.

Rais Lakeba alimtaka kamanda huyo wa jeshi kumuacha Kai aingie mji wa Amhara.

Baadae kamanda alimruhusu Kai kuelekea Amhara. Alimpatia gari aina ya Pajero pamoja na vyakula. Kai aliingia kwenye gari. Kabla hajaondoka, kamanda huyo aliwachagua wanajeshi sita  kwa ajili ya kumlinda Kai. Lakini Kai alikataa akisema kuwa ugonjwa wa Ebola haupigwi kwa risasi. Alitaka kwenda mwenyewe, hakutaka binadamu mwingine apatwe na ugonjwa huo kwa ajili yake.

Nchini Tanzania, raia wote wa nchi hiyo, pamoja na Serikali yao, walikuwa kwenye majonzi makubwa, wakijua kuwa Kai hawezi kurudi. Taifa la Tanzania lilimtegemea kijana huyo kwani alikuwa ni mwanasayansi pekee na mkubwa kuwahi kutokea kwenye historia ya nchi hiyo. Hivyo walijivunia kuwa na mwanasayansi pekee kutoka barani Afrika akitoka kwenye nchi yao.

Kai aliwasha gari na kuondoka jijini Addis Ababa. Aliichukua picha ya mkewe na kuibandika kwenye kioo cha mbele cha gari. Maana alikuwa akimtamani kumwangalia muda wote. Alikuwa haamini kama kweli anakwenda kumpoteza mke mzuri kama Julia.

Nini kitaendelea? Usikose kesho.           

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU