Z ANTO KUTOKA ‘BINTI KIZIWI’ HADI ‘KACHEZE UNAPOCHEZAGA’

Z ANTO KUTOKA ‘BINTI KIZIWI’ HADI ‘KACHEZE UNAPOCHEZAGA’

539
0
KUSHIRIKI

NA JOHANES RESPICHIUS

KAMA ulikuwa shabiki wa muziki wa Bongo Fleva miaka ya 2008, bila shaka utakuwa unaukumbuka wimbo wa Binti Kiziwi, ulioimbwa na Ally Mohamed, maarufu Z Anto, akimshirikisha ‘Pingu’.

Binti Kiziwi ulifanya vema, hivyo kumtambulisha vizuri Z Anto kwenye anga ya Bongo Fleva, kwani ulikuwa kama wimbo wa taifa kutokana na jinsi ulivyobamba.

BINGWA lilifanya mahojiano na staa huyu wa singo ya Kisiwa cha Malavidavi ambaye ni muda mrefu amepotea kwenye ramani ya Bongo Fleva, ambapo ameelezea milima na mabonde aliyoyapitia kwenye maisha yake ya sanaa.

BINGWA: Umekuwa kimya kwa kitambo kidogo, unaweza kuelezea ujio wako mpya?

Z Anto: Kwa wakati huu nina kila sababu ya kurudi tena kwenye sanaa, kwani nimeshajua kila changamoto inayoikabili tasnia na dawa yake nimeshaipata tayari.

Ujio huu mpya si wa kubahatisha, kwasababu zipo kazi za kutosha na tayari nimeajiri watu wa kusambaza kazi zangu na kusimamia kila kitu katika biashara yangu ya muziki, tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo nilikuwa nafanya kazi kivyangu.

Ndani ya mwezi huo, natarajia kuachia singo yangu ya ‘Kacheze Unapochezaga’, ambayo inazungumzia matukio mbalimbali nilipokuwa sisikiki, kwani wapo watu wengi walinikimbia na wengine walinipa moyo.

BINGWA: Unazungumziaje suala la aliyekuwa mke wako, Sandra kukamatwa na dawa za kulevya nchini China?

Z Anto: Sikuwahi kutaka kuzungumzia suala hili, lakini kifupi tu, wakati Sandra anakamatwa na dawa za kulevya nchini China, tulikuwa tuna takribani miaka mitatu tumeachana.

Nakumbuka siku moja kabla ya kwenda China alinipigia simu akiniomba msamaha kwamba nimsamehe kwa kila kitu alichonifanyia na kwamba anaomba nikunjue roho yangu ili afanikiwe katika safari hiyo.

Nilimwambia kuwa sina tatizo lolote, hivyo akasafiri kuelekea nchini humo, baada ya muda mfupi nikasikia kwamba amekamatwa na dawa za kulevya.

BINGWA: Mkiwa kwenye uhusiano wenu, ulikuwa unajua kwamba Sandra alikuwa anashughulika na ishu za madawa.

Z Anto: Tangu mwanzo nilikuwa najaribu kutumia nafasi yangu kuvunja ukaribu wake na Cliff Patrick ‘Jack’, kwani nilikuwa nimeshapata taarifa zake kujihusisha na ishu za madawa, lakini hakunielewa.

Biashara hizo naweza kusema kuwa ndicho chanzo cha mahusiano yetu kuvunjika, kwani Sandra hakuelewa jambo lolote nililokuwa namweleza akaendelea kuwa karibu na Jack.

BINGWA: Katika kipindi Sandra akiwa jela nchini China, mmewahi kuwasiliana?

Z Anto: Yaah! Kipindi yuko jela aliwahi kunitumia barua ambayo alikuwa anazidi kuniomba radhi kwa kutofuata kile nilichokuwa namwambia… niliumizwa sana na barua hiyo.

Toka barua hiyo nilikuwa napata taarifa kwamba kuna barua yangu imekuja, lakini familia yake hawakutaka kunipa.

BINGWA: Ikitokea akaachiwa na kurudi hapa nchini, akikuomba msamaha mrudiane kwenye mahusiano, utakubali?

Z Anto: Nilimsamehe, lakini kurudiana kimahusiano haiwezekani kabisa.

BINGWA: Kitu gani kulisababisha ukaikimbia Tip Top Connection?

Z Anto: Kikubwa zilikuwa tofauti za kibiashara, kwani mkataba ulikiukwa, hasa kutokana na mauzo ya albamu yangu ya Binti Kiziwi, ambayo ilivunja rekodi kwa wakati huo na kipindi hicho nilikuwa nafanya ziara yangu nje ya nchi.

Cha kustaajabisha niliporudi nchini na kwenda kwa Mhindi kuangalia fedha zangu, nilikuta uongozi umeshachukua fedha nyingi sana bila ya mimi kujua lolote.

Yote tisa, kumi, nikiwa kwenye shoo Kenya nikapigiwa simu kwamba bosi Abdul Bonge na Madee wameandaa tamasha Burundi, hivyo niende nchini humo kuungana nao watanirudishia gharama zangu.

Al-hamdulillah watu walifurika uwanja mzima, kwani ilifanyika katika uwanja wa mpira, lakini cha kushangaza tunarudi nikaambiwa hakuna faida yoyote iliyopatikana kwenye shoo ile, hivyo sikupata hata thumuni, ikabidi nijiengue tu kiaina.

BINGWA: Bifu lako na Babu Tale lilianzia wapi?

Z Anto: Mimi na Tale tofauti zilianza mwanzoni kabisa wakati ndio natoka, ambapo alikuwa anataka niachie video kwanza halafu ndio audio ya wimbo, kitu ambacho binafsi nilikikataa kabisa.

Nilifanya hivyo kwasababu maisha niliyokuwa nimetoka bado yalikuwa magumu, nikasema nikitangulia kuachia video halafu naendelea kuishi mazingira yale kitaani itanisumbua.

Lakini bosi aliendelea na msimamo wake na mimi nikawa na wa kwangu, ikafikia hatua tukawa hatuongei kabisa mpaka akamwambia Abdul Bonge kwamba hawezi kusimamia kazi zangu nina kiburi.

Mwisho wa siku niliamua kuondoka Tip Top ambapo Bonge alimtuma Madee kunifuata nyumbani na baada ya kurudi tena hatukuwa tunaongea. Tale nimekuja kuongea naye siku narekodi nyimbo ya ‘Binti Kiziwi’ baada ya kuambiwa na Bonge anisimamie studio alikuwa na kazi nyingine.

BINGWA: Kitu gani kilikupoteza baada ya kutoka Tip Top?

Z Anto: Kipindi ambacho nilionekana nimepotea, kuna mambo yalikuwa yananikwamisha ikiwa ni pamoja na kupeleka nyimbo zangu, baadhi ya watu kutoka katika uliokuwa uongozi wangu wanakwenda kuzizuia zisipigwe redioni.

Hivyo nilipogundua suala hilo nilijipanga kwa nguvu zangu mwenyewe hadi nilipoachia ‘Kisiwa cha Malavidavi’, ikasimama na kufanya vyema sokoni, ambapo baada ya hapo niliamua kufanya shughuli nyingine mbali na muziki.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU