PLUIJM, YANGA KUNA KITU

PLUIJM, YANGA KUNA KITU

5754
0
KUSHIRIKI

NA MICHAEL MAURUS

KUNA kitu si bure. Huna haja ya kusita kusema hivyo kutokana na kile kinachoonekana baina ya watu wa Yanga na kocha wao wa zamani, Hans van der Pluijm.

Kwa wale waliobahatika kufika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi kushuhudia mechi ya kirafiki baina ya Yanga na Singida United, wanaweza kuwa mashahidi wa hilo.

Mara baada ya Pluijm kuingia uwanjani wakati kikosi chake cha Singida kikiingia kupasha, mashabiki wa Yanga walimshangilia mno Mholanzi huyo.

Kitendo hicho kilionekana kumgusa mno Pluijm ambapo naye aliwapungia mikono, akifanya hivyo kwa muda mrefu kabla ya kukaa katika nafasi yake.

Mashabiki wa Yanga kumshangilia zaidi Pluijm badala ya kocha wao wa sasa, George Lwandamina, maana yake ni kwamba bado wanamkubali Mholanzi huyo pamoja na kuondoka Jangwani kuliko ilivyo kwa Mzambia wao huyo.

Hivyo, mashabiki wa Yanga wapo tayari kumuona kocha wao huyo aliyewapa mataji mawili ya Ligi Kuu Tanzania Bara, akirejea Jangwani wakiamini ndiye ‘mwarobaini’ wao wa makombe.

Kwa upande wa Pluijm, naye inaonekana kuna kitu moyoni mwake dhidi ya Yanga. Ni kama vile bado hakubali alistahili kuondolewa Jangwani akitamani kurejea katika nafasi yake.

Kwa waliofika Uwanja wa Taifa juzi, bila shaka watakubali kuwa Pluijm alikuwa na furaha isiyo kifani pale timu yake ilipokuwa ikiongoza kwa mabao 2-1 dhidi ya Yanga, akifahamu kuiliza timu yake hiyo ya zamani ndiyo ‘golden chance’ yake ya kurejea Jangwani.

Kwa muda wote ambao timu yake ya Singida United ilikuwa mbele, lakini pia kandanda la hali ya juu lililoonyeshwa na vijana wake waliokuwa wakishangiliwa vilivyo na mashabiki wa Simba, Pluijm alikuwa na furaha mno.

Alikuwa akisimama na kuzunguka hapa na pale katika eneo lake la kujidai la benchi la ufundi, huku muda wote akiwa anatabasamu akifahamu kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuwafanya mashabiki wa Yanga kupandwa na hasira na mwisho wa siku kumpigania ili arejeshwe kundini.

Hata hivyo, mwisho wa siku Yanga ilishinda kwa mabao 3-2, kitendo kilichoonekana kumnyong’onyesha Pluijm kwa kiasi fulani, japo bado aliondoka uwanjani akijivunia soka lililoonyeshwa na vijana wake waliowafunika kabisa mastaa wa Jangwani.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU