NAUNGA MKONO WAZO LA KUANZISHA MFUKO WA WASANII

NAUNGA MKONO WAZO LA KUANZISHA MFUKO WA WASANII

376
0
KUSHIRIKI

NA CHRISTOPHER MSEKENA

NILIPATA fursa ya kuhudhuria kikao cha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe na wasanii, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam Agosti 3, mwaka huu.

Nilitegemea nitakutana na wasanii wengi, hasa wale ambao malalamiko yao huwa wanayaandika kwenye mitandao ya kijamii, lakini haikuwa hivyo, niliokutana nao ni walewale ambao wamezoeleka na wengine hawana majina makubwa.

Licha ya uchache wa wasanii waliohudhuria mkutano ule, uliokuwa unawahusu moja kwa moja, sitasahau mipango na mikakati kabambe ambayo Dk. Mwakyembe aliiweka hadharani mbele ya wasanii wachache na wadau wengine wa sanaa waliohudhuria.

Mosi, Waziri aliteua wasanii wanaounda kamati ya kushughulikia masuala yanayowakabili wasanii, likiwamo suala la sera na sheria, ili kuboresha maslahi ya msanii mmoja mmoja na katika kamati hiyo iliundwa na wasanii kama Nikki wa Pili, Azma Mponda, Witness Mwaijanga na mtangazaji Taji Liundi.

Sina shaka na kamati hiyo, ninachosubiri kuona ni utendaji kazi wake, ambao utaleta matokeo mazuri endapo wasanii wenyewe wataiunga mkono na kuipa ushirikiano katika kusimamia yale maazimio ambayo yatakuwa na tija kwenye tasnia nzima ya sanaa.

Lakini pia mbali na kuteua kamati hiyo, Dk Mwakyembe aliwataka wasanii wa muziki kuunda mfuko ambao utakwenda kutatua changamoto za udhamini wanazokutana nazo katika kazi zao.

Wasanii wamekuwa hawana mitaji ya kufanya kazi zao katika ubora mkubwa, hali hiyo imefanya kuwe na wasanii wachache pekee ambao wanaweza kumudu gharama kubwa wanazozitoa kwenye uandaaji wa kazi zao.

Waziri Mwakyembe alisema kutokana na malalamiko yanayotokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wasanii, ambazo nyingi zinasababishwa na mikataba inayowanyonya kwenye kazi zao, ni vema sasa wasanii hao kupitia chama chao cha Tanzania Urban Music Association (TUMA), kuanzisha mfuko ambao utakuwa unatoa mikopo kwa wasanii ili kuwezesha utendaji wa kazi zao pasipo kutegemea wadhamini.

Namnukuu: “Ninafikiri dawa tunayohitaji ni kuanzisha mfuko wa wasanii ambapo kila msanii atatakiwa kuchangia fedha. Jambo ambalo litawavutia wadau wengine kuchangia mfuko huo na kuwaondoa dhana ya utumwa na mfuko huo utamsaidia msanii aliyejisajili kupata mkopo bila kutozwa riba yoyote,” alisema.

Hali za kiuchumi za wasanii zinatofautiana, kuna wasanii wanaweza kufanya video popote pale kwa sababu wana mitaji ya kutosha, lakini kuna wengine hawana uwezo huo. Hawawezi kufanya audio na video kubwa bila kupitisha bakuli kwa wadau ili apate fedha ya video.

Bila shaka kuanzishwa kwa mfuko huo kutapunguza kadhia hiyo ya wasanii wasio na uwezo kuombaomba. Lakini mbali na huo mfuko kuwasaidia kwenye kazi, pia unaweza kuwa msaada mkubwa wasanii wanapokutana na changamoto za kiafya zinazohitaji fedha nyingi.

Aidha, Mwakyembe alisema kuwa, tasnia ya sanaa ina mchango mkubwa katika kuongeza pato la Taifa, hivyo akaonyesha kiu yake ya kutaka sanaa irasimishwe, ili kupunguza tatizo la ajira na pia kutumika kama chombo maalumu cha kuielimisha jamii kwa kuwa kupitia sanaa jamii inapata ujumbe kwa urahisi.

Hili ni wazo zuri ambalo litakwenda kuongeza ufanisi wa kazi za sanaa, kwa kuwa msanii anakuwa anayo sehemu ya kukimbilia anapokwama kimtaji, sanaa ni kazi na wenzetu wanawekeza fedha nyingi, ndiyo maana inawalipa, hivyo sisi tusione tabu kuunda mfuko utakaotatua changamoto ya mitaji.

Iwe hivyo kwenye muziki na filamu, hali kadhalika katika sanaa nyingine.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU