DUNIA YA MKE WANGU

DUNIA YA MKE WANGU

551
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia

Alielekea upande wa dereva ambapo hakumuona mtu yeyote zaidi ya damu zilizokuwa kwenye kiti zikionyesha kuwa zilimwagika wiki mbili zilizopita.

Aligeuza na kupiga hatua kuelekea nyuma ya lori. Wakati huo moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali kupita siku zote. Alihisi yuko kwenye mateso makubwa yasiyokuwa na mfano. Alianza kumuomba Mungu pindi alipokuwa akipiga hatua za uoga kuelekea nyuma ya lori. Moyo wake ulisema kuwa unaomba umuone Julia ndani ya gari hilo hata akiwa maiti.

SASA ENDELEA

Alipofika nyuma, ambako kulikuwa na turubai, alisimama kwa dakika mbili. Kisha alihema, akashusha pumzi na kuipandisha. Kwa shauku ya uoga huku akitetemeka mithili ya mtu aliyeogeshwa maji ya barafu, Kai alifunua turubai na kukuta mtu akiwa amelala ndani ya lori, mwishoni kabisa.

Upesi alipanda na kuingia, alipiga hatua za taratibu kumfuata yule mtu aliyekuwa amelala kama mfu. Moyo wake ulimdunda na kuwasha taa ya hatari. Alimkuta mtu huyo akiwa amejifunika shuka kuanzia miguuni hadi usoni.  Alimfunua taratibu huku akitokwa na machozi mengi. Kwa kuwa akili yake iliamini yule alikuwa ni mkewe na si mtu mwingine.

Kai alishtuka kwa nguvu baada ya kuiona sura ya mke wake. Hakuamini kabisa. Alimtazama usoni kwa huzuni kubwa huku akibubujikwa na machozi yasiokatika. Alishindwa kujizuia alilia kwa sauti akijua ameipata maiti ya mkewe.

Alishangaa kuona Julia akishtuka na kuinuka. Macho yake yaligongana na macho ya Julia. Wote walibaki wanatazamana wasiamini mara moja kile wakionacho.

“Juliaaaaaa!” aliongea Kai kama chizi.

“Kaiiii! Alijibu Julia huku akihema.

Mke na mume wanaopendana pasipo mfano walitazamana wasiyaamini macho yao tena. Kai alimkumbatia Julia kwa nguvu huku akilia kama mtoto mdogo. Julia naye alimshika Kai vilivyo asitake kumuachia mara moja.

“Mke wangu!” aliongea Kai.

“Mume wangu!? alijibu Julia.

“Ni wewe kweli?” aliuliza Kai huku akirudi kumtazama Julia usoni na kumkumbatia tena.

“Ni mimi mume wangu.”

“Asante Mungu siamini huu ni muujiza. Mke wangu u mzima?”

“Nisamehe mume wangu naomba unisamehe,” aliongea Julia akilia kilio kikuu.

“Shiiiiii hujanikosea mpenzi nyamaza usilie kwa ajili ya hilo. Bali lia kwa furaha kwa kuwa umeniona mumeo,” aliongea Kai huku akimfuta machozi Julia.

Walitazamana usoni. Kai aliupeleka mdomo wake ili kumbusu Julia. Julia alirudisha uso nyuma akikataa kupewa busu hilo.

“Nini tena mke wangu?” aliuliza Kai kwa huzuni.

“Mume wangu mimi ni mwathirika.”

“Najua na sijali kuambukizwa,” aliongea Kai na kumbusu Julia kinguvu.

Hisia kali za mapenzi zilimchukua Julia na kumpeleka paradiso, paradiso  aliyokuwa ameikosa kwa muda mrefu. Alishindwa kuutoa mdomo wake kutoka kwa Kai maana alishakuwa amezidiwa na kutulia mithili ya maji kwenye mtungi. Alihisi raha isiyoelezeka, baada ya kupewa busu na mumewe.

Baada ya dakika moja, Julia aliutoa mdomo wake, kwa  hasira alimpiga Kai kibao.

“Nimekwambia mimi ni mwathirika huwezi kufanya hivyo,” aliongea Julia huku akitokwa na machozi.

Kai alitabasamu akatikisa kichwa na kumtekenya Julia. Julia alicheka kwa huzuni huku akiona aibu. Lakini baadae alionyesha sura ya umakini. Alimtazama Kai kwa muda na kumwambia.

“Mume wangu nashukuru nimekuona kabla sijaondoka duniani…”

Kabla hajamalizia sentensi yake, Kai alimkatisha kwa kumpiga  tena busu takatifu. Alimbeba kwa mikono yake miwili na kumtoa mle ndani ya lori. Alipiga hatua kuelekea kwenye gari alilokuja nalo, huku akitazamana na mkewe aliyekuwa ameishiwa nguvu kutokana na kuto kula chochote tokea jana.

Alimuingiza kwenye gari. Alikaa karibu naye na kumlaza kwenye kifua chake. Alichukua kopo la juisi na kuanza kumnywesha. Julia alikunywa haraka akiivuta kwa kasi maana njaa ilikuwa inakaribia kumuua. Kai alimlisha chakula kama mtoto mdogo anayeanza kuota meno huku akitabasamu muda wote.

“Nataka umalize vyote hivi,” aliongea Kai kwa machozi akimtania mkewe aliyekuwa akila kwa pupa huku naye akibubujikwa na machozi.

Baada ya kula, Julia alipata nguvu. Baadae Kai alishtuka baada kuliona jeraha liliokuwa kwenye bega la mkewe.

Nini kitaendelea? Usikose alhamisi

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU