SIKILIZIA HAYA KUTOKA LIVERPOOL EPL 2017-18

 SIKILIZIA HAYA KUTOKA LIVERPOOL EPL 2017-18

417
0
KUSHIRIKI

MERSEYSIDE, England

HUKU dirisha la usajili la majira ya kiangazi likielekea kufungwa, Liverpool hawajaonekana kuwa bize sokoni.

Ni Mohamed Salah pekee aliyeingia akiwa na uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza. Liver imeshindwa kuwasajili Virgil van Dijk na Naby Keita ambao imekuwa ikiwafukuzia tangu kuanza kwa majira ya kiangazi.

Hivi karibuni, Jurgen Klopp, alisema hana mpango wa kusajili beki wa kati, kauli inayoashiria kuwa ameachana rasmi na mpango wa kumchukua Van Dijk wa Southampton.

Liver wamepangwa kucheza na Hoffenheimn ya Ujerumani katika mchezo wa kuwania tiketi ya kwenda Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kibarua hicho ni mbali na kile cha kumzuia Philippe Coutinho kuondoka Anfield hasa baada ya Barcelona kuonekana kuing’ang’ania saini ya Mbrazil huyo.

Keshokutwa Liver wataanza msimu wa 2017-18 wa Ligi Kuu England (EPL) kwa kuvaana na Watford na siku tatu baadaye watakiwasha na Hoffenheimn ya Bundesliga.

Kwa kuitazama Liver ya Klopp, haya ni baadhi ya mambo yanayoweza kukitokea kikosi hicho msimu ujao.

Roberto Firmino kufunga mabao 20

Kwa mara ya mwisho mchezaji wa Liver kufunga mabao 20 ilikuwa ni miaka mitatu iliyopita.  Ulikuwa ni msimu wa 2013-14 ambapo Luis Suarez alifunga mabao 31 na Daniel Sturridge akaweka 21.

Msimu uliopita, Sadio Mane aliweka 13, Firmino akatupia 12 na Divock Origi akawa na 11.

Msimu ujao, Firmino anaonekana kuwa ataweza kufuta rekodi hiyo chafu hasa baada ya kukabidhiwa jezi namba 9 huku Salah akipewa namba 11.

Mbrazil huyo amekuwa kwenye kiwango kizuri katika mechi za ‘pre-season’, ambapo alizitungua Atletico Madrid na Athletic Bilbao.

Kwa upande mwingine, taarifa za juzi zimedai kuwa wakala wake, Roger Wittmann, ameonekana mjini Barcelona, lakini haikuelezwa kuwa amekwenda kushughulikia uhamisho wa nyota huyo kujiunga na Barca.

Liver kuvuka makundi Ligi ya Mabingwa

Msimu uliopita, walitinga ‘top-four’ na kuziacha Arsenal na Manchester United zikiwa nje.

Soka la kushambulia kwa kasi la Liver linaweza kuwa faida kwao mbele ya timu yoyote. Ni kama walivyoonyesha walipoichapa Bayern Munich mabao 3-0 katika mchezo wa pre season uliochezwa Ujerumani kwenye Uwanja wa Allianz Arena.

Taarifa njema kwa mashabiki wa Anfield ni kwamba, straika hatari wa Hoffenheim, Sandro Wagner, haonekani kuwa fiti kuelekea mchezo wao wa Agosti 15.

Mpachikaji mabao huyo wa kimataifa wa Ujerumani ambaye alipasia nyavu mara 11 msimu uliopita, alicheza kwa dakika nane tu katika mchezo uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kati ya Hoffenheim na Bologna kutokana na majeruhi ya ‘enka’.

Majeruhi kuendelea kuitesa

Kuelekea msimu ujao, tayari Klopp ameshaongeza mtaalamu wa afya kwenye chumba cha kubadilishia. Hiyo ni baada ya kikosi chake kuteswa na majeruhi msimu uliopita.

Kwa misimu miwili iliyopita, nahodha Jordan Henderson, hajacheza kwa dakika 90 katika zaidi ya mechi 30 za Ligi Kuu England.

Tayari kikosi hicho kitawakosa Nathaniel Clynena, Adam Lallana, katika mechi za awali na Daniel Sturridge hakucheza mechi mbili za mwisho msimu uliopita.

Mabeki Dejan Lovren na Joel Matip, wamekuwa wakikaa nje mara kwa mara wakiuguza majeraha.

Huenda Klopp akalazimika kuwageukia makinda Trent Alexander-Arnold na Ben Woodburn, jambo ambalo litakuwa hatari  kutokana na uzoefu mdogo walionao.

Klopp anapaswa kusajili wachezaji wapya wawili ili kuweza kukabiliana na majanga hayo msimu ujao.

Beki kimeo kuisumbua tena

Msimu uliopita, Liver waliruhusu mabao 40. Tangu kuondoka kwa kocha Kenny Dalglish katika msimu wa 2011-12, Liver imekuwa ikiruhusu mabao mengi katika kila msimu.

Tangu kutimka kwa Dalglish, msimu ambao Liver walimaliza ligi wakiwa nafasi ya nane, timu hiyo imeruhusu mabao 50 mara mbili.

Klopp ameshindwa kumchukua Van Dijk ambaye amekuwa akifanya kazi nzuri katika safu ya ulinzi ya Southampton.

Msimu uliopita, kukosekana mara kwa mara kwa majeruhi Lovren na Matip, kulikuwa tatizo kubwa kwenye eneo la beki wa kati.
Liver wanakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Chelsea ambayo pia inamtolea macho Van Dijk mwenye umri wa miaka 25.

Hata hivyo, Southampton wameendelea kushikilia uamuzi wao wa kutomuuza beki huyo wa kimataifa wa Uholanzi, ambaye anatajwa kuwa na thamani ya pauni milioni 60.

Kuhakikisha safu yake ya ulinzi inakuwa sawa msimu ujao, Klopp anahitaji nguvu ya mlinzi huyo aliyewaambia mabosi wake wa sasa kuwa anataka kuondoka.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU