NANI KANG’ARA SIMBA DAY?

NANI KANG’ARA SIMBA DAY?

1924
0
KUSHIRIKI

NA MWANDISHI WETU

JUZI Jumanne ilikuwa ni Tamasha la Simba Day ambapo klabu hiyo ilipata fursa ya kujaribisha ‘mitambo’ yao waliyoinasa dirisha hili la usajili kwa ajili ya msimu ujao.

Katika tamasha hilo lililofanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Simba ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon Sports, ambapo walishinda bao 1-0.

Wachezaji wote wapya waliosajiliwa na Simba pamoja na wale wa zamani walipata nafasi ya kucheza katika mchezo huo.

Je, ni mchezaji gani kati ya wale wapya aling’ara katika mchezo huo wa Simba Day dhidi ya Rayon Sports?

Okwi

Emmanuel Okwi ambaye amesajiliwa kwa mara ya tatu katika klabu hiyo ya Simba, juzi alicheza kipindi kimoja na kufanikiwa kutoa pasi ya goli pekee la ushindi lililofungwa na Ibrahim Mohamed ‘Mo’, pia alipiga shuti moja ambalo lilichezwa na mlinda mlango wa Rayon Sports.

Pamoja na wengi kudhani kwamba atakuwa ameachwa na umri mkubwa, lakini Okwi alionyesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kuwatambuka mabeki na hata kuminyana nao huku akitumia akili ya hali ya juu.

Niyonzima

Haruna Niyonzima aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Okwi na katika dakika 45 alizocheza, kiungo huyo wa zamani wa Yanga alitengeneza nafasi nne za mabao.

Kama nafasi hizo zingeweza kutumiwa vizuri na Shiza Kichuya, ambaye mpira mmoja ulipanguliwa na kipa wa Rayon, kisha pasi nyingine aliikosa.

Nafasi nyingine mbili ilikuwa ni ya John Bocco na ya Muzamiri Yassin, ambapo kama zingetumika vizuri basi katika mechi hiyo moja angekuwa ametoa pasi nne za mabao.

Bocco

Ingawa hakuweza kufunga bao lolote na kupoteza nafasi kadhaa za mabao, lakini alionyesha kwamba akizoeana na wenzake ataweza kucheza vizuri na kusaidia Simba kwenye michuano mbalimbali.

Katika mchezo huo moja ya kitu kilichokuwa kivutio kwa watu ilikuwa ni jinsi ambavyo aliweza kutumia nguvu zake katika kuwania mipira na mabeki na kubaki nayo kusubiria wengine na jinsi alivyokuwa akiwakimbia mabeki.

Nyoni

Erasto Nyoni alionyesha kwamba Simba walifanya jambo la maana sana kunasa saini ya beki huyo wa zamani wa Azam FC.

Kwanza ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi na mwenye uzoefu mkubwa, kipindi cha kwanza aliweza kupiga krosi tano nzuri, kama washambuliaji wa Simba wangekuwa makini na kuzitumia vizuri basi wangeweza kushinda mechi hiyo kwa mabao mengi.

Pamoja na kusaidia safu ya ushambuliaji, lakini aliweza kutimiza majukumu yake kwenye kukaba na hata alipobadilishwa upande wa kushoto na kumpisha beki wa kulia, Ally Shomari, bado aliendelea kufanya vizuri.

Ally Shomari

Pamoja na kuingia dakika chache kwenye mchezo huo, lakini Ally Shomari, aliweza kuonyesha kwamba ni moja ya wachezaji wazuri ambao wamesajiliwa na klabu hiyo.

Gyan

Nicholas Gyan naye ni mchezaji mwingine aliyepewa nafasi ya kuonyesha mambo yake katika mechi hiyo, ambapo aliingia kuchukua nafasi ya Mo na kuonyesha uwezo wake na kuwatishia sana mabeki wa Rayon kutokana na kasi yake.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU