KUONDOKA NIYONZIMA KUNAUMA KULIKO AJIB

KUONDOKA NIYONZIMA KUNAUMA KULIKO AJIB

2357
0
KUSHIRIKI

Na mwandishi wetu

NI klabu gani kati ya Simba na Yanga imeumia sana kwa kuondokewa na mchezaji wao?

Mshambuliaji Ibrahim Ajib, amejiunga na Yanga akitokea Simba kwa dau la shilingi milioni 50, huku akipewa gari.

Huku kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, akiachana na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kutua kwa Wekundu wa Msimbazi kwa zaidi ya shilingi milioni 100.

Baada ya mashabiki wa Simba kuwa na hofu kubwa juu ya Niyonzima kusajiliwa na klabu hiyo, hatimaye juzi Jumanne kila kitu kuhusu Niyonzima kilikuwa wazi.

Katika siku hiyo ya Jumanne ambapo klabu ya Simba walikuwa wakiadhimisha tamasha lao la Simba Day linalofanyika Agosti 8 kila mwaka, Niyonzima alitambulishwa kwa mashabiki hao.

Katika utambulisho huo, ambapo Simba walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, Niyonzima alipata nafasi ya kucheza dakika 45 na kuwafurahisha sana mashabiki wa Simba.

Simba ilitambulisha wachezaji wengine kama Emmanuel Okwi, Nicholas Gyan, John Bocco, Aishi Manula, Ally Shomari, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na wengine wa zamani na wapya.

Takwimu

Katika mchezo huo wa kirafiki, Niyonzima aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Okwi, ambapo alifanikiwa kuonyesha uwezo mkubwa.

Pamoja na Niyonzima kuonekana kutokuwa fiti kwa kuwa alichelewa kuungana na wenzake, lakini mambo kadhaa aliyofanya uwanjani yalitosha kuonyesha kwamba ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na ataisaidia sana Simba kwenye Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ukiachana na mbwembwe alizoonyesha kwa kupiga ‘outer’ mbili zilizoamsha shamrashamra katika mchezo huo, pia Niyonzima aliweza kutengeneza nafasi nne za mabao.

Moja ya nafasi hiyo alimtengenezea Shiza Kichuya ambaye alipiga shuti lililookolewa na mlinda mlango wa Rayon.

Mwingine aliyetengenezewa nafasi nzuri ya bao ni Bocco na Muzamiri Yassin, ambao wote walishindwa kutumia nafasi hizo kabla ya Kichuya kupoteza nafasi nyingine.

Kwa takwimu hizo na jinsi Niyonzima alivyocheza katika mechi hiyo, jambo lililowazi kwamba mashabiki wa Yanga walitoneshwa kidonda ambacho kilionekana kupona baada ya kutambuliswa kwa Ajib.

Kwani Ajib naye alipata nafasi ya kuonyesha uwezo wake katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United, mchezo ambao Yanga walishinda mabao 3-2.

Kwenye mchezo huo uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, Ajib aliweza kupiga mashuti mawili, ambapo moja lilipaa pembeni ya lango na jingine kuzuiwa na mabeki wa Singida United.

Zaidi ya mashuti hayo mawili aliyopiga Ajib, hakukuwa na kingine kwa upande wa takwimu zaidi ya kuonyesha ufundi wake wa kuchezea mpira ingawa alicheza dakika nyingi zaidi ya Niyonzima.

Uzoefu

Kingine kilichoonekana ni uzoefu wa wachezaji hao wawili, ambapo Ajib alionekana kutekwa na kelele za mashabiki wakati Yanga wanacheza na Singida United na kupoteza mwelekeo na kusahau mambo muhimu uwanjani na kuanza kucheza na mashabiki badala ya kutoa ushirikiano kwa wenzake.

Hilo lilikuwa tofauti kwa Niyonzima, kwani pamoja na kushangiliwa na mashabiki ila aliendelea kufanya majukumu yake na ndio maana aliweza kutengeneza nafasi hizo nne za mabao.

Uzoefu huo wa kumudu presha ya mashabiki uwanjani ulioonyeshwa na Niyonzima, unatokana na kupita kwake kwenye klabu nyingi kama Rayon Sports FC na APR zote za Rwanda, Yanga kisha Simba.

Hilo liko tofauti kwa upande wa Ajib ambaye timu yake ya kwanza kubwa kuichezea ni Simba na sasa ndio amejiunga na Yanga.

Hata ukiangalia kwa upande wa timu za taifa, Niyonzima ameweza kucheza mechi nyingi zaidi tofauti na Ajib ambaye amekuwa akiitwa na kuachwa na hata anapoitwa ni mara chache kupata nafasi ya kucheza.

Hivyo ni wazi kabisa kwamba, Simba watanufaika na uzoefu wa Niyonzima kwenye Ligi Kuu na mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.

Mataji

Niyonzima ana kismati cha mataji, kwani mwaka wake wa kwanza kujiunga na APR  (2007) alisaidia timu hiyo kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu, kisha wakafanya hivyo mwaka 2009, 2010 na 2011.

Kama alivyobeba mataji ya Ligi Kuu Rwanda mara nne, hicho ndicho kilichotokea Yanga ambapo tangu atue amebeba mataji manne pia.

Mataji hayo manne ya Ligi Kuu Tanzania Bara ni ya msimu wa 2012/13, 2014/15, 2015/16 na 2016/17.

Hilo liko tofauti kwa Ajib, kwani tangu aanze kucheza soka mataji yake makubwa ni lile la Banc ABC Super akiwa na Simba B, kabla kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania msimu uliopita.

Umri

Moja ya kitu pekee ambacho Yanga watajivunia kwa Ajib ni umri wake, mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya ushambuliaji na kiungo, ana umri wa miaka 21.

Hivyo bado ana muda mrefu wa kuichezea Yanga kutokana na umri wake huo aliokuwa nao.

Niyonzima ana umri wa miaka 27, ingawa ana uwezo wa kucheza zaidi ya misimu mingi na yeye, lakini kutokana na umri huo hataweza kuzidi zaidi ya misimu minne.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU