MWAKALEBELA AAHIDI KUENDESHA SOKA KIBIASHARA

MWAKALEBELA AAHIDI KUENDESHA SOKA KIBIASHARA

381
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

MGOMBEA wa nafasi ya rais katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, amesema akipewa ridhaa ya kuongoza shirikisho hilo ataufanya mpira kuwa biashara na si burudani pekee.

Uchaguzi Mkuu wa TFF unatarajiwa kufanyika kehokutwa mkoani Dodoma, ambapo wagombea sita watawania nafasi ya urais.

Akizungumza wakati akizindua kampeni zake jana katika Ukumbi wa Hoteli ya Double View jijini Dar es Salaam,  alisema sasa umefika wakati wa soka la Tanzania kuwa biashara yenye faida kwa Taifa licha ya kutambulika kama burudani kwa jamii.

Alisema ili kufanikisha hilo, akichaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu ataanza kuunda uongozi mpya utakaotawaliwa na utawala bora ili kila chombo kiweze kufanya kazi kwa ufanisi na pia kuhakikisha miundombinu ya soka inakuwa bora.

“Lazima tuwe na miundombinu bora kama tunataka kucheza soka, lakini hatuna mafanikio na tunajua hali ya viwanja vyetu, haya ni miongoni mwa mambo ambayo nitayafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa.

“Nimesikia sera kadhaa watu wanazungumza mambo ya kufikirika, lakini mimi nilijipima nikiwa katibu mkuu wakati wa rais Leodegar Tenga, hivyo najua nini cha kufanya ili mambo yaende na kuleta mafanikio,” alisema.

Mwakalebela aliongeza kuwa wakati akiwa katibu mkuu wa TFF walifanya mambo mengi ikiwamo kupata wadhamini na kuanzisha mashindano ya soka la vijana ambayo kwa sasa mengi yamekufa.

“Kila kitu kinawezekana Tanzania hususani katika mpira wa miguu, hivyo ninaomba ridhaa ya wapiga kura ili niweze kuongoza TFF kwa miaka minne ijayo na ninawaahidi nitaendeleza yale niliyoyafanya wakati nikiwa katibu mkuu TFF kuanzia mwaka 2006 hadi 2010,” aliongeza Mwakalebela.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU