BARCELONA WAKIMTAKA MRITHI WA NEYMAR LAZIMA KIBUBU KIVUNJWE

BARCELONA WAKIMTAKA MRITHI WA NEYMAR LAZIMA KIBUBU KIVUNJWE

343
0
KUSHIRIKI

Buy-FC-Barcelona-Football-Tickets-FootballTicketNetCATALONIA, Hispania

HIVI sasa inaonekana wazi mchezaji yeyote ambaye atatua Barcelona kuchukua nafasi ya Neymar ataigharimu timu hiyo kiasi kikubwa cha fedha licha ya kutomaliza hata mwezi tangu wapokee euro milioni 222 za uhamisho wake kwenda PSG.

Licha ya kwamba watu wengi wanaona ni kitu chepesi kwa Barca kumpata mchezaji wanayemtaka kisa wana hela nyingi, lakini ukweli unadhihirika kuwa si kitu chepesi, hadi sasa ofa zao kila wanapoziwasilisha mezani zinakataliwa.

Hivi karibuni rais wa klabu hiyo, Josep Maria Bartomeu, alisema hatathubutu kutumia ovyo fedha zilizoingia kwenye akaunti, lakini presha inayotoka kwa mashabiki ambao wanataka mchezaji wa maana wa kumrithi Neymar inaonekana kumzidi.

Kila kitu kinawezekana na kama Liverpool wakilegeza kamba, ina maana Phillipe Coutinho atatua Barca na kuwa mchezaji wa gharama zaidi Hispania.

Barca hawana budi kutumia fedha nyingi kumpata staa wanayemtaka kwani waliyempoteza ni mzito. Hawatakuwa na jinsi kwani hivi sasa wapinzani wao, Real Madrid wameshaanza kurudi kwenye ufalme na kuwakamata haitakuwa kazi rahisi.

Mapema wiki hii, mtandao wa BBC uliripiti kuwa Liverpool ilizifumbia macho euro milioni 100 kama ofa ya kumwachia Coutinho.

Wakati kukiwa na tetesi kwamba klabu ziko kwenye mazungumzo, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, yeye ameendelea kuwa na msimamo wake ule ule kwamba Coutinho hauzwi, hofu yake ikiwa ni kumpoteza mchezaji muhimu katika msimu huu mpya na kukiwa na jukumu la kufanya vizuri Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Aidha, Coutinho anayo nafasi ya kuomba auzwe lakini hadi sasa hajaonesha dhamira ya kufanya hivyo.

Dembele…

Wakati Coutinho akiendelea kuwa mjadala mzito, Barca pia wanatajwa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Dortmund, Ousmane Dembele, ambaye hadi kufikia jioni ya juzi Alhamisi, mwandishi wa SkySports, Kaveh Solhekol, alinukuu taarifa za Ujerumani kuwa kinda huyo alikuwa safarini kuelekea Barcelona.

Dembele alizua mtafaruku nchini Ujerumani. Alianza kwa kugombana na mwenzake mazoezini (kama ilivyokuwa kwa Naby Keita na Neymar), halafu baadaye ikataarifiwa hakufika katika kambi ya mazoezi ya Dortmund na simu yake haikupatikana hewani.

Huyo naye ataigharimu Barca takribani euro milioni 100! Je, watathubutu kutumia euro milioni 200 kwa wachezaji hao? Kama wana nia watafanya kweli, lakini kama wanabipu, huenda wakawakosa wote iwapo watafanya masikhara.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU