DANNY ROSE KAWACHANA ‘LAIVU’ SPURS, WAMEZIDI UBAHILI KWENYE MSHAHARA

DANNY ROSE KAWACHANA ‘LAIVU’ SPURS, WAMEZIDI UBAHILI KWENYE MSHAHARA

329
0
KUSHIRIKI

download (2)LONDON, England

MAPEMA wiki hii beki wa kushoto wa klabu ya Tottenham, Danny Rose, aliibuka na malalamiko kwa klabu yake hiyo kuhusu mshahara kiduchu wanaowapa tofauti na klabu nyingine za EPL zinavyowalipa nyota wao.

“Ninastahili mshahara wa kueleweka zaidi ya huu wa sasa,” yalikuwa maneno ya Rose alipohojiwa, kauli iliyozua tafrani katika uwanja wao wa mazoezi, Enfield.

Beki huyo wa kushoto wa kikosi hicho cha kocha Mauricio Pochettino, anaaminika kupokea mshahara wa pauni 65,000 kwa wiki, lakini kwa uwezo wake na timu itakayomsajili bila shaka itampa mara mbili au tatu ya mshahara huo.

Kwa mfano, Rose amepitwa mbali na Luke Shaw wa Manchester United ambaye ndiye beki wa kushoto anayelipwa vizuri zaidi EPL, akikusanya pauni 130,000 kila wiki.

Mwezi uliopita, Man City ilimsajili beki wa kushoto, Benjamin Mendy, kutoka Monaco kwa kitita cha pauni milioni 52 na inaaminika atalipwa mshahara wa pauni 100,000 kwa wiki hapo bila kujumuisha nyongeza.

Rose kila akiangalia wenzake wanavyokusanya mipunga ya maana kila wiki, akili yake inachanganyikiwa. “Kwenye maisha kama ukijiona unastahili zaidi, kwanini ung’ang’anie kwenye kidogo?” Rose aliliambia gazeti la The Sun.

“Mie si wa namna hiyo. Nitahakikisha napata ninachostahili. Naijua thamani yangu. Kama wenzangu walivyo hapa Spurs, kwa maoni yangu nastahili zaidi ya nikipatacho.”

Ndani ya kikosi cha Tottenham, wachezaji wanaolipwa zaidi ni mlinda mlango, Hugo Lloris na Harry Kane, wote wakilamba pauni 100,000 kwa wiki.

Wakati kipa anayelipwa zaidi EPL, David de Gea wa Man United, anakusanya pauni 200,000 kwa wiki!  Mara mbili ya Lloris.

Aidha, mshambuliaji anayelipwa zaidi ni Sergio Aguero wa Manchester City (pauni 240,000), mara mbili zaidi ya Kane.

Tottenham pia ilimpoteza beki wao mahiri wa kulia, Kyle Walker, ambaye alitua City kwa kitita cha pauni milioni 50 na sasa Mwingereza huyo atakusanya mshahara wa pauni 150,000 kwa wiki huku aliyemrithi Spurs, Kieran Trippier, akilipwa pauni 65,000 kwa wiki.

Bado hawajaisha, Dele Alli, naye ni supastaa wa Spurs. Mara kadhaa amehusishwa na timu za Barcelona na Real Madrid.

Licha ya hivyo, Alli analipwa mshahara wa pauni 60,000 kwa wiki. Wakati viungo wengine kama Yaya Toure akilipwa pauni 220,000 na City. Paul Pogba yeye pale United anaweka mfukoni mshahara wa pauni 280,000 kwa wiki. Hapo ndipo Rose alipoanza kutokwa povu, inakuwaje yeye na wenzake walipwe kiduchu?

Wakati watu wengi wakimsifia mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy, kuwa ni fundi wa kusajili wachezaji wakali bila kelele nyingi, bado ameshindwa kuwalipa wachezaji wake mishahara minono kulingana na kazi kubwa wanayofanya uwanjani.

Na huenda akamweka Pochettino kwenye wakati mgumu wa kuchezesha kikosi hicho bila mabeki wake tegemeo wa pembeni msimu huu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU