DUNIA YA MKE WANGU

DUNIA YA MKE WANGU

373
0
KUSHIRIKI

BINGWA MCHORO HADITHI PG21.p.Ilipoishia

Hata hivyo, Serikali ya Ethiopia ilikuwa ikimfuatilia Kai. Taarifa ya Kai kutoka katika mji wa Amhara, ilishakuwa imewafikia viongozi wa nchi hiyo. Maofisa wa Serikali, walitumwa uwanja wa ndege kwenda kuonana na Kai. Walifahamu kila kitu juu ya yeye kumpata mkewe. Tayari walishakuwa wamethibitisha kuwa mke wake alikuwa anaumwa.

SASA ENDELEA

Kwa kuwa alichokuwa akikihitaji Kai ni kuona anaondoka yeye na mkewe katika nchi hiyo, alilikubali ombi lao. Walimsihi sana asiweze kuishtaki Serikali yao. Walijitetea kuwa mji wa Amhara ulikuwa hauingiliki ndio maana walishindwa kuwatoa madaktari na wauguzi waliokuwa katika mji huo.

Hata hivyo, maofisa hao wa Serikali, hawakujua kuwa Kai alikuwa akifahamu kuhusu mauaji yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo, kwa ruhusa ya Serikali ya kuwaua raia wote waliokuwa mpakani.

Maofisa hao walipeana mikono na Kai, baada ya kuhitimisha maongezi hayo. Wakati huo, ukaguzi mkali ulikuwa ukiendelea pale uwanjani kwa watu waliokuwa wakitoka katika nchi hiyo. Jeshi la umoja wa mataifa pamoja na lile la Umoja wa Afrika (AU), walikuwa kwenye operesheni hiyo wakihakikisha  binadamu yeyote mwenye virusi vya Ebola hatoki kwenye nchi hiyo.

Julia alikuwa kwenye mawazo makali akiwa pale mgahawani, akimsubiri Kai aliyekuwa amekwenda kukata tiketi ya ndege. Alizidi kujiuliza kuwa watatokaje kwenye nchi hiyo, kwa sababu ulinzi na ukaguzi uliokuwa pale uwanjani, ulikuwa ni mkubwa na usio mtazama mtu fulani.

Mamia ya watu walikuwa wakiikimbia nchi hiyo. Wageni wote pamoja na watu wa taifa hilo waliendelea kuhangaika pale uwanjani wakihangaikia usafiri. Usafiri ulikuwa wa tabu kwa kuwa kila mgeni alihitaji kuondoka katika nchi hiyo. Lilikuwa jambo gumu kwa raia wa nchi hiyo kupata viza za kuelekea kwenye mataifa mengine.

Hata hivyo, usafiri wa kwenda bara la Ulaya na Marekani, ulikuwa haupatikani kirahisi licha ya watu kupimwa virusi vya Ebola. Jiji la Addis Ababa lilikuwa katika hatari ya kuingiwa na ugonjwa huo kutokana na kupatikana kwa baadhi ya watu wakiwa na virusi hivyo. Tayari nusu nzima ya nchi ya Ethiopia ilikuwa na maambukizi ya kutisha.

Kai aliandaliwa nafasi ya kusafiri pamoja na mkewe. Hata hivyo serikali ya Uingereza ilikuwa imeiomba serikali ya Ethiopia kumtoa Kai na mkewe katika nchi hiyo. Kai yeye hakujua lolote kuhusu hilo, hakujua kuwa anaruhusiwa kurudi Tanzania kwa msaada wa serikali ya Uingereza, iliyoshinikizwa na umoja wa mataifa, kupitia chama cha wanasayansi.

Serikali ya Ethiopia ilijifanya inampa Kai msaada wa kutoka katika nchi hiyo. Ili kumfunga mdomo asiishtaki kuhusu kutelekezwa kwa madaktari waliokwenda nchini humo akiwemo mkewe.

Kai alikwenda kumfuata Julia kwenye ule mgahawa. Alimkuta mwenye huzuni na uwoga wa hali ya juu.

“Usijali mke wangu tunarudi nyumbani,” aliongea Kai akimtazama Julia kwa macho ya huruma.

“Naumia sana mume wangu, jinsi ambavyo nimekupa shida. Muda huu ilitakiwa tuwe London tukifurahia ujio wa watoto wetu. Ninapswa kuadhibiwa,” aliongea Julia akitokwa na machozi.

“Useme hivyo mke wangu, kila jambo linatokea kwa sababu maalumu. Mimi binafsi nakupongeza kwa ujasiri wako na upendo uliouonyesha kwa raia wa Ethiopia, jinsi ambavyo uliwaokoa wale watoto 10,000 kutoka Keneza. Ninaamini Mungu atakulipa,” aliongea Kai.

Julia alitokwa na machozi maana maneno ya mumewe yalikuwa yametengeneza bustani ya maua kwenye moyo wake. Upesi alimkumbatia Kai na kulia sana. Kai alimfariji mkewe kadri vile alivyoweza, japo huzuni iliyokuwa kwa Julia ilikuwa ni kubwa, kwa kuwa alijiona ni mwenye hatia kutokana na kumtaabisha mumewe aliyehangaika kumtafuta katika nchi hiyo.

“Inuka twende mpenzi,” aliongea Kai akimpa Julia mkono.

Julia aliinuka kwa tabu kutoka na uchovu wa mimba, pamoja na homa ya Ebola iliyoanza kumnyemelea kutokana na kuelekea kwenye hatua ya tatu ya kuugua.

Tayari ujauzito wa Julia ulikuwa ukitimiza miezi minne na wiki tatu. Hivyo usumbufu wa mimba ulianza kuwa  mkubwa. Watoto wake walicheza tumboni vile watakavyo, wasijue mateso aliyokuwa akikumbana nayo mama yao.

Maofisa wa Serikali walimwongoza Kai na Julia katika eneo la wasafiri wa kiserikali. Walifanikisha kuingia kwa Kai na Julia katika ndege inayokwenda Tanzania. Lakini pamoja na hayo, si kwamba Kai asingeruhusiwa kupita pale uwanja wa ndege. Angeruhusiwa hata kama angekuwa na Julia aliyekuwa mwathirika wa Ebola. Hii ni kwa sababu umoja wa mataifa ulishatoa amri kwa nchi hiyo kumlinda Kai na kumruhusu kwenda kokote kule. Lakini Serikali ilijifanya inamsaidia Kai ili asifichue yale aliyoyaona kwenye taifa hilo pindi alipoingia kumtafuta mkewe.

Nini kitaendelea? Usikose Jumatatu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU