HEKAHEKA DODOMA, MRITHI WA MALINZI AKISAKWA

HEKAHEKA DODOMA, MRITHI WA MALINZI AKISAKWA

305
0
KUSHIRIKI

downloadNA WAANDISHI WETU, DODOMA

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) linatarajia kupata safu mpya ya uongozi leo pale itakapofanya uchaguzi mkuu katika ukumbi wa Hoteli ya St. Gasper mkoani hapa.

Uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa katiba ya shirikisho, baada ya viongozi waliokuwa madarakani chini ya Rais Jamal Malinzi, kumaliza kipindi cha miaka minne.

Katika uchaguzi huo, nafasi ya rais inawaniwa na wagombea sita ambao ni Shija Richard, Fredrick Mwakalebela, Ally Mayay, Wallace Karia, Iman Madega na Emmanuel Kimbe, huku Mulamu Ng’ambi, Mtemi Ramadhani na Michael Wambura wakiwania nafasi ya makamu wa rais.

Wagombea wengine katika uchaguzi huo ni wajumbe wa kamati ya utendaji wanaounda Kanda 13 za mikoa ya Tanzania Bara.

Akizungumza jijini hapa jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Revocatus Kuuli, alisema awali wapiga kura walikuwa 132 lakini wameongeza watatu.

Kuuli alisema idadi ya wapiga kura hao imeongezeka kutoka mkoa mpya wa Songwe, hivyo watakuwa 135 ambao wanatoka katika vyama vya soka vya mikoa na vyama shirikishi.

Alisema vyama shirikishi ni pamoja na Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), Chama cha Soka la Wanawake (TWFA), Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA) na vinginevyo.

“Nafasi ya rais na makamu wake, mshindi atapatikana baada ya kupata asilimia 50 zaidi ya nusu ya wapiga kura kama ikishindwa kufikia asilimia hiyo, kura zitarudiwa kwa wagombea wawili watakaoongoza kwa kupata kura nyingi,” alisema Kuuli.

Rutayuga aenguliwa kwa kufoji vyeti

Mgombea Pellegrini Rutayuga ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu kutoka Mkoa wa Kagera, ameenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi kwa madai ya kukosa sifa kwa kufoji vyeti.

Mwenyekiti Kuuli amewaambia waandishi wa habari kuwa, idadi ya wapigakura sasa itakuwa ni 134 badala ya 135, huku zoezi la kuhakiki wajumbe likiwa linaendelea katika hoteli walizopangiwa wajumbe St. Gasper na Modern Hoteli.

Dodoma kimya tofauti na chaguzi nyingine

Hali ya jijini Dodoma imeonekana kuwa tulivu huku wajumbe wa mkutano mkuu wakiwa kimya na kutokuwa na hali ya kuhangaika kama ilivyokuwa katika chaguzi nyingine.

Hadi kufikia saa 12 jioni, wajumbe wengi walikuwa wamejifungia hii ni kutokana na kutotaka kuonekana wakifanya kampeni za wazi na kuogopa kushukiwa wanafanya vitendo vya rushwa, kifupi uchaguzi hauna shamrashamra kabisa.

Polisi, Wapelelezi, Takukuru wamwagwa kila kona

Kutokana na kauli ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, kusema watashirikiana vema na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), polisi, wapelelezi na maofisa wa taasisi hiyo, wamemwagwa katika viunga vya mkoa huo hasa maeneo ya hoteli wanazokaa wajumbe za St. Gaper na Modern Hoteli, yote ni kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa uhuru na haki.

Alfred Lucas afukuzwa Dodoma

 Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, jana alirudishwa Dar es Salaam na bosi wake Kaimu Katibu Mkuu, Salum Madadi, kwa madai kuwa Dodoma kuna watendaji wengi na anatakiwa akafanye kazi Dar es Salaam.

Taarifa za awali zinadai kuwa Ofisa huyo alirudishwa Dar baada ya kubainika kuwa alikuwa anamfanyia mgombea mmoja kampeni, hali ambayo haikuwa sahihi kutokana na hali ya uchaguzi huo.

“Ni kweli nimerudishwa Dar es Salaam na nimeingia leo (jana),” alithibitisha Lucas alipopigiwa simu na BINGWA.

Fedha zakauka mifukoni mwa wagombea

Hii ni hofu ya kukamatwa na Takukuru, wagombea wa uchaguzi Dodoma wametakiwa kutokuwa na fedha mfukoni  huku wanayotakiwa kuwa nayo isizidi Sh 500,000.

Wadhamini wa TFF kushuhudia uchaguzi

Kwa mara ya kwanza wadhamini wa TFF wamealikwa kuhudhuria uchaguzi leo, ambao ni Joel Bendera na Stephen Mashishanga.

Mkutano kuanza saa tatu St. Gasper

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Salum Madadi, alisema mkutano mkuu utaanza saa 3:00 asubuhi.

Madadi alisema hadi jana jioni wajumbe wa mkutano huo waliendelea kuwasili mkoani hapa na kushindwa kupata idadi kamili kwa watakaohudhuria mkutano huo.

Alisema anaamini wajumbe wote watahudhuria mkutano huo ili waweze kushiriki moja kwa moja kuchagua viongozi wao ambao watakuwa madarakani kwa kipindi kingine cha miaka minne.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi huku Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Mohamed Kiganja, akiwepo mkoani hapa kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.

Shija, Mwakalebela, Mayay, Karia wawapa kigugumizi wajumbe

Wagombea urais, Shija, Mwakalebela, Mayay na Karia, wameonekana kuwapa kigugumizi wajumbe wa mkutano mkuu huo.

Katika eneo la hoteli hiyo, wameonekana wajumbe wengi wakifika na kuondoka kimya kimya, huku wagombea wakifanya kampeni chini kwa chini na kwa umakini mkubwa.

Licha ya kampeni hizo kuendelea, lakini wajumbe wameonekana kuwa na kigugumizi juu ya nani kati ya wagombea hao wanaopewa nafasi kubwa ya kuvaa viatu vya Malinzi, aliyemaliza muda wake wa miaka minne kuliongoza shirikisho hilo, huku kukitarajiwa kuwa na mchuano mkali baina yao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU