KUELEKEA AGOSTI 23, TAWI YANGA KUZINDULIWA YOMBO

KUELEKEA AGOSTI 23, TAWI YANGA KUZINDULIWA YOMBO

384
0
KUSHIRIKI

2NA WINFRIDA MTOI

WAKATI Yanga ikitarajia kushuka dimbani Agosti 23, mwaka huu kucheza mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wao Simba, matawi ya timu hiyo hayapo nyuma katika kupanga mikakati ya kuhakikisha Mnyama anakufa siku hiyo.

Kila mahali ukipita hivi sasa mashabiki wa soka hapa nchini hasa wa timu hizi kongwe, kubwa ni mchezo huo ambao unatarajia kuvuta hisia za watu wengi kutokana na mvuto ulioanza kupatikana katika kipindi cha usajili.

Licha ya Wanayanga kutambiwa na Simba kuhusu usajili waliofanya kwa kuwachukua nyota wengi, mashabiki hao hawajali chochote kwani wanaendelea na mikakati yao.

Katika kuweka mambo sawa na kuongeza mzuka wa ushangiliaji siku hiyo, kesho tawi jipya la Yanga, Yombo Machimbo, linazinduliwa rasmi na matawi mbalimbali ya klabu hiyo yatakutana.

Mwenyekiti wa tawi hilo jipya, Ismail Mbeba, alisema wameamua kufanya uzinduzi huo haraka iwezekanavyo ili kujipanga na mechi  hiyo pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alisema kuna vitu vingi wameviandaa vya tofauti ili kuleta mvuto ikiwamo burudani na kuzindua kauli mbiu yao itakayobamba katika msimu ujao wa ligi.

Mbeba alisema wana uzoefu wa mechi zinazowakutanisha watani hivyo watakapokutana matawi mengi katika uzinduzi wao, watapata mawazo mengi lakini kubwa litakuwa ni mikakati ya kumuua Mnyama mapema.

“Sisi ujue Simba tunawapatia sehemu ndogo sana, tunawajua udhaifu wao mkubwa upo kwenye umaliziaji, ndiyo sababu hatutishiki na tambo zao za kusajili wachezaji wenye majina. Si umeona hata mechi ya Simba Day waliambulia bao moja,” alisema Mbeba.

Kumbukumbu 

za mechi ya ‘derby’

“Mimi nina umri wa zaidi ya miaka 40 na mimeshuhudia mechi nyingi ya Yanga na Simba kuanzia miaka ya 90. Kuna kipindi tuliwahenyesha Simba kwa misimu mitatu mfululizo hawajatufunga,” alisema Mbeba.

Aasema mechi ambayo ataikumbuka siku zote ni ile ya mwaka 1993, ambapo Said Mwamba ‘Kizota’ aliwafunga Simba mabao mawili peke yake, wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, (Uhuru) Dar es Salaam.

Alitamba kuwa wataendelea kujivunia kuifunga Simba mara nyingi na kutwaa makombe mengi kuliko wao ambao hadi sasa wanatambia kuwafunga mara mbili msimu uliopita katika mechi ya Kombe la Mapinduzi na mechi ya ligi.

 Majumba Sita nao kusherehekea miaka miwili

Katika hatua nyingine, Tawi la Yanga Majumba Sita linatarajia kufanya sherehe ya kuadhimisha miaka miwili tangu kuanzishwa kwake, siku hiyo hiyo ambapo msanii wa nyimbo za Singeli, Msaga Sumu atakuwa anatoa burudani.

“Tunaelekea katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, tumeona tufanye sherehe ya kuadhimisha miaka miwili ya tawi letu na itakuwa siku maalumu ya kutoa shukrani zetu kwa uongozi kufanikisha Yanga kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo,” alisema Ika Kibona, Katibu Mkuu wa tawi hilo.

Alisema wanatarajia matawi mechi ya Dar es Salaam kuhudhuria huku mgeni rasmi atakuwa Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa na watatumia nafasi hiyo kuhamasisha uongozi kuongeza nguvu ya mapambano ili kuchukua ubingwa kwa mara ya nne.

“Hakuna tatizo kwa kuwa tunakutana, tena tutakuwa matawi mengi, kuhusu mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba tutaweka mikakati hapa hapa na hatusikilizi maneno ya watu,” alisema Kibona.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU