LA LIGA 2017-18… >MADRID, BARCELONA, ATLETICO NA VITA KALI YA UBINGWA ...

LA LIGA 2017-18… >MADRID, BARCELONA, ATLETICO NA VITA KALI YA UBINGWA >MESSI KUMBURUZA TENA RONALDO TUZO YA MFUNGAJI BORA?

445
0
KUSHIRIKI

images (1)MADRID, Hispania

KWA misimu 15 iliyopita, taji la La Liga limekuwa likibebwa na klabu mbili tu Hispania; Real Madrid na Barcelona. Baada ya Barca kutesa kwa misimu miwili mfululizo, msimu uliopita ilikuwa ni zamu ya mahasimu wao, Madrid.

Msimu ujao wa Ligi Kuu hiyo ya Hispania unatarajiwa kuanza Agosti 18, na tayari ratiba imeshatoka, ambapo Madrid wataanza safari yao ya kuutetea ubingwa kwa kuvaana na Deportivo La Coruna, huku  Barca wakiwakaribisha Real Betis.

Hata hivyo, Girona, Levante na Leaganes zinatajwa kuwa huenda zikajikuta zikishindwa kukabiliana na mikikimikiki ya La Liga na hatimaye kushuka daraja.

Utamu mwingine wa msimu ujao utakuwa kwenye mbio za kukiwania kiatu cha mfungaji bora, ambapo msimu uliopita Lionel Messi alimfunika mpinzani wake, Cristiano Ronaldo.

Messi, mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or, aliibuka mbabe mbele ya Mreno huyo baada ya kupachika mabao 37.

Ronaldo alijikuta katika nafasi ya tatu kwa mabao yake 25, kwani ya pili ilikwenda kwa Luis Suarez, aliyewatungua walinda mlango mara 29.

Je, Messi ataendeleza ubabe wake kwa Ronaldo kwa misimu miwili mfululizo?

Kwa upande mwingine, uhondo mwingine utakuwa kwenye vita ya ubingwa na kinyang’anyiro cha kuingia ‘top three’, ambapo ni Madrid, Barca, Atletico Madrid na Sevilla ndizo zinazopewa nafasi kubwa.

Real Madrid

Madrid wamelichukua taji hilo la La Liga mara 33, huku wapinzani wao, Barca wakifanya hivyo mara 24 na Atletico Madrid wakiwa wameshinda mara 10.

Madrid wanaingia msimu ujao wakiwa na nguvu ya rekodi yao nzuri ya msimu uliopita, ambapo waliweza kulibeba mara mbili mfululizo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikiwa ndiyo klabu pekee kufanya hivyo katika historia ya michuano hiyo.

Katika soko la usajili, Madrid wamekiongezea nguvu kikosi chao kwa kuwasajili Theo Hernandez kutoka Atletico na Dani Ceballos aliyekuwa na Real Bets msimu uliopita. James Rodriguez, Fabio Coentrao wameondoka kwa mkopo na Pepe amejiunga na Besiktas.

Barcelona

Katika misimu tisa iliyopita, Barca imechukua ubingwa wa La Liga mara sita. Msimu ujao kikosi hicho kitakuwa chini ya kocha Ernesto Valverde, aliyechukua mikoba ya Luis Enrique.

Msimu ujao, Barca watakuwa na presha ya kuchukua La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya, hasa baada ya kutofanya vizuri msimu uliopita, ambapo walichukua taji la Copa del Rey pekee.

Barca si wabovu sana kwa kuzitazama mechi zao za michuano ya ‘pre-season’ ya ICC, ambapo waliweza kuzichapa Juventus na Manchester United.

Licha ya kuondokewa na Neymar aliyekwenda PSG, tumaini la kocha Valverde msimu ujao litakuwa kwa mastaa wake wapya,  Nelson Semedo, Gerard Deulofeu na Marlon, waliotua Catalunya kwa jumla ya Euro milioni 47.5.

Pia, bado wameendelea kuzisumbua Liverpool na Juve juu ya mastaa wao, Philippe Coutinho na Paulo Dybala.

Atletico Madrid

Bado Atletico ina nafasi kubwa ya kushika nafasi ya tatu msimu ujao, ingawa inaweza kuwa ngumu kidogo kutokana na adhabu yao ya kutosajili.

Mabingwa hao wa La Liga kwa msimu wa 2013-14 hawajasajili sana katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi na imewauza makinda Oliver Torres na Theo Hernandez waliokwenda Porto na Madrid.

Wamemchukua Vitolo kutoka Sevilla, ambaye hata hivyo hatacheza hadi Januari, na wamekuwa wakimtamani mchezaji wao wa zamani anayeichezea Chelsea,  Diego Costa, lakini wana Pauni milioni 26 pekee.

Sevilla

Msimu uliopita walikuwa changamoto kubwa kwa vigogo Barca, Madrid na Atletico, kwenye safari ya ubingwa. Walimaliza ligi wakiwa nafasi ya nne, baada ya kujikusanyia pointi 72 katika mechi zao 38. Waliachwa pointi sita pekee na Atletico, walioshika nafasi ya tatu nyuma ya Madrid na Barca.

Huenda wakamaliza ligi wakiwa ‘top three’ msimu ujao, hasa baada ya usajili walioufanya kwa kumsajili mpachikaji mabao hatari wa Sampdoria, Luis Muriel, kwa ada ya euro milioni 20.

Ingawa wamewapoteza Vitolo aliyekwenda Atletico, Vicente Iborra, Yevhen Konoplyanka, Adil Rami na Mariano, watakuwa na mastaa Ever Banega aliyetokea Inter Milan, Nolito aliyekuwa Man City, Guido Pizarro na Sebastien Corchia wa Lille.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU