Nani Rais mpya TFF?

Nani Rais mpya TFF?

305
0
KUSHIRIKI

download (1)NA TIMA SIKILO

BAADA ya mvutano mkubwa katika usaili na kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), leo ndio kile kivumbi chenyewe ambapo wadau wa soka watamjua rais mpya na wajumbe watakaoendesha shirikisho hilo baada ya uchaguzi huo kufanyika mjini Dodoma.

Jumla ya wagombea 64 wamefuzu kuwania nafasi mbalimbali kwenye shirikisho hilo, baada ya mchakato huo wa uchaguzi kukumbwa na matukio mbalimbali ya utata, ikiwamo kile kilichoitwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Revocatus Kuuli, kuwa ni kwenda kinyume cha taratibu za uchaguzi, baada ya baadhi ya wajumbe kutaka kuwapitisha wagombea kinyemela.

Hivyo kamati hiyo ya uchaguzi ilivunjwa na Kamati ya Utendaji ya TFF na wajumbe wote wanne na kubakizwa mwenyekiti pekee na kuwekwa wajumbe wapya ambao walikaa na kufanya upya mchakato huo wa uchaguzi.

Kamati hiyo iliwapitisha wagombea sita kwa nafasi ya urais, ambao leo wataonyeshana kazi kwenye kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi baada ya kila mmoja kunadi sera zake tangu Agosti 7, mwaka huu na hadi jana jioni zilipofungwa.

Wagombea watakaominyana kwenye nafasi ya urais ni Imani Madega, Walace Karia, Fredrick Mwakalebela, Ally Mayay Tembele, Shija Richard na Emmanuel Kimbe.

Wagombea watatu waliokatwa na kukosa nafasi ya kuwania nafasi hiyo leo ni aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi, ambaye hakupitishwa kutokana na kushindwa kuhudhuria kwenye usaili, kitu ambacho ni kinyume cha kanuni ya 11 (7) ya uchaguzi wa TFF toleo la 2013.

Wengine waliokatwa ni Fredrick Masolwa na John Kijumbe, ambao wote hawakuwa na uzoefu angalau miaka mitano kwenye masuala ya soka, kitu ambacho ni kinyume cha kanuni ya 9 (3) ya uchaguzi wa TFF toleo la 2013, huku Athuman Nyamlani akijitoa mwenyewe kwenye kinyang’anyiro hicho.

Kufuatia kukatwa kwa Malinzi ambaye amekaa kwenye nafasi hiyo ya urais kwa muda wa miaka minne tangu 2013, hivyo uchaguzi huo utafanyika leo bila kuwa na mtu wa kutetea kiti chake.

Malinzi hakupata nafasi ya kufanya usaili baada ya kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, siku chache kabla ya mchakato huo kufanyika na baadaye alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kufunguliwa mashtaka 28 pamoja na wenzake wawili, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Msigwa na Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, ambapo moja ya mashtaka hayo ni kuhusishwa na utakatishaji fedha ambalo limemfanya akose dhamana na kushindwa kuhudhuria usaili uliofanyika kwa siku tatu.

Je, ni nani ataibuka rais mpya wa shirikisho hilo baada ya kiti hicho kukosa mgombea wa kukitetea kwa mara ya kwanza tangu Chama cha Soka Tanzania (FAT) na kuwa Shirikisho la Soka (TFF) kwenye uchaguzi huo wa leo.

Pamoja na wagombea hao wa urais, upande mwingine nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF, kamati hiyo ya uchaguzi imepitisha wagombea watano, wakati mmoja aliamua kujitoa mwenyewe.

Wagombea wanaowania nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF ambao wamepitishwa na kamati hiyo ya uchaguzi na leo wataonyeshana kazi ni Michael Wambura, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela, Stephen Mwakibolwa na Mulamu Nghambi, huku Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ akiamua kujitoa baada na yeye kufikishwa mahakamani na moja ya mashtaka aliyofunguliwa likiwa ni kutakatisha fedha.

Kwa upande wa wagombea wa Kamati ya Utendaji watakaotoana jasho leo wapo wajumbe 53, kutoka katika kanda zote 13. Kanda ya Kwanza ambayo ina mikoa ya Kagera na Geita, ilikuwa na wagombea wanne lakini wamepitishwa watatu na mmoja alikatwa. Kanda ya pili ambayo ni Mara na Mwanza, itakuwa na wagombea wanne wakati kanda ya tatu ambayo ni Shinyanga na Simiyu, ina wagombea watatu.

Kanda ya nne ni Arusha na Manyara, ambayo ina wagombea watatu na kanda ya tano ambayo ni Kigoma na Tabora wakichuana wagombea wanne.

kanda ya sita ni Katavi na Rukwa, kuna wagombea wawili na kanda ya saba ambayo inajumuisha Mbeya na Iringa, wagombea wanne wataumana, kanda ya nane yenye mikoa miwili wa Njombe na Ruvuma, wagombea wanne na wataminyana. Kanda ya Tisa yenye mikoa ya Lindi na Mtwara wagombea wawili watamalizana wenyewe kwa wenyewe. Kanda ya 10 yenye mikoa ya Dodoma na Singida kutakuwa kivumbi cha wagombea watano, huku Kanda ya 11 ambayo ni Pwani na Morogoro ilikuwa na wagombea watatu watapambana na Kanda ya 12 yenye mikoa ya Kilimanjaro na Tanga iliyokuwa na wagombea watatu wamepita wawili na kanda ya 13 ambayo ni Dar es Salaam peke yake ilikuwa na wagombea 15 na wakapita 12.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU