TABIA ZINAZOCHOCHEA UPENDO

TABIA ZINAZOCHOCHEA UPENDO

606
0
KUSHIRIKI

unnamedUPENDO ni hisia za dhati juu ya mtu au kitu fulani. Ni hisia zinazokuja zenyewe bila shuruti au ombi fulani. Ukiwa na hisia hizi mhusika utamchukulia kipekee na kumjali kwa kiwango stahili.

Hata siku moja huwezi kumwacha akiumia au akidhurika mbele yako. Katika kila hali utajitahidi awe katika mazingira salama na ya amani. Ndani ya hisia hizi huwezi kutaka kukaa mbali na mhusika wala kuona akiwa na mtu mwingine anayekupa wasiwasi na mashaka.

Ukiwa mwanamke, hutopenda mwenzako akae sana na wanawake labda wale wenye nasaba na wewe au unaowaamini sana. Halikadhalika ukiwa mwanamume hutopenda akae na wanaume wengine wasio na nasaba na wewe na wenye kukupa wasiwasi. Hapa nazungumzia hisia za upendo ndani ya mapenzi.

Hisia hizi huwa tofauti sana na zile hisia za upendo wa kawaida. Upendo wa kaka na dada, shangazi na mjomba. Hisia za namna hii hazilingani na zina sifa tofauti kabisa.

Ila japo ukweli ni kwamba hisia za upendo huja ‘automatically’ ila pia wakati mwingine hupotea kwa namna hiyo pia.

Kuna vitu vinaweza kusababisha mhusika akazidi kukupenda na kuna vitu ukifanya mhusika hatoweza kukupenda zaidi.

ahati mbaya sana kuna mengi yanafanyika katika majumba bila kujua kama yana athari kubwa ya kudidimiza upendo wa wahusika kwao.

Una hakika mpenzi wako anakupenda? Ni kwa namna gani unafanya aendelee kukupenda na kukujali siku zote?

Hata kama unapanda mbegu katika ardhi ya rutuba ila bila huduma nzuri mbegu husika huenda isikue wala kufika lengo unalotaka. Mapenzi ni kama mbegu. Anayekupenda ni kama ardhi ya rutuba unapoenda kupanda mbegu yako ya upendo.

Japo ukweli ni kwamba ardhi hiyo inaweza kustawisha mbegu yako ila bila kuimwangilia vizuri pamoja na kuihudumia kwa namna inayofaa katu haiwezi kukua. Nipo hapa kukuelekeza namna bora ya kumwagilia upendo wako katika ardhi yenye rutuba katika moyo wa mpenzi wako.

Vitu viko vingi vya kufanya ili mwenzako azidi kukupenda na kukujali ila nitakuletea vichache ila vyenye maana kubwa. Ni bora kujua vichache vya maana kubwa kuliko kujua vingi vyenye maana ndogo. Karibu katika ukurasa huu wa maarifa ya ndoa na maisha yako ya mapenzi.

(i)                 HESHIMA, shuleni wanafunzi wanafundishwa heshima, nyumbani wazazi wanafundisha heshima, kazini wakubwa wetu wa kazi  wanatusisitizia tuheshimiane. Hata hapa katika suala la mapenzi tunaizungumzia heshima. Nini heshima?

    Heshima haishii katika salamu au mavazi. Ni mjumuisho wa matendo yako karibu yote kwa wahusika au mhusika.

Katika mapenzi unatakiwa kuwa na heshima stahiki kwa mpenzi wako. Heshima haimaanishi u muoga au mjinga sana, hapana. Heshima huku inamaanisha katika jumla ya vitu na mambo yako kwake.

Unamtazama vipi? Mnaongea nini na unafanya nini? Kila mmoja anapenda kuheshimiwa. Hakuna mtu anayetaka kuonekana wa hivi hivi kwa mwenzake.

Unapotoa heshima kwa mwenzako maana yake unamfanya ajihisi wa thamani na maana sana kwako.

Unapotoa ahadi unatimiza? Anapokukataza kufanya jambo fulani huwa inakuaje? Unakubali kwa mdomo kisha unakana kwa vitendo? Kwa namna hiyo unamfanya mwenzako ajihisi unyonge na asiye na thamani katika maisha yako. Kwa namna hiyo hata namna anavyokutazama na kukutafsiri huwa tofauti sana.

Ndiyo, anakupenda sana ila ni kwa namna gani upendo utastawi sehemu isiyomfanya ajihisi wa thamani? Kwa aina yoyote hapa kuna jambo usilotarajia litatokea.

Kuwa mnyonge chumbani hiyo si heshima, kuogopa kumchangamkia mwenzako ndani pia hiyo si heshima. Naomba nieleweke.

Heshima maana yake si kuwa mnyonge wala kushindwa kusema unachojihisi. Heshima si kutendewa mabaya na kunyamaza, hapana.

Heshima ni kujali na kuthamini matendo na maneno ya mwenzako. Ni kumsikiliza na kujali nini mwenzako anataka kutoka kwako. Ila isiwe kila kitu, kuna baadhi wanaweza kutaka yasiyohitajika usimtimizie kwa namna ya kusema nina heshima kwa mwenzangu.

Kuwa makini heshima ndani ya nyumba ni uti wa mgongo wa amani na furaha.

(ii)KUMSIKILIZA, hakuna mtu anayependa kuona wakati anaongea akidharaulika. Kila mmoja anapenda na kutamani kipindi cha mazungumzo yake pawe kimya kwa maana ya kusikilizwa. Vipi wewe kwa mwenzako?

    Unapaswa kuwa na tabia ya kumsikiliza mwenzako. Usikivu wako unamfanya aone ni kwa namna gani unavyomthamini na kumjali. Hata kama anaongea maneno unayoyaona hayana pointi suala si kumpuuza au kumdharau, hapana.

Ni kumsikiliza hadi mwisho halafu kumpa usahihi wa kitu chenyewe. Kila mmoja hupenda kuwa mtu maalumu na wa thamani kwa mwenzake na huwa huo umaalumu na uthamani unapimwa kwa namna anavyosikilizwa.

Akiongea anataka kuona kweli anaongea bila kujali nini anaongea. Kwake hii huwa ina maana kuwa alipo ni mahala salama penye umuhimu na thamani ya maisha yake.

(iii)Kujishusha, wakati mwingine inabidi iwe hivi. Ndiyo, mapenzi si jela wala utumwa. Ila pia katika namna ya kutafuta suluhu na amani katika nyumba inabidi ujifunze kuwa katika hali hii. Ni hali bora yenye kuchochea amani na upendo zaidi baina yenu. Hali ya kujishusha!

Japo kukosea unaweza kuwa umekosewa wewe ila wakati mwingine kuwa mpole na muungwana zaidi. acha kufikiria kuonesha umwamba! Wengi huenda watasema huu si utumwa sasa. Hapana, huu si utumwa bali ni busara na uwerevu ambao wengi hawana.

Unapojishusha kuna hali fulani unaitengeneza kwa mwenzako. Kuna umaalumu na upekee fulani ambao wengi hawana unakuwa unampa mwenzako.

Migogoro na ugomvi mwingi katika uhusiano huwa kwa kuwa hakuna hata mmoja baina yao anayetaka kujishusha. Kama ukijishusha mbali na kumaliza migogoro kadhaa katika nyumba yako pia unafanya mwenzako akufikirie katika namna bora na ya kipekee zaidi.

Hakuna asiyetaka kuwa na mtu wa aina hii. Kama mwenzako anakupenda hapa atakupenda zaidi kwa maana utakuwa umemfanya ajione maalumu sana. Jishushe pindi inapotokea mitafuruku yenu!

(iv) Kuomba msamaha, hata Mwenyezi Mungu kaweka msamaha, ina maana kukosea huwa kupo tu.

 

  Ndiyo, hatukiwi kukosea kwa makusudi kwa kigezo cha uwapo wa msamaha ila kibinaadamu huwa tunakosea.

Umemkosea  na bila shaka mwenzako hana amani kwa sababu hiyo! Kaa naye kisha omba msamaha. Muombe kidhati huku ukimuahidi hutorudia pamoja na kuonesha kujutia kwa yote uliyoyafanya.

Msamaha humaanisha wewe ni muungwana wala hukufanya jambo husika kwa makusudi. Wakati mwingine unaweza kuwa hujafanya kosa ila mwenzako akahisi umefanya kosa. Jambo linaweza kuwa dogo au la kawaida ila mwenzako akatafsiri kama kosa.

Kwa kuwa anaona ni kosa epuka kuchochea ugomvi zaidi, kaa naye kisha muombe msamaha. Tena kama unajua kuna kitu Fulani kizuri huwa anapenda baada ya kuomba msamha mfanyie ili siku iwe nzuri zaidi.

Hakuna mtu anayeishi bila kufanya makosa. Ila baadhi huwa tunawahukumu zaidi kwa maana mbali na kutenda makosa huwa wanajifanya wajuaji na kutotaka kuomba radhi. Tabia hii katika uhusiano wako ni sumu. Inamfanya mwenzako kukuona jeuri na mfanya makosa kwa makusudi. Omba msamaha kwa dhati.

Muoneshe kuwa thamani yake katika maisha yako ni kubwa hivyo kama kosa basi ulilifanya bila kujua athari zake katika furaha yake.

(v)Kumsaidia, unadhani ni katika suala la pesa pekee? Hapana. Unaweza kumsaidia katika kila namna, iwe ushauri ama hata kuelekeza mahala panapopatikana kitu hitajiwa.

  Kila mmoja katika maisha huwa kuna kipindi anakwama katika jambo fulani. Mtu akiwa katika hali hiyo wakati mwingine hupelekea kuona kama kila kitu kinaenda mrama upande wake. hujiona mnyonge na kwa wengine hukumbwa na hali fulani ya kukata tamaa. Onesha umuhimu wake kwako.

Mpe msaada hitajiwa. Hata kama huna msaada wa moja kwa moja, jaribu kumpa faraja na amani katika moyo wake. mfanye ajihisi kuwa kitu alichokosa si kikubwa kama kukukosa wewe.

Katika faraja na matumaini kila kitu atakiona chepesi kwake. Mshauri kwa utulivu huku ukimpa nguvu ya matumaini kupitia maneno yako. Katika kipindi chote cha shida yake kuwa mpole sana kwake na zidisha hali ya upendo na kumjali. Hii itamfanya apate amani na raha na matokeo yake kitu alichokosa au jambo linalomtatiza haliwezi kuwa na madhara sana katika akili yake.

Usikariri na kuamini msaada pekee wa kumpa mwenzako ni pesa, hata kama huna una nafasi ya kumpa msaada wa mawazo na furaha ikarudi tena katika maisha yake.

Msaidie mwenzako anapokwama. Msaidie kutafuta afueni ya tatizo lake katika kipindi kigumu. Unapofanya hivi unadhani ni kwa namna gani asiweze kukuona una thamani na maana kubwa katika maisha yake?

Atakujali na kukupenda. Atakuwaza na kutaka kila siku uwe na amani kwa sababu unaonesha thamani na umuhimu wake katika maisha  yake.

i) Msifie, nani hapendi kusifiwa akifanya vizuri? Hakuna! Mpe sifa inayostahili mwenzako. Akikupa au akikufanyia jambo unaloamini ni bora na linalohitaji kumsifia usisite kufanya hivyo.

 Kama akiacha kusifiwa na wewe unadhani akasifiwe na nani? Unapomsifia anaona ni kwa vipi kitu au kitendo chake kinavyothaminiwa.

Na siri nyingine watu wasioijua ni kuwa unapomsifia mtu kwa jambo zuri alilokufanyia unampa kasi au shauku ya kukufanyia tena na zaidi pengine.

Kama jana kakupa unachostahili katika namna bora, mpe sifa yake. Hii itamfanya kujua kuwa jana ulifurahi na itamfanya na leo au kesho atake kukufurahisha tena. Unaposhindwa kutoa sifa kwa mwenzako unamfanya asione tofauti ya kukufanyia kitu kizuri na kibaya.

Jana kakukera umesema wee mpaka kero ila leo kakufanyia jambo jema umenyamaza kana kwamba hajafanya kitu. Ajue vipi kama jambo husika limekupa furaha na amani? Tuseme kwako baya ndiyo baya ila zuri halina maana? Kama unavyomfanya ajue kwa baya analokufanyia pia mfanye ajue kwa zuri analokufanyia.

Kila binaadamu hupenda kuwa mzuri kimatendo. Mpenzi wako pia huhitaji aonwe bora na wa thamani sana kwako. Msifie kwa zuri lake ili ajue ni kwa namna gani unathamini matendo yake. Ila mbali na kumfanya akuone una shukurani pia utamfanya azidi kukufanyia matendo bora.

(vii) Kuwa muwazi, kuna wengi wanaharibu amani na furaha ya wenzao kwa usiri usio na maana. Kitu kidogo unataka mwenzako asijue, unadhani atakufikiria vipi?

 Mapenzi yanajengwa na wivu na asili ya wivu huja katika makisio. We fanya siri kwa jambo lisilohitaji usiri ila jua mwenzako atakutafakari vingine.

Wewe ndiye yeye kwa maana Mu mwili mmoja, sasa siri siri za kazi gani? Ukiongea na simu unaonekana kuna kitu unahofia, sms zako hutaki azione.

Unawasiliana na kina nani hao? Kwanini hutaki asione? Hapa utamfanya mwenzako awe na mashaka zaidi na wewe na mashaka haya yakizidi ndiyo huwa yanapunguza ile ladha na amani ya wapendanao.

Kuwa huru kwake, mfanye ajue mengi yanayokuhusu. Uhuru na uwazi unaompa unamfanya akuone kila kitu kwake. Hatokuwa na hofu wala mashaka na matendo yako.

Kila jambo unalofanya atakuwa na amani nalo kwa maana hakuna kitu kinachomtia wasiwasi katika matendo yako. Hawezi kukuwazia mabaya, hawezi kukuona unatabia mbaya. Hapa unadhani kiwango chake cha upendo juu yako kitakuwa vipi?

Atakupenda sana kwa maana anajua wewe ni mtu unayehifadhi amani na furaha yake. Hakuna unachomtia mashaka au maswali yasiyo na majibu.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU