WAJUMBE TFF MSIFANYE MAKOSA

WAJUMBE TFF MSIFANYE MAKOSA

215
0
KUSHIRIKI

download (1)NA CLARA ALPHONCE

LEO Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatarajia kupata viongozi wapya ambao wataiongoza taasisi hiyo kwa miaka minne ijayo, baada ya uongozi uliopo madarakani chini ya Rais Jamal Malinzi, kumaliza muda wake.

Uchaguzi huo utafanyika makao makuu ya nchi, mjini Dodoma, ambapo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF,  watawapigia kura wagombea 29 wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika shirikisho hilo.

Wajumbe watakaopiga kura ni Mwenyekiti wa Mkoa, Katibu wake na mjumbe mmoja wa mkutano mkuu, pamoja na wenyeviti wa vyama na wanachama wa shirikisho hilo.

Bila shaka wapiga kura wamepata nafasi ya kuzisikia vizuri sera za wagombea hao wakati wa kampeni zao. Hivyo, leo ni wakati wa kufanya uamuzi sahihi kwa kumchagua mgombea mwenye njaa ya mafanikio ya soka la Tanzania.

Wapo viongozi waliofanya vizuri na kulifikisha soka hapa lilipo, lakini bado tuna safari ndefu ya kufika pale tunapohitaji kufika.

Huu ni wakati wa kufika pale tulipohitaji kwa miaka mingi na ili tuweze kufanya hivyo, lazima tuwe na viongozi wazuri na wenye uwezo wa kutufikisha mbele na kuachana na viongozi wenye maneno mengi.

Kwa kuwa wao ndio watakaokuwa na fursa ya kupiga kura leo, wajumbe wa mkutano mkuu pale wanapaswa kutenda haki kwa kumchagua kiongozi na si kusubiri kutupa lawama kwa uongozi utakaoingia madarakani.

Ukweli ni kwamba, wapiga kura ambao ni wajumbe wa TFF, wana rungu la kukuza au kudidimiza soka la Tanzania kwa kutumia karatasi nyeupe za kupigia kura.

Ni wazi kuwa soka la Tanzania lina madudu mengi na kila anayeingia madarakani amekuwa na maneno matamu ya kuwalainisha wapiga kura, lakini mwisho wa siku hakuna jipya linalofanyika zaidi ya kurudi nyuma.

Kutokana na majanga ambayo yamelikuta soka la Tanzania, wakati tulionao si wa kujiandaa bali ni wa kusema sasa tunashiriki michuano mikubwa Afrika na duniani na kufanya vizuri au kuonyesha na sisi ni wapinzani na si washiriki kama ilivyo kwa kila mwaka.

Hilo litawezekana ikiwa kila mpiga kura atatumia kalamu na karatasi yake vizuri kwa kuchagua kiongozi mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya ndani ya soka.

Kwa miaka mingi TFF wameshindwa kuondoa mahaba yao kwa klabu kongwe za Simba na Yanga katika utendaji wa kazi wake na kulifanya soka la Tanzania kupoteza thamani yake katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Ushabiki huo umewafanya viongozi kushindwa kufuata kanuni na kufanya maamuzi kwa matakwa yao, kitu ambacho kimekuwa kikilitafuna soka la Tanzania kwa miaka mingi.

Viongozi wanaotakiwa kwa sasa ni wale wenye misimamo na kusimamia kanuni, kutetea haki ya wanyonge wasio na sauti.

Kuondoa migogoro, kuhakikisha ligi inachezwa kwa misingi ya haki na kuacha upendeleo wa baadhi ya timu, hasa zile ambazo viongozi wake wana sauti na ushawishi mkubwa katika mchezo wa soka.

TFF ni taasisi kubwa hapa nchini, hivyo haitakiwi kuwa na viongozi wanaojifunza kuongoza, au wanaoenda kutafuta kujitajirisha.

Soka ni mchezo unaopendwa zaidi duniani, kwa maana kwamba una fursa ya kuingiza fedha nyingi kama kutakuwa na umakini katika uwekezaji na utekelezaji.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU