DUNIA YA MKE WANGU

DUNIA YA MKE WANGU

418
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia

 “Najua nitakufa siku si nyingi ila naomba ujitahidi kunipa dawa ili nifanikiwe kujifungua kabla sijaondoka duniani,” aliongea Julia kauli iliyoushtua moyo wa Kai.

SASA ENDELEA

“JULIA mke wangu wewe bado una nguvu ya kuishi kwanini unakata tamaa,” aliuliza Kai kwa huzuni.

“Hali yangu mbaya Kai, ujauzito nilionao unaweza ukachangia niishi maisha mafupi. Maana nakaribia hatua ya tatu ya kuugua. Dawa za Vilter primase naona hazina nguvu kutokana na hii mimba.”

“Usiogope mke wangu,” aliongea Kai akilengwa na machozi.

“Siogopi kufa ila naogopa kukuacha peke yako. Pia sipendi kuona najifungua watoto wangu wakiwa na Ebola.”

Wakati wanaongea hayo, walikuwa wakipanda ngazi kuelekea vyumba vya juu, Kai akiwa amemshika Julia. Ilikuwa ni huzuni kubwa kwa Julia kutokana na kujua kuwa maisha yake hayakuwa na muda mwingi hapa duniani.

Kai alimpeleka Julia hadi chumbani. Julia alikaa kwenye kitanda na kukigusa gusa akikumbuka tukio la mara ya mwisho kabla hajaondoka kwenda Ethiopia.

Baadaye kidogo Kai alimpikia mkewe chakula kizuri. Ingawa Julia alikuwa na nguvu kidogo za kufanya kazi, lakini Kai hakutaka mkewe afanye lolote kwa wakati huo kwa sababu alijua mwili wake unatumia nguvu nyingi kupigana na usumbufu wa mimba pamoja na virusi vya Ebola, ambavyo hufanya kazi kwa bidii na kwa kasi ndani ya mwili wa binadamu.

Baada ya chakula, Kai alimpeleka Julia bafuni kuoga. Aliingia pamoja naye kwenye sinki. Waliendelea kuongea mengi wakiwa ndani ya maji, huku wakipata kinywaji.

“Mume wangu naogopa sana kuonana na wazazi wetu hasa mama yangu,” aliongea Julia.

“Hupaswi kuogopa mke wangu kwani tayari ukweli wote wanaujua.”

“Nimefanya kosa kubwa sana kiasi cha kutamani niihame nchi, nijifiche mama asinione. Huwa najiuliza ni upendo gani niliokuwa nao wa kuwafikiria wale wananchi wa Keneza huku nisifikirie kuwa mimi ni mjamzito? Najiona wa ajabu sana.”

“Lakini wakati unaamua kwenda Ethiopia si ulijua kuwa utarudi baada ya siku tatu?”

“Pamoja na hayo mpenzi. Ilitakiwa nifikirie maisha yangu mimi na watoto wangu. Saa nyingine huwa nawaza kuwa huenda ibilisi aliniingia. Akanishawishi kwenda Ethiopia.”

“Hapana usikufuru. Pia naomba uache kujilaumu, ukifanya hivyo, unaniumiza na mimi pia.”

Kai alimsogelea Julia hadi karibu na uso wake. Taratibu alianza kuupeleka mdomo wake ili ambusu Julia. Julia alimzuia kwa mikono yake akimtaka asifanye hivyo.

“Kumbuka mimi ni mwathirika,” aliongea Julia.

“Nilishakueleza kuwa sijali hilo. Unadhani wakati nachukua uamuzi wa kuja Ethiopia sikujua kuwa na mimi ninaweza kupata maambukizi? Nilijua ila kwa kuwa niliamua kufa kwa ajili yako sikuona shida yoyote. Sikuogopa kabisa kwa kuwa sura yako inaishi kwenye moyo wangu,” aliongea Kai maneno yaliyokuwa bustani ya maua kwenye nfasi ya Julia.

“Sawa hata nikikukataza wewe pia ni mwathirika,” aliongea Julia.

“Kwanini unasema hivyo,” Kai aliuliza.

“Sidhani kama hukupata maambukizi kwa safari ya kwenda Amhara na kurudi, wewe pia utakuwa na Ebola. Kwa sababu virusi vilikuwa vikisambaa kwa njia ya hewa, kutokana na idadi nyingi ya maiti. Hivyo ni vigumu na wewe mume wangu kuwa mzima.”

“Mimi ni mzima mke wangu nadhani hii ni habari ya kushangaza kwako.”

“Inawezekana vipi?”

“Mungu ni mkuu kwangu, aliniwezesha kugundua kinga ya Ebola. Ila niliithibitisha kuwa inafanya kazi, baada ya kuja Amhara.”

“Mmmh mume wangu umeanza utani wako?”

“Sikutanii mke wangu nimefanikiwa.”

“Mungu ni wema, umewezaje mpenzi?”  aliuliza Julia akistaajabu sana.

“Nitakuhadithia,” alijibu Kai huku akitabasamu.

“Dunia ya wanasayansi inajua kama umefanikiwa?” aliuliza Julia.

“Bado sijamjulisha yeyote yule. Nitafanya hivyo hivi karibuni.”

Julia alimkumbatia Kai, alifurahi kuona mume wake amefanikiwa kugundua kinga ya virusi vya Ebola.

“Hongera sana mume wangu, najivunia kuwa mkeo. Nakuomba siku ufanikiwe kugundua dawa ya Ebola. Hata nikiwa kaburini roho yangu itakupa nguvu ya kugundua tiba hiyo,” aliongea Julia kwa machozi.

Kai alimtazama mke wake kwa muda kidogo kisha akamwambia.

“Nitahakikisha kabla ya siku tatu kupita, nitakuwa na dawa ya kutibu Ebola. Mtu wa kwanza kumpa dawa hiyo atakuwa ni mke wangu,” aliongea Kai kwa kujiamini.

Julia alimtazama mume wake asiyaamini maneno yake.

Nini kitaendelea? Usikose kesho

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU