SIMBU AWE CHACHU KUIBUA VIPAJI ZAIDI VYA RIADHA

SIMBU AWE CHACHU KUIBUA VIPAJI ZAIDI VYA RIADHA

326
0
KUSHIRIKI

MWANARIADHA wa Tanzania aliyetwaa medali ya shaba katika Mbio za Dunia zilizofanyika jijini London, Uingereza, Alphonce Simbu, aliwasili jijini Dar es Salaam juzi na kulakiwa na wadau mbalimbali wa mchezo huo, viongozi wa Serikali na ndugu zake.

Simbu alifanikiwa kutwaa medali hiyo na kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika mbio hizo huku wenzake saba wakitoka kapa.

Kitendo cha Simbu kutwaa medali ya shaba katika mbio hizo za dunia, kimepokewa kwa furaha kubwa na wadau wa mchezo huo hapa nchini kutokana na ukweli kwamba, kwa miaka mingi Tanzania imekuwa msindikizaji kwenye mashindano hayo.

Mbali ya hilo, pia Simbu amefanya kweli katika mashindano hayo katika kipindi hiki ambacho Tanzania imekuwa ikishindwa kufanya vema katika michuano mbalimbali ya kimataifa na kubakia kuwa wasindikizaji kila inaposhiriki.

Si katika riadha pekee, hata michezo mingine ukiwamo ule unaopendwa zaidi duniani wa soka, Tanzania imekuwa haifanyiki vizuri pamoja na kuwekeza nguvu nyingi katika maandalizi pamoja na sapoti kutoka kwa wadau mbalimbali.

BINGWA kama ilivyo kwa wadau wengineo wa michezo nchini, tumefurahishwa mno na mafanikio ya Simbu kule London, tukiamini amefungua mlango kwa wanariadha wengine nchini kufuata nyayo zake.

Lakini pia, mafanikio ya Simbu katika mbio hizo za dunia ni kama salamu kwa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kuona ni vipi wanaweka mikakati ya nguvu kuibua vipaji zaidi katika mchezo huo, ili mwisho wa siku viweze kufuata nyayo za Simbu.

Kwa upande wetu, tunaamini iwapo RT watajipanga vilivyo, wanaweza kuzalisha akina Simbu lukuki tayari kuzidi kuuwasha moto kwenye michuano ya kimataifa, kuanzia mbio za Dunia, Olimpiki, Michezo ya Afrika (Africa Games), Jumuiya ya Madola na mingineyo.

Kwa bahati nzuri, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaaliwa kuwa na vipaji vya riadha ambavyo iwapo vitavumbuliwa na kuendelezwa ipasavyo, nchi yetu inaweza kuwa tishio katika mashindano mbalimbali kama ilivyo Kenya ambayo imekuwa ikitesa mno na kuzitambia nchi kubwa kama Marekani, China, Uingereza na nyinginezo.

Tumalizie kwa kumpongeza Simbu kwa mafanikio yake hayo, lakini pia tukiitaka RT ‘kukaza msuli’ kuhakikisha inaibua vipaji zaidi vya riadha na kuviendeleza ili Tanzania iweze kuendelea kung’ara kwenye michuano mbalimbali ya anga ya kimataifa.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU