DUNIA YA MKE WANGU

DUNIA YA MKE WANGU

442
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia

“Dunia ya wanasayansi inajua kama umefanikiwa?” aliuliza Julia.

 “Bado sijamjulisha yeyote yule. Nitafanya hivyo hivi karibuni.”

Julia alimkumbatia Kai, alifurahi kuona mume wake amefanikiwa kugundua kinga ya virusi vya Ebola.

 “Hongera sana mume wangu, najivunia kuwa mkeo. Nakuomba siku ufanikiwe kugundua dawa ya Ebola. Hata nikiwa kaburini roho yangu itakupa nguvu ya kugundua tiba hiyo,” aliongea Julia kwa machozi.

Kai alimtazama mke wake kwa muda kidogo kisha akamwambia.

 “Nitahakikisha kabla ya siku tatu kupita, nitakuwa na dawa ya kutibu Ebola. Mtu wa kwanza kumpa dawa hiyo atakuwa ni mke wangu,” aliongea Kai kwa kujiamini.

Julia alimtazama mume wake asiyaamini maneno yake.

SASA ENDELEA

“MACHO yako hayaamini niyasemayo lakini moyo wangu unaokupenda umenipa nguvu. Nahitaji nguvu yako pia kwani sihitaji kuona unakufa kwa Ebola,” aliongea Kai.

Julia hakuwa na neno la kumkatisha tamaa mume wake, alimkumbatia  akionyesha kumpa moyo. Ukweli halisi ulionyesha kuwa jambo hilo lisingewezekana hasa kwa muda mfupi. Kwa kuwa Kai alikuwa amekaa muda mrefu chuoni lakini hakufanikiwa kugundua dawa ya Ebola. Alitembelea maabara kuu ya dunia, alikaa na wanasayansi wakubwa lakini bado dawa haikupatikana.  Hivyo isingewezakana kupatikana kwa muda mfupi, ndani ya siku tatu.

Hivyo alimpa moyo tu mume wake lakini upande fulani hakusadiki kuwa jambo hilo linaweza kufanilkiwa, ingawa alijua kuwa Kai alikuwa amefanikiwa kugundua kinga.

Baada ya kukaa muda mrefu kidogo mle ndani ya sinki, ambako waliongea mengi, Kai alimbeba Julia na kumpeleka chumbani ambapo alimpaka mafuta na kumvalisha lile gauni lake analolipenda kulivaa usiku. Walilala pamoja wakiendelea kuongea mengi.

Siku hiyo ilikuwa ni nzuri sana kwa Kai. Kwani hapo awali alishakuwa ameshakata tamaa ya kuja kulala tena na mkewe kitanda kimoja.

Asubuhi ilifika jua lilichomoza na kuangaza hadi kwenye chumba chao chenye dirisha kubwa. Kai alishtuka kutoka usingizini na kukuta amelala peke yake. Julia hakuwa pale kitandani.

Alishangaa, ilionyesha Julia alikuwa amewahi kuamka. Alishuka kutoka kitandani na kuelekea jikoni ambako alikuta birika la chai likiwa juu ya jiko likichemka. Pembeni alikuta mayai yaliyopikwa, pamoja na vipande vya mkate vilivyopakwa asali na vilainishi vingine vya mikate.

Alistaajabu na kutabasamu. Lakini hata hivyo Julia hakuwepo pale jikoni.

“Mpenziiii!” Kai aliita.

Hakujibiwa, utulivu ulikuwa ni mkubwa mle ndani. Alipiga hatua huku akiendelea kuita.

“Juliaaa! Mke wanguu!.”

Hali ya kutojibiwa ilimtisha alielekea kwenye choo kingine akikiacha choo cha chumbani kwao. Alimkuta Julia akiwa ameinama. Alimkimbilia na kumuinua.

“Juliaaa  uko sawa mke wangu,” aliuliza Kai.

Alishangaa kuona damu zikimtoka masikioni na puani huku akiwa ametapika chakula chenye mabonge meusi. Julia aliinua macho na kumtazama Kai kwa huruma. Alishindwa kumwambia mumewe chochote upesi Kai alimkumbatia huku akitokwa na machozi.

“Pole mpenzi usijali utapona,” aliongea Kai kama mtu aliyechanganyikiwa.

Alimbeba na kumpeleka bafuni ambapo alimuogesha tena na kumbadirisha nguo. Julia hakuwa na neno la kumwambia mumewe. Alibaki kimya huku akitokwa na machozi, akionyesha kuwa alikuwa amekata tamaa ya kuendelea kuishi.

Hali ile ilionyesha kuwa tayari Julia alikuwa ameingia kwenye hatua ya pili ya kuugua. Hatua ambayo damu humtoka mwathirika sehemu zote zenye matundu.

“Kai mume wangu,” aliongea Julia kwa sauti ya chini.

“Naam mke wangu,” alijibu Kai huku akitokwa na machozi.

“Naomba ukubali ombi langu nitakalokuomba,” aliongea Julia.

“Omba lolote nitakukubalia.”

Julia alishusha pumzi na kuipandisha alimtazama Kai aliyekuwa anamvalisha gauni jingine.

“Naomba uniue,” aliongea Julia kauli iliyomshtua Kai.

Japo Kai alishtuka, lakini alicheka kicheko cha kujilazimisha akijua mkewe anamtania.

“Sitanii niko makini,” aliongea Julia.

“Najua akili yako haiko sawa,” alijibu Kai.

Julia alimshika Kai na kumwambia.

“Kama unanipenda naomba uniue.”

“Nakupenda ndio lakini siwezi kufanya ujinga huo.”

“Mume wangu tazama navyoteseka, sifai tena kuendelea kuwa pembeni yako. Damu zimeshaanza kunitoka kila sehemu. Nimegundua siwezi kujifungua na hata kama nikijifungua watoto watakuwa na kasoro kubwa. Sidhani kama unapenda kuona wanao wanazaliwa wakiwa na viungo nusu. Sikujua kuwa wajawazito wenye Ebola wanateseka kiasi hiki.”

“Pamoja na hayo siwezi kukuua,” aliongea Kai kwa hasira huku akitokwa na machozi.

“Kai mpenzi, naomba uniruhusu mimi nipumzike kwa amani. Sahau kuhusu tiba, nimependa kulala mwenyewe. Niache nife Kai, sipendi kuona unateseka kwa ajili yangu. Tafadhali sana.”

Maneno ya Julia yalimuumiza sana Kai, aliyachukulia kama upepo, japo yalikuwa na ukweli kulingana na hali iliyokuwa ikimtesa mkewe.

“Naomba nisikilize mke wangu. Nakupenda sana tena sana. Siwezi kufanya hivyo mapema, lakini na mimi nakuomba  ombi la mwisho, tafadhali nikubalie nami nitakukubalia lako,” aliongea Kai akiwa amemshika Julia mashavu.

“Niambie mume wangu.”

“Naomba ukae na mimi kwa siku tatu  halafu nitalikubali ombi lako.”

“Siku tatu?”

“Ndio.”

“Unaniahidi?”

“Nakuahidi mke wangu, nitakuua. Nachotaka ni kukaa na wewe kwa mara ya mwisho kabla hujaondoka duniani, vumilia hizi siku tatu kisha nitafanya hivyo sawa mpenzi?” aliongea Kai huku akitokwa na machozi mengi.

“Sawa ombi lako nimelikubalia,” alijibu Julia kwa tabasamu la tabu na kumkumbatia mumewe.

Baada ya maongezi hayo ya kutisha, Kai alimlaza Julia na kumwenyesha dawa za Vilter primase pamoja na dawa za kupunguza maumivu. Kisha alimlisha chakula na kumlaza kitandani. Alimuimbia nyimbo nzuri iliyomletea  Julia  usingizi.

Baada ya Julia kulala, Kai alikwenda kufungua traka kubwa lililokuwa na vifaa vyake vya maabara, pamoja na madawa mbalimbali. Vifaa alivyokuwa ametokana navyo London, Uingereza. Alielekea kwenye chumba kikubwa na kuvipanga. Alikifanya chumba hicho kuwa maabara kubwa.

Hii ilionyesha kuwa Kai hakuwa tayari kuona mke wake anakufa kwa ugonjwa huo. Nafsi yake iliyokuwa ikiishi kwenye nafsi ya Julia, ilikataa kuondoka na roho ya Julia na kuucha mwili pamoja na nafsi nyingine ya Kai duniani.

Baada ya kupanga vifaa vyote na madawa ndani ya maabara hiyo, Kai alipiga goti kumuomba Mungu. Machozi yakiwa yanatiririka mashavuni mwake, Kai alimwambia Mungu.

“Baba muumba ardhi na mbingu. Samahani sijakuomba umponye mke wangu bila mimi kuteseka. Nakuomba utumie sayansi yangu kama njia ya muujiza wako. Najua siwezi kugundua dawa ya Ebola kwa akili yangu mwenyewe. Dunia nzima sasa inateseka kutokana na ugonjwa huu. Na hii ni dunia ya mke wangu. Naamini mke wangu akipona basi waliopo duniani wote  wamepona. Nashukuru ulimtuma mtumishi wako ndotoni na kuja kwake hakika kumeonyesha tumaini jipya. Naomba umuokoe mke wangu na dunia yake. Watu wote wapone kupitia Julia. Nipe nguvu ya kutenda, Amina.”

Baada ya sala hiyo, Kai alichukua vitabu vya Ebola na makaratasi yote aliyoandika kuhusu ugonjwa huo. Alisoma kwa zaidi ya masaa manne. Aliingia kwenye intaneti na kuipitia tovuti ya maabara kuu ya dunia. Ili kuona wanasayansi wenzake, walikuwa wanafanya nini kuhusu kugundua dawa ya ugonjwa huo.

Wakati huo vyombo vya habari, vilishakuwa vimetangaza kuwa nusu nzima ya dunia ilishakuwa imeshashambuliwa na virusi vya Ebola. Zaidi ya watu milioni 900 walishakuwa wamepoteza maisha na wengine wengi wakiishi na virusi hivyo.

Kai alianza kazi ya kutafuta dawa hiyo akiwa nyumbani kwake. Alihitaji kufanya hivyo ndani ya siku tatu. Tayari alishakuwa ameweka ahadi kwa Julia kuwa baada ya siku tatu, atamkatisha uhai wake ili akapumzike. Hakupenda hilo litokee na hakuwa tayari kufanya hivyo alihitaji mke wake apone.

Aliamini kama alifanikiwa kugundua kinga ya virusi vya ugonjwa huo, basi atafanikiwa pia kutengeneza dawa itakayoua virusi ndani ya mwili wa binadamu, ambayo itakuwa ni tiba. Moyo wa Julia ulikuwa ukidunda kwenye nafsi ya Kai. Mioyo ya watoto wake ilikuwa pia kwenye moyo wa Kai.

Alianza kuvitumia vile viunganishi alivyokuwa amevitumia wakati wa kugundua kinga. Seli za mmea wa Sanbira pamoja na kemikali zilizoundwa kwa chembe hai za damu.

Nini kitafuatia? Usikose kesho   

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU