Wenger aona ni bora kumwachia Sanchez aondoke bure kuliko kumuuza

Wenger aona ni bora kumwachia Sanchez aondoke bure kuliko kumuuza

435
0
KUSHIRIKI

 

Alexis Sanchez

LONDON, England

KWA lugha nyingine unaweza kusema ni kwamba amepiga hesabu kali, baada ya Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, kusema kuwa yeye pamoja na klabu yake wanafikiria kujitoa kafara kwa ajili ya fedha kwa kumwachia nyota wao, Alexis Sanchez, aondoke akiwa kama mchezaji huru mwakani kuliko kumuuza msimu huu.

Sanchez anamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu na inavyoonekana hadi sasa nyota huyo wa timu ya Taifa ya Chile hana mpango wa kusaini mkataba mpya na huku kuzidi kuwapo taarifa zinazodai kuwa anataka kuondoka na kwenda kujiunga na  Manchester City, Paris Saint-Germain na  Bayern Munich.

 

Hata hivyo, Wenger ameendelea na msimamo wake akisema kuwa hana mpango wa kumuuza Sanchez hata kama mkataba wa straika huyo wa zamani wa Barcelona kuwa unakaribia kumalizika.

“Hii itakuwa ni kafara ya kifedha. Ni kafara ambayo unatakiwa kupiga hesabu ni gharama zipi itakugharimu,” alisema Wenger kuhusu Sanchez ambaye alikuwa nje ya uwanja wakati wa mechi yao ya fungua dimba katika michuano ya Ligi Kuu England dhidi ya Leicester City  na huku akijiandaa kesho kuikosa mechi dhidi ya Stoke City kutokana na maumivu ya tumbo.

“Unapomwachia mchezaji akaondoka na kisha ukanunua mwingine unakuwa unaingia gharama kubwa kuliko kile ulichokipoteza. Vile vile unapoongeza mkataba inaweza kukugharimu kiasi kikubwa tofauti na kile ulichokipoteza unamwachia, hivyo unatakiwa kutafakari urefu wa mkataba vile vile kiasi ambacho mchezaji anakihitaji,” aliongeza Mfaransa huyo.

 

Alisema kuwa baada ya kuangalia hayo, suala la kuachia fedha linaweza likawa si kubwa kama wengine wanavyotafakari.

Hata hivyo, Wenger alisema huo ndio mtazamo wake, lakini atafanya hivyo  baada ya bodi ya wakurugenzi kama watakubaliana naye na akasema kuwa endapo watampinga basi atakubaliana nao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU