PLUIJM AIFANYIA UKACHERO MWADUI

PLUIJM AIFANYIA UKACHERO MWADUI

882
0
KUSHIRIKI

331368_heroa

NA MASYENENE DAMIAN, MWANZA

KOCHA wa Singida United, Hans van der Pluijm, ameifanyia ukachero timu ya Mwadui iliyokuwa ikicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Pamba jijini hapa.

Pluijm alikuwa uwanjani kuisoma timu hiyo, itakayofungua dimba na Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Agosti 26, mwaka huu, Mwadui Complex, mkoani  Shinyanga.

Katika mchezo huo, Mwadui iliichapa mabao 5-3 Pamba inayojiandaa na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL), itakayoanza Septemba 16, mwaka huu.

Mabao ya Mwadui yaliwekwa nyavuni na Salim Khamis aliyefunga mawili, Awadh Juma aliyefunga mawili na Nyanda Babi aliyetupia moja.

Kwa upande wa Pamba waliofunga ni  Peter Magata, Emannuel Manyanda na Meshack Kikona kwa njia ya penalti.

Akizungumza na BINGWA jijini hapa,  Kocha Mkuu wa Mwadui, Jumanne Ntambi, alisema pamoja na mapungufu yaliyoonekana katika safu ya ulinzi, lakini ana imani kubwa na idara ya ushambuliaji.

“Vijana wanakwenda vizuri, wamejenga imani kubwa japokuwa bado mabeki wangu wana matatizo machache kwa mfano leo (juzi) wameruhusu mabao matatu lakini kiukweli timu iko safi, vijana wanashindana.”

Pamba ilifanikiwa kushinda mabao 3-1 dhidi ya Mbao FC katika mchezo wa kwanza wa kirafiki kujiandaa na Ligi Daraja la Kwanza Bara.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU