DUNIA YA MKE WANGU

DUNIA YA MKE WANGU

354
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia

Usingekuwa huu ujauzito, ningevumilia kuishi na wewe kwa kipindi hiki cha hatua ya pili ya kuugua. Lakini kutokana na hii mimba, nateseka sana halafu si unajua virusi vinazaliana kwa kasi?” aliongea Julia kwa machozi mengi akimshika shika Kai kichwani.

Na wakati anaongea hayo, damu zilikuwa zikimtoka puani, masikioni pamoja na mdomoni. Kai alilia sana kama mtoto mdogo akimshika Julia kwa nguvu. Huzuni zilikuwa zimetawala mle ndani.

 “Naomba ukachukue sindano unichome. Nahitaji sindano ya Ritrino ili nife nikiwa usingizini. Fanya hivyo mume wangu nionee huruma,” aliongea Julia akimuondoa Kai kwenye kifua chake.

Kai alinyanyuka pasipo kupenda, akamtazama mkewe mara nyingi. Kisha akaenda maabara kwenda kuchukua sindano ya Ritrino, sindano ambayo sumu yake humuua mtu akiwa usingizini.

 

SASA ENDELEA

Alishuka ngazi kutoka chumbani na kuelekea maabara. Huzuni isiyo na mfano ilimtawala. Ingawa alikuwa na imani kuwa amepata dawa ya ugonjwa wa Ebola, lakini aliona mke wake alikuwa amefika kiwango cha mwisho cha kuvumilia. Masaa sita yalikuwa yamebakia ambayo yangemthibitishia kuwa dawa ya Sanbira tricony aliyoigundua ilikuwa na madhara kwenye mwili wa binadamu au haikuwa na madhara.

Hata hivyo, alikuwa amepata kujua kuwa dawa hiyo haikuwa na madhara ya muda mfupi baada ya kuitumia. Hii ilitokana na kutohisi tofauti yoyote katika mwili wake tokea alipoitumia saa moja iliyopita. Ilibaki kuthibitisha tu kama dawa hiyo ilikuwa na madhara yanayoweza kutokea baada ya siku na baada ya miaka.

Yeye kama mwanasayansi alijua anaithibitisha vipi dawa hiyo, ili ajue kama haikuwa na madhara ya miaka kadhaa baada ya mgonjwa kuitumia.

Maumivu na hitaji alilokuwa akilihitaji Julia, lilimuumiza sana. Ni kweli alikuwa akiyaona mateso anayopata mkewe kutokana na hatua ya pili ya kuugua, lakini ombi la mkewe la kutaka kumuua lilimfanya aione siku hiyo mbaya sana kwenye maisha yake.

Aliingia maabara na kuchukua sindano kama mkewe alivyomtaka. Alirudi chumbani akiwa na machozi mengi ya kufutwa. Alimsogelea Julia taratibu, huku akihema kwa upole. Wakati huo Julia alikuwa akitazama dirishani akiitazama bahari ya hindi.

Julia aligeuka na kumkuta Kai akilia kilio kikubwa. Huku akiwa na sindano mkononi. Alimsogelea mumewe na kumkaribia kabisa. Kai alimbeba na kumlaza kitandani.

“Kai wewe ndio mume bora ambaye sijapata kuwahi kumuona kwenye dunia hii. Hata marafiki zangu hawana mume kama wewe. Najivunia kuolewa na wewe. Endapo ningekuwa nimekukosa, ningekuwa nimekosa tunda bora la rohoni. Ninaondoka duniani lakini ninaamini nitakuona siku moja,” aliongea Julia kwa machozi.

Kai alijikaza kiume asilie kilio kikubwa maana maumivu aliyokuwa akiyahisi, yalikuwa ni makubwa. Julia aliendelea kuongea akimfariji Kai kwa mara ya mwisho.

“Now I am not scared to go,” ( Sasa siogopi kwenda) aliongea Julia.

“I love you,” (nakupenda) alijibu Kai akiwa amemshika Julia vilivyo.

“I love you too,”(nakupenda pia) alijibu Julia kwa huzuni kuu.

“Naogopa sana mke wangu. Siwezi kuishi,” aliongea Kai.

“Mungu akulinde usije ukachukua uamuzi wa kunifuata mimi. Mungu hatakusamehe. Naomba unichome sasa  nilale. Usijali tutaonana katika ufalme wake. Nakutakia maisha mema,” aliongea Julia akitokwa na chozi la mwisho.

Kai alimbusu Julia akamshika mkono na kumchoma sindano huku akilia sana. Baada ya sekunde saba, Julia alifumba macho usingizi mzito ulimchukua.

Baada ya Kai kumaliza zoezi hilo, alifuta machozi na kujivika roho ya ujasiri. Alizunguka mle chumbani kama kichaa, akikizunguka pia na kitanda alicholala Julia.

Kai alikuwa amemdanganya tena mkewe hakuwa amemchoma sindano ya Ritrino, sindano ya sumu. Bali alikuwa amemchoma ile sindano aliyokuwa amemchoma mwanzo ya kumuongezea usingizi wa kawaida. Ina maana hakuwa amemuua kama Julia alivyokuwa amehitaji. Hakuona umuhimu wa kufanya hivyo kwa kuwa alibakisha saa chache za kuthibitisha kama dawa ya Ebola aliyokuwa ameigundua ilikuwa haina madhara kwa binadamu.

Alipumzika pembeni kwa Julia akiitazama saa ya ukutani. Wakati huo ilionyesha kuwa ilikuwa ni saa 8:45 mchana. Aliendelea kusubiri huku akihangaika moyoni. Viungo vya mwili wake vyote vilitetemeka. Alitamani kusimama na kuinuka. Huku akizidi kumuomba Mungu aendelee kuwa upande wake.

Baada ya saa saba kupita, Kai alikwenda upesi maabara, akajichoma sindano na kuivuta damu yake. Akaiweka kwenye kifaa cha Riccer biker. Kisha akaichanganya  damu hiyo na dawa ya Anvirrer. Akaitikisa mara nyingi na kuiweka kidogo kwenye kioo cha hadubini.

Aliichunguza mara moja na kupata majibu. Baada ya kutoa jicho kwenye hadubini, Kai alishusha pumzi na kupiga magoti.

“Asante Mungu hakika wewe ni mfalme unayepaswa kusujudiwa. Nitakushukuru siku zote za maisha yangu. Hakika umenisaidia kumponya mke wangu pamoja na dunia yote kwa sayansi niliyoipenda. Asante pia kwa kusikia kilio cha watu, pande zote za dunia. Unastahili sifa,” aliongea Kai akimshukuru Mungu kwa machozi akilia kama mtoto mdogo.

Kai alikuwa amepata majibu kuwa dawa ya Ebola aliyokuwa ameigundua, dawa ya Sanbira tricony, ilikuwa haina madhara yoyote kwa binadamu. Alithibitisha hilo baada ya matokeo aliyokuwa ameyangoja kwa saa saba kuonyesha kuwa dawa hiyo haikuwa na athari zozote kwa mtumiaji hata kwa miaka mingi ijayo.

Furaha yake ilikuwa kubwa na isiyoelezeka. Alilia kama mtoto mdogo, akicheka peke yake kama mtu aliyekuwa anakwenda kurukwa na akili.

Upesi aliivuta dawa ya Sanbira tricony kwa sindano na kuelekea haraka chumbani. Alipofika chumbani, alimsogelea Julia mke wake kipenzi, aliutafuta mshipa mkubwa kwenye mkono wake wa kulia na kumchoma ile sindano. Aliisukuma nusu nzima ya dawa ya Sanbira tricony. Dawa iliingia kwenye mwili wa Julia na kuanza kusambaa kwa kasi.

Alimtundikia pia dripu ya maji. Maji hayo aliyachanganya kidogo na dawa ya Ebola. Muda wote alikuwa akitabasamu, furaha ilikuwa kubwa kwa mwanasayansi Kai Luda, hakuamini kama ni kweli mke wake alikuwa anakwenda kupona ugonjwa wa Ebola.

Baada ya kufanya hivyo, alikwenda ufukwe wa bahari kwenda kupumzika. Alisubiri Julia aamke. Dawa ya usingizi aliyokuwa amemchoma ilikuwa ni ya saa sita. Hivyo, Julia angeamka saa mbili usiku.

Julia alipokuwa akichomwa sindano hiyo, alijua kuwa anachomwa sindano ya sumu, sumu aina ya Ritrino ambayo humuua mtu akiwa usingizini. Lakini haikuwa hivyo, Kai hakumchoma sindano hiyo.

Saa mbili usiku ilitimia, Julia alifumbua macho na kujikuta akiwa mzima, akiwa pale pale kitandani. Hakuamini, alitazama huku na kule asiamini kama bado alikuwa katika dunia hii. Pembeni yake aliiona dripu. Moja kwa moja alijua kuwa mume wake alikuwa amemuongopea. Hakuwa amemuua kama walivyokubaliana.

Julia alikasirika na kuchukia kitendo cha mume wake kumchoma sindano ya usingizi badala ya sindano ya sumu. Alimkasirikia kwa kuvunja ahadi na kumuongopea.

Lakini hata hivyo, alijishangaa baada ya kujiona ni mwepesi kidogo. Hali yake ya mwili ilikuwa tofauti na hapo mwanzo. Maumivu ya kichwa aliyokuwa akiyapata hapo awali  yalikuwa yamepungua. Alijiuliza nini kilikuwa kimemtokea. Akiwa katika sintofahamu hiyo, Kai aliingia mle chumbani.

Macho yao yaligongana, Kai alitabasamu kisha akapiga hatua kumsogelea Julia aliyejawa na sintofahamu huku akiwa na ndita tatu usoni. Kai alipomfikia Julia amlisogelea na kumkumbatia kwa nguvu.

“Umeniongopea tena kwanini hukuniua, hunipendi?” aliuliza Julia kwa hasira.

“Punguza hasira mke wangu, wewe sasa ni mzima,” aliongea Kai akimtazama Julia usoni.

“Kivipi mbona sikuelewi?”

“Tutakuwa wote katika maisha yetu ya ndoa mimi na wewe. Hakika Mungu ni mkuu kwetu.”

“Sitaki kusikia misamiati yako. Nataka kujua kwanini hujaniua?”

“Kwa sababu nakupenda na siwezi kuishi katika sayari hii bila wewe Julia.”

“Ina maana unapenda mimi niteseke?”

“Julia mke wangu wewe ni mzima bado siku tatu upone kabisa.”

“Unanitania?”

“Sikutanii mke wangu, kwani nimefanikiwa kupata dawa ya Ebola,” aliongea Kai na kumuweka mke wake mdomo wazi akimshangaa asiamini ayasemayo.

“Je kwa sasa unahisi tofuti yoyote katika mwili?” Kai aliuliza.

Julia alijitazama mwili wake na kujibu.

“Ni kweli mwili wangu ni mwepesi tofauti na mwanzo.”

Nini kitafuatia? usikose kesho

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU