HONGERA WANACHAMA SIMBA KWA KUJITAMBUA

HONGERA WANACHAMA SIMBA KWA KUJITAMBUA

425
0
KUSHIRIKI

JANA wanachama wa timu ya Simba walifanya mkutano wao mkuu kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya kutoka mfumo wa sasa na kuingia kwenye mpya kutumia utaratibu wa kununua hisa katika uendeshaji wa klabu hiyo.

Mkutano huo umefanyika baada ya kuwapo kwa kilio cha muda mrefu kutoka kwa watu wa kada mbalimbali, wakikosoa na kutaka mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa uendeshaji wa klabu kongwe za soka nchini za Simba na Yanga.

Msingi wa ukosoaji umekuwa ukijikita katika ukweli ulio wazi kwamba, pamoja na klabu hizi kuwa kongwe kwa zaidi ya nusu karne bado hakuna mafanikio ya maana yaliyofikiwa iwe ni katika malengo ya kuanzishwa kwao kisoka na hata kiuchumi.

Sisi BINGWA tunaunga mkono jitihada zilizofanywa na wanachama hao hadi kufikia makubaliano ya kubadili uendeshaji wa klabu hii.

Kuunga kwetu mkono kunatokana na kwamba tuna imani klabu hiyo itaweza kupiga hatua kimaendeleo, baada ya kuondokana na mfumo wa kutegemea wanachama ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukichangia klabu hizo kufanya vibaya si kimataifa na hata pia katika michezo ya ndani ya nchi.

Ukiangalia tangu kuanzishwa kwa klabu hizi hakuna hata moja iliyofanikiwa kutwaa ubingwa wowote wa michuano mikubwa ya Afrika inayoendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), zaidi ya kuishia kuwa wasindikizaji.

Matatizo haya yamekuwa yakisababishwa katika eneo la menejimenti na uendeshaji wa klabu hizo, kutokana na kuwa na matatizo    lukuki ambayo kimsingi ndiyo chanzo cha kushindwa kufikia mafanikio katika soka la Afrika.

Hali hiyo ya kuendeshwa kwa mfumo wa uanachama ambao katika hali ya sasa hauwezi kabisa kukidhi changamoto zinazojitokeza.

Soka la sasa linahitaji misuli ya kiuchumi kiasi kwamba michango ya wanachama na makusanyo ya mapato getini hayawezi kabisa kusaidia chochote zaidi ya kutatua gharama ndogo ndogo. Mfumo huu ni wa utegemezi, unatengeneza matundu mengi katika kuendesha klabu hizi.

Ni mfumo ambao hakika ndicho chanzo cha mkwamo wa klabu zetu nyingi zilizowahi kutamba huko nyuma.

Itoshe kusema kwamba mfumo huu ndio sasa umekuwa chanzo cha kuzalisha ‘miungu watu’ ndani ya klabu hizo. Kila anapojitokeza mtu mwenye uwezo wa kifedha na akaonesha kujiweka karibu na klabu hizi hata kwa maslahi yake binafsi ataonekana mwokozi.

Neno lake huwa sheria na ndilo hufuatwa. Anaweza kutoa amri zozote na asipingwe na yeyote hata kama ni fyongo.

Miungu hawa wamekuwa na nguvu hata ya kuamua hatima ya timu zinapocheza uwanjani. Ndio wanaosajili na kupanga wachezaji uwanjani. Ndio wanaoamua ushindi wa timu zao kupitia kuwamiliki wachezaji na kuwaelekeza nini wafanye uwanjani. Wanawekeza rasilimali na fedha kuwaridhisha mashabiki kupitia ushindi wa uwanjani, huku klabu zikiwa hoi bin taabani kwenye akaunti.

Baadhi ya wanachama wenye njaa zao nao hawako nyuma katika kutumia mfumo huu kujinufaisha. Wataanzisha migogoro ili wazimwe kwa fedha.

Wengine wamekuwa wakijipachika  kazi ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya getini ambayo yamekuwa yakiishia mikononi mwao huku klabu zikifa njaa.

Kwa ujumla mfumo wa wanachama katika uendeshaji klabu za soka umepitwa na wakati, haufai na hauna tija katika maendeleo ya soka la kisasa, hivyo BINGWA tunawapongeza wanachama wa Simba kwa hatua waliyoifikia na tunaziomba klabu nyingine kuiga mfano kama huo kwani unaweza kuwa mkombozi wa soka letu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU