UFALME WA KILA MMOJA UHARIBU MAPENZI

UFALME WA KILA MMOJA UHARIBU MAPENZI

355
0
KUSHIRIKI

Ili watu zaidi ya mmoja waweze kuishi pamoja kwa amani, ni lazima mmojawapo ajifanye mnyonge. Hakutaweza kupatikana maelewano baina yao ikiwa kila mmoja atajifanya mjuaji.

Watu waliopo katika mahusiano katu hawawezi kuwa na amani kama wakiwa na hali ya kila mmoja kutaka kuonekana zaidi bila kutoa upenyo wa mwingine kusikika au kumrekebisha kunapokuwa na kosa.

Mapenzi si kama ulingo wa siasa kila mmoja kung’ang’ania kutetea hoja zake hata kama si thabiti. Mapenzi ni kusikilizana na kuamua kuelewana bila kushurutishana.

Katika mahusiano kunapokuwa na kitu mfano wa ushindani, basi wahusika hawawezi kuwa na amani tarajiwa katika mahusiano yao. Katika ustawi wa amani katika mapenzi yoyote duniani, ni lazima mmoja kati ya wahusika ajifanye’ mdogo’ kwa namna flani. Kunapokuwa na hali kama hii, kila siku ugomvi au makwazo ya hapa na pale huwa yanatatulika kirahisi.

Kupatikana utulivu katika mahusiano inahitaji mmoja kati ya wahusika katika mahusinao husika awe  mpole na mwenye hekima katika kuweza kunusuru mahusiano.

Kila mmoja anapojifanya kijogoo hakuna mahusiano yenye nguvu kuvumilia hali hiyo. Ni lazima tu kuachana kutatokea. Mafahali wawili katu hawawezi kukaa zizi moja!

Kwa aliye na busara na hekima akiona mwenzake anapanda juu, yeye hushuka chini na kuangalia namna ya kuweza kutatua tatizo husika. Mwenye busara katu hawezi kuruhusu malumbano baina yao.

Katika namna yoyote hujitahidi kutatua mgogoro hata kama yeye ndiye mkosewa. Ila mkosefu wa busara huwa kinyume chake. Na matokeo yake, katika uhusiano wake amani hukosekana na mwishowe wahusika huishi kimazoea na si kwa mapenzi ya dhati.

Kukaripiana na mwenzako inapotokea kutofautiana si kutatua migogoro bali ni kuzidisha petrol katika moto wa ugomvi wenu. Kukaa kimya au kujitahidi kutatua ugomvi hakumaanishi unyonge wala ujinga, bali humaanisha busara na ukomavu wa akili.

Unapoamua kuwa chini kunapotokea kutoelewana kunazidi kuyaweka mahusiano yenu katika hali ya kuendelea kuwa hai.

Malumbano huchochea zaidi hisia za hasira na ghadhabu na matokeo ya yote ni wahusika kujikuta kufanya matendo ambayo ni lazima tu watakuja kujutia baadaye.

Katika hasira kunakuropoka au kupigana. Katika hasira kuna kuchukua maamuzi mabaya na kutoa kashfa. Ukifika huko unadhani unayaweka mahusiano yako katika upande upi, kama si wa kupoteza? Fikiri tena, mafahali wawili hawakai zizi moja daima.

Tambua kuwa kila unapolumbana na mpenzi wako unapunguza nguvu ya upendo baina yenu. Kwa maana hapo hapatakosa maneno ya karaha na kukera. Ni nani wa kuyafurahia maneno hayo? Nani yuko radhi kumsikia mpenzi wake anayempenda akimtolea kashfa? Hakuna.

Kwanini usikubali kuwa mnyonge baada ya kuanza malumbano baina yenu ili mahusiano yenu yaendelee kuwa na uhai na amani? Achana na kujiona kijogoo badala yake kuwa na kinywa kilichojaa maneno matamu na yenye kumfanya mwenzako afurahie upamoja wenu.

Maneno matamu ambayo karibu kila muda akiyafikiria moyo wake uwe na faraja na kumfanya atamani kuwa na wewe muda wote. Wapenzi wenye uwezo wa kuepuka migogoro ni wapenzi wenye asilimia kubwa ya kuweza kudumu kwa muda mrefu katika mahusiano yao.

Unapokaa mbali na malumbano na mpenzi wako, maana yake unajiepusha na maneno ya karaha na ya kukera. Ukifanya hivyo unamaanisha kuwa unatengeneza vizuizi vya kuleta mvurugano na machafuko katika mahusiano yenu. Kitu kitakachokupelekea katika raha na amani ya kweli katika mapenzi.

ramadhanimasenga@yahoo.com 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU