HUWEZI KUPATA AMANI KUPITIA SURA WALA UMBILE LAKE, ANGALIA HILI SUALA

HUWEZI KUPATA AMANI KUPITIA SURA WALA UMBILE LAKE, ANGALIA HILI SUALA

478
0
KUSHIRIKI

NI vyema kila mmoja akawa na mtu anayeamini ni mzuri na anayemvutia. Unapokuwa na mtu wa aina hii katika maisha, kila muda utakuwa unajihisi kuwa naye karibu na kufanya kila jambo zuri unalotakiwa kufanya.

Tofauti na mtu wa aina hii itakuwa si ajabu kufanya mambo tofauti na matarajio yake. Ila mbali na ukweli huo, haipaswi kufanya chaguo la mtu kwa kigezo cha uzuri wa sura au umbile. Ila ni vyema ukawa na mtu ambaye unahisi kwako ni mzuri na bora mbele ya macho yako. Umeelewa hapo?

Yaani ni vyema kuwa na mtu ambaye moyo wako umemchagua na kumuona mzuri na bora. Na wala haifai kuwa na mtu kwa kigezo cha uzuri wa sura au umbile lake.

Hata kama atakuwa anasifiwa vipi na jamii inayomzunguka ila kama ndani ya moyo wako hana thamani na ubora halisi wa mapenzi, huwezi kuuona uzuri wake kwa kipindi kirefu.

Hii ni tofauti na mtu ambaye kuwa naye imesababishwa na hisia zako. Yeye anaweza kuwa si mzuri sana kwa wengine au asiwe mwenye kuvutia kwa wengi  ila kama hisia zako juu yake ni za dhati, basi kila siku atakuwa mzuri na wa maana katika maisha yako. Hujawahi  kuona hali hii?

Unakuta msichana/ mvulana anayeonekana kama hana mvuto mkubwa akiwa katika mahusiano na mtu anayemwona mzuri na bora kuliko wale bora mnaowasifia?  Haiwi hivi kwa sababu nyingine ila huwa hivi kwa kuwa upendo uliopo katika moyo wa mhusika unafanya kazi juu yake ndiyo maana macho yake yanaona tofauti na wengine. Unaitaka amani katika mahusiano yako?

Angalia ni wapi moyo wako unapohitaji kuliko kufikiria sifa za kuwa na mtu fulani mtaani. Amani yako katika mahusiano haijashikwa katika sura wala umbile la mtu. Amani yako itapatikana kama moyo wako utakuwa na hisia za kweli na yeye akajihisi hivyo kwako. Sura na umbile ni nakshi tu, ila upendo ndiyo huwa unatoa thamani na maana halisi ya kuwa na fulani katika mahusiano.

Ikiwa kweli unahitaji kuwa katika mahusiano yenye kutoa tafsiri halisi na matokeo bora, unahitaji kuruhusu moyo wako ufanye kazi kuliko macho yako. Ni kweli kutokana na umbile na urembo wa sura yake unaweza kudhani ukiwa naye kila siku utakuwa na furaha na amani. Ila huo si ukweli.  Maisha ya ndoa au mahusiano ya muda mrefu yatakupa kitu usichokitegemea.

Baada ya kuishi naye kwa kipindi kirefu na kuuzoea uzuri wake unaweza kuona kuna kitu kimepelea katika mahusiano yenu. Hapo ndipo visa na ugomvi mdogo hukuzwa na kuonekana mkubwa. Katika akili ya haraka haraka watu husema “fulani mjinga mbali na kuwa na mwanamke mzuri kama Yule ila anamletea visa?”

Ila kimsingi visa hivi ama ugomvi huu huja ‘automatically’. Mhusika hujikuta akimkera mwenzake bila kujali mwonekano wake kwa sababu ndani ya moyo wake hana thamani kitu kinachopelekea hata macho yake sasa yaanze kumtazama katika maana tofauti.

Moyo wako na wake ukiwa umeridhiana bila kujali mwonekano wake daima atakuwa bora kwako kama ilivyo wewe kwake. Upendo si suala la anaonekana vipi ila ni suala la namna unavyomhisi katika moyo wako.

Ikiwa nguvu ya umbile lake imekuvuta kwake, kuna hati hati ya mahusiano yako kuwa na raha katika kipindi kifupi kisha baada ya hapo yafuate madhila yasiyokwisha na hatimaye kupelekea kifo cha mapenzi yenu.

Ila kama hisia zako na zake zimegusana kidhati, hata kama unaonekana vipi haitakuwa neno kwake, utakuwa bora na mwenye kuvutia. Bila kujali unaonekana vipi ila kwake utakuwa bora na mwenye kuvutia.

Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia (Psychoanalyst)

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU