MAANDALIZI FAINALI 2019 YASHIRIKISHE WADAU, SERIKALI

MAANDALIZI FAINALI 2019 YASHIRIKISHE WADAU, SERIKALI

301
0
KUSHIRIKI

SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF), jana lilizindua rasmi kampeni za maandalizi ya michuano ya fainali za vijana Afrika wenye umri chini ya miaka 17, zikatazofanyika mwaka 2019.

Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam chini ya Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia, ikiwa ni kampeni ya kuhakikisha michuano hiyo inafana.

Hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuandaa michuano kama hiyo, ambayo ilianzishwa miaka 32 iliyopita tofauti na nchi kama Rwanda, Ghana, Nigeria, Afrika Kusini, Misri na Angola ambazo zimewahi kufanya hivyo kwa timu za vijana na za wakubwa.

Licha ya kuwa mara ya kwanza kuandaa michuano hiyo, pia itakuwa ni mara ya pili kwa timu ya Taifa ya Tanzania kushiriki michuano hiyo, baada ya ile iliyofanyika nchini Gabon ambapo ilitolewa katika hatua ya makundi.

Sisi BINGWA tunalipongeza Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwa kutupatia nafasi kama hiyo ambayo tunaamini itamaliza kiu ya Watanzania ya kuandaa michuano ambayo inasimamiwa na shirikisho hilo.

Pamoja na pongezi hizo, tunachoomba ni kuona maandalizi ya michuano hiyo yanaanza mapema kwa kuishirikisha Serikali, TFF na wadau wengine wapenda soka kwa hapa nchini.

Ombi letu hilo linatokana na kwamba, tumeshuhudia uwezo uliooneshwa na timu shiriki kama Ghana, Mali, Guinea na Niger ambazo zilishiriki katika fainali zilizopita zilizofanyika nchini Gabon na kufanikiwa kuliwakilisha vema Bara la Afrika katika fainali za dunia, zitakazofanyika Oktoba mwaka huu nchini India.

Kuandaa fainali hizo hakutoshi bali tuhakikishe  tunafanya vizuri, kwani tulishuhudia jinsi Gabon ilivyotia aibu baada ya kuandaa michuano hiyo ambapo ilifungwa jumla ya mabao 10 katika mechi tatu za hatua ya makundi na kuondolewa mapema katika michuano hiyo.

Hivyo ni lazima tujizatiti mapema kwa kuandaa timu imara, ambayo itaweza kupambana na timu hizo kutoka mataifa ya ukanda wa Afrika Magharibi ambayo yamepata mafanikio makubwa.

Lakini pamoja na hayo, maandalizi hayatakuwa na maana ama kuzaa matunda endapo wadau hao hawatakaa pamoja.

Kwa upande wa TFF pamoja na kuwa imeshaanza maandalizi hayo kwa kuchagua wachezaji watakaoiwakilisha nchi, wanatakiwa pia kuhakikisha benchi la ufundi linafanya kazi zake kwa weledi  ili kuandaa timu imara ambayo itabakiza kombe hilo nyumbani.

Maandalizi hayo yanatakiwa kuhusisha mechi za kirafiki za mara kwa mara, ili kuiwezesha timu hiyo kuzoea  mikikimikiki.

Katika hilo, BINGWA  tunaamini  viongozi wa TFF ambao wamekabidhiwa jukumu hilo kwa sasa watatumia jitihada zilizotumika kuandaa Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za Gabon  ili kuandaa Serengeti Boys ya 2019.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU