CHANZO CHA WAPENZI KUCHOKANA

CHANZO CHA WAPENZI KUCHOKANA

716
0
KUSHIRIKI

NI ndoto ya kila mmoja kuwa katika mahusiano ya raha, faraja na amani kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Ila kwa bahati mbaya kabisa  waliopo katika aina hiyo ya maisha si wengi, ukilinganisha na idadi ya waliopo katika mahusiano. Wengi wao ni majuto na karaha.Tayari wameshachokana.

Suala la kuchokana katika mahusiano kwa aina flani sasa linaanza kuonekana kama suala la kawaida miongoni mwa wapendanao. Si ajabu tena kusikia mtu akisema: “Dah wanajifanya wanapendana…. ila muda si mrefu watachokana tu”. Watu wengi wana fikra hizo.

Wengi wanaamini kuchokana kwa wapenzi ni suala ambalo haliepukiki. Wapo pia wanaoamini kuwa katika mahusiano kwa muda mrefu hupelekea wahusika kuchokana. Si kweli hata kidogo.

Wapo baadhi ya watu waliokuwa katika mahusiano kwa muda mfupi sana na bado wakachokana. Moja ya sababu ya wapendanao kuchokana si kuwa katika mahusiano husika kwa muda mrefu. Hapana.

Suala hapa si muda wa kukaa katika mahusiano. Kuna kitu kingine. Vifuatavyo ni vitu vinavyochangia watu kuchokana.

LAWAMA

Wengi huwa hawalitizami tatizo hili, ila pia ni sumu katika mapenzi. Tabia ya baadhi ya watu kuendekeza lawama zisizo na maana dhidi ya wapenzi wao huchangia kuyafanya mapenzi yao yazorote.

Kwa kawaida mtu anapoona analaumiwa bila sababu ya msingi wala maana huanza kujihisi kero. Katika hatua za mwanzo ataanza kuchukia lawama zenyewe.

Kisha baadaye ataanza kumchoka na  kumpuuza mtoa lawama.   Unapoendekeza lawama zisizo za lazima kwa mwenzio hugeuka kero kwake.

Na katika suala la mapenzi unapogeuka kuwa kero badala ya faraja na liwazo kwa mwenzako, ujue muda si mrefu stori katika mapenzi yenu itabadilika. Muda si mrefu utaanza kuyaona mabadiliko.

Hawezi kukujali sana kama mwanzo maana umeshakuwa kero kwake. Ziangalie vizuri lawama zako. Kama hazina maana ni vyema ukaachana nazo, kwa maana  ni sumu katika faraja ya kweli ndani ya mahusiano yako.

KURUDIA MAKOSA

Haijalishi ni mtiifu au ana maadili kiasi gani, kila binaadamu hukosea. Na hiyo ni moja kati ya sifa inayomtofautisha binaadamu na malaika.

Ila mbali na suala hilo, binaadamu mwenye akili na mwenye kuheshimu hisia za wengine, huwa anapaswa kujifunza kutokana na makosa. Mtu anaposhindwa kufanya hivyo huchukuliwa kama jeuri au katili.

Katika suala la mapenzi kuomba msamaha kuna thamani yake. Tena kubwa.

Mtu aombapo msamaha huwa ni ishara ya kuelewa na kuthamini. Na mara nyingi kwa wapenzi waliojaa hekima na upendo husameheana pale wanapokoseana.

Kukoseana kwa binaadamu ni suala ambalo ni ngumu sana kuliepuka. Kutokana na kuwa ni moja kati ya maumbile yake. Ila pia mtu anapoomba msamaha na kusamehewa na kuendelea kurudia makosa. Huanza kutazamwa katika mtazamo tofauti.

Huonekana kama mtu asiyejali na kuthamini. Taratibu watu huanza kumtoa maana. Wengine huanza kuhisi ni mtu asiyefaa kuthaminiwa wala kuaminiwa.

Katika maisha ya kimahusiano hali haiko tofauti pia. Mtu anayekosea mara kwa mara huanza kuonekana kama asiyejali na kuthamini hisia za mwingine. Na mara nyingi hali kama hii ikitokea, mkosewa huanza kuhisi anafanyiwa kusudi.

Huanza kuhisi kama yupo kwa ajili ya kubembeleza penzi kwa mtu asiye stahili. Kuanzia hapo huanza kutomjali sana kwa kuamini ni mtu asiyefaa.

Kutokana hatakuwa anamjali sana hata kiwango cha upendo juu yake huwa kinapotea tu. Zile bashabasha na mahaba aliyokuwa anamuonesha mwanzo nayo huyeyuka. Hali kama hiyo inapotokea tu, kila mmoja huanza kumuona mwenzake kuwa ni udhia katika furaha yake. Kwa maana mkosewa atahisi anaonewa huku pia mkosaji atahisi hapati alichokuwa anapata mwanzo kutoka kwa mwenzake. Neno kuchokana hapo huchukua nafasi.

KUTOBADILIKA

Hapa inabidi tuelewane vizuri. Ninaposema kubadilika, namaanisha kubadilika katika hali nzuri zaidi. Si kubadilika tu.

Mabadiliko yanayoboresha kitu huwa ni yale yanayokuwa chanya. Haya ninayoyamaanisha mimi. Si yale ya akina flani.

Wapenzi wengi hili hawana. Kila siku wao ni yaleyale. Maongezi aliyoyatumia kumchombeza mwenzake miaka mitatu iliyopita ndiyo haya haya anayotumia mwaka huu.

Maana kila kitu unachosema kwake ni marudio. Hapa pia ni lazima tuwekane tena sawa.

Simaaanishi umwambie kitu kipya hata kama ni cha uongo. Hapana!

Unaweza kufanya au kumwambia hayo hayo ya zamani katika hali tofauti. Hii huchangia kuleta bashabasha na msisimko zaidi baina ya wapendanao. Mapenzi ni ubunifu!

UTANI

Wapenzi wengi wanaishi kama wapo katika foleni ya kutaka kuchomwa sindano. Maisha yao yamejaa u ‘serious’ uliokithiri. Ni kama vile wanaogopana!

Katika ustawi wa penzi hali kama hii si nzuri sana; kwa maana huwa inapelekea wahusika kutokuwa huru sana na wenzi wao. Katika hili mawili huwa ni lazima yatokee.

Kumuogopa sana mpenzi wake au kumchoka sana kwa maana kila siku watakuwa wanafanya kitu cha aina moja kutokana na aina ya maisha wanayoishi.

Utani katika mapenzi ni kitu kinachofanya kila mmoja aongeze na hamu ya kuwa na mwenzake. Kwa kuwa mapenzi ni burudani na amani.

U ‘serious’ unapozidi katika mapenzi huyapoozesha na kufanya kupotewa na hamu ya kuwa karibu na mwenzake.

Maana katika maisha si kila muda ni wa kuongea mipango na mambo mazito mazito. Wakati mwingine ni bora kujisahaulisha matatizo na kero nyingine kwa utani na vicheko vya mara kwa mara. Watu wasiyofanya haya huchokana mapema sana.

MIGOGORO YA MARA KWA MARA

Kwa kuwa wanaokuwa katika mahusiano ni watu wenye akili timamu na wenye uwezo wa kutafakari masuala tofauti, suala la migogoro ni ngumu sana kuepukika. Maana watu wenye upeo wa kutafakari si ajabu kutofautiana kifikra. Lakini mbali na hayo migogoro ni sumu kubwa  katika mapenzi ikiwa wahusika wasipokuwa madhubuti kuidhibiti.

Kunapokuwa na migogoro ya mara kwa mara huwa hakuna fursa ya wahusika kufurahia mapenzi kwa pamoja. Hali kama hiyo inapotokea wahusika huanza kujihisi upweke japowapo katika mahusiano. Matokeo ya yote hayo ni kila mmoja kuanza kuhisi shida kuwa karibu na mwenzake kwa maana muda mwingi watakuwa wanalumbana badala ya kufurahia umoja wao.

Hapo ile raha na faraja ya wapendanao huanza kutoonekana. Kila mmoja humuona mwenzake ni kikwazo cha furaha yake.

MAJIBU MAFUPI

Ili wapenzi wawe na hamu ya kuwa pamoja, kila mmoja ni lazima ampe mwenzake sababu ya kufurahi na kuwa na amani moyoni.

Moja kati ya sababu ya kumpa furaha na faraja mwenzako katika mahusiano ni katika kauli na majibu yako.

Mpenzi wako akiwa anakueleza jambo kiurefu na kwa upana na wewe unamjibu kwa ufupi jua humfanyi kuwa na raha na mazungumzo husika. Kwa maana atakuwa anajiona kama yeye ndiye mwenye shida zaidi ya mazungumzo husika kuliko mwenzake. Hali kama hiyo si nzuri sana.

Kwani humfanya mhusika awe anasita kuanzisha mada baina yenu, hata iwe nzuri vipi. Kwa kuwa anajua hatimaye utamwacha katika hali ya unyonge kutokana na majibu yako.

Kwa kuliona hilo ataanza kukuona kama si chanzo tena cha furaha yake na badala yake atakuchukulia kama mtu usiyetambua thamani yake. Mwishoni hamu ya kuwa na wewe nia lazima tu imtoke.

TAMAA

Kama wahusika waliamua kuwa katika mapenzi baada ya mmoja kuwa na tamaa na mwenzake, na si kupendana kwa dhati na yakini ya nafsi, kuchokana ni suala lisiloepukika.

Mara kadhaa katika makala zangu nimekuwa nikisema tamaa haina maisha marefu. Tamaa siku zote humfanya muhusika awe na kiu ya ghafla na jambo flani hata wakati mwingine kupelekea kupoteza vitu vyake vya muhimu na vya thamani, lakini baada ya kufanikiwa katika jambo hilo kila kitu kwake hubadilika ghafla.

Kukiona atakuwa hakitamani tena. Kukitumia atakuwa anaona kama hastahili vile. Hata katika mapenzi suala ni hilo hilo tu.

Mtu aliye na tamaa na mtu flani huweza kuonekana kumhangaikia flani kwa kila kitu na kuweza hata kufanya baadhi ya watu wadhani kuwa ana mapenzi naye, ila kama ilivyokuwa desturi ya tamaa; akimpata tu kwa muda mchache kila kitu kitaanza kubadilika. Kwake atakuwa mzigo. Atamuona hana jipya. Ilimradi tu. Hiyo ndiyo tamaa na asili yake. Kumchoka mtu huwa ni katika muda mchache sana. Wala pia huwa haiangalii mvuto wa muhusika wala kipato chake.

KUTOKUWA HURU KWA WAHUSIKA

We na mpenzi wako kila mmoja yuko huru na mwenzake? Kila mmoja anaweza kumwambia jambo lolote la kimapenzi mwenzake bila kusitasita? Vizuri sana.

Katika ustawi wa penzi na kujenga hali ya upya wa penzi, kila siku hali hiyo inahitajika sana. Ila wengi hawana.

Kutokuwa huru na mpenzi wako hufanya akuone kama ndugu yake wa jinsia tofauti. Kwa hali hiyo atakuwa haoni kitu kipya sana kutoka kwako.

Mpenzi wako anahitaji kuona tofauti akiwa na wewe na watu wengine na ndiyo maana hata jina lako lina maana tofauti. Mpenzi, Sweetie, Honey! Si kaka, dada au rafiki.

Usipokuwa huru na mpenzi wako unafanya hata upamoja wenu ukose msisimko, hivyo kuweza kupoozesha penzi lenu. Matokeo yake ndiyo kuchokana kunapotokea.

KUTOTOKA PAMOJA

Outing! Huwa unatoka na mwenzako? Wengi huwa hawafanyi hivyo. Baadhi hudhani ni lazima kwenda katika maeneo ya gharama kubwa ndiyo huleta maana ya neno lenyewe. Hapana. Si lazima iwe hivyo.

Hata kwenda katika maeneo tulivu pasina kuhitaji gharama  pia huleta maana na kuweza kustawisha na kuinua tena penzi. Wengi wanaofanya hivi hujikuta kila siku wakiwa na mtazamo bora katika mapenzi yao.

Outing huchochea kuleta upya na raha baina ya wapendanao. Katika hali hii kuchokana si suala linalotarajiwa kutokea.

Ukifuata kwa makini yote yaliyomo hapa hakika kuchokana na mpenzi wako itakuwa ni ndoto. Utakuwa ukisikia kutoka kwa wengine tu. Japo ningependa kutoa sababu zingine nyingi, lakini naomba niishie hapa ili nipishe mada zingine zipate nafasi.

ramadhanimasenga@yahoo.com

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU