TATIZO LIKIKUTOKEA FANYA HIVI KULIMALIZA

TATIZO LIKIKUTOKEA FANYA HIVI KULIMALIZA

499
0
KUSHIRIKI

 

Tatizo la wengi wakipata matatizo ni kukurupuka (panick). Badala ya kutafakari namna ya kupambana na tatizo husika, wao huanza shutuma, kupost hisia zao za chuki katika mitandao ya kijamii na kukasirikiana.

Ifahamike ugomvi hauwezi kuwa sababu ya wahusika kuachana kama wakiwa makini katika kushughulika nao. Ila ugomvi utakua chanzo na sababu ya wahusika kuachana ikiwa wahusika wasipokua makini katika kupambana nao.

Inatakiwa baada ya kuona kuna hali ya kuzuka mgogoro katika mahusiano husika, mmoja ni lazima ajifanye mjinga. Awe tayari kuumia kwa ajili ya ugomvi husika ili mahusiano yao yabaki kuwa imara.

Inatakiwa kuwa hivi. Ugomvi ukitokea mmoja ni lazima ama aache kutoa lawama kwa mwingine, ama aache kujitetea sana badala yake awe tayari kuomba msamaha.

Kuomba msamaha huku maana yake anakubali kuwa kosa husika anahusika nalo ila inatakiwa afanye isionekane kuwa kahusika nalo moja kwa moja.

Mfano. Mwenzako anaweza kuwa anakutuhumu kwa kumsaliti. Hii ni tuhuma nzito sana. Si vema kukurupuka kuikubali ama kuikataa tu ilimradi.

Badala ya  kukataa tu inabidi ukatae huku ukikubali kuwa hisia za mwenzako ziko sahihi kuwaza hivyo, kwa sababu tu ya ukaribu wako na mhusika ama mazingira ambayo umeonekana na mhusika. Sasa wewe inabidi ukomae hapa katika kuomba msamaha.

Omba msamaha kuwa ulikuwa ni ujinga kuwa katika mazingira ya hivyo na mhusika. Omba msamaha kuwa kwa namna moja ama nyingine hata mwenzako angeonekana katika mazingira flani na mtu wa jinsia tofauti na yake ama angekuwa ana mazoea  sana na mhusika hata wewe ungemuwazia vibaya.

Omba msamaha hapa kwa dhati huku ukiahidi kuwa makini zaidi ama kuacha mazoea na mhusika. Wengi wanakosea pale wanapokuwa wakituhumiwa na wenzao kwa vitu ambavyo hawajafanya. Wao badala ya kuangalia kwanini wanatuhumiwa, hukataa tu ama kujifanya na wao wamekasirika.

Heshimu hisia za mwenzako. Kakutuhumu kwa sababu kuna mambo kaona hayako kawaida. Hata kama kweli hukumkosea, cha kufanya si kukataa tu. Bali mwambie uhalisia ulivyokuwa huku pia ukikiri baadhi ya makosa. Kukataa tu kuna tafsiri mbili kwa mwenzako.

Kwanza anakuona unamfanya mjinga. Pili, anaona kama unajitetea tu kwa kosa ambalo umefanya. Usimfanye awaze hivi. Muombe msamaha.

Mahusiano mengi  ya zama hizi yanashindwa kufika mbali kwa sababu wahusika wakikosea hukimbilia katika mitandao ya kijamii kuandika mambo kuhusiana na ugomvi wao ama kununiana. Katika hali hii ugomvi ni lazima uzidi kuwa mkali.

Mgogoro wa mapenzi kwa sababu ni wa kihisia inabidi uthibitiwe mapema. Ukiacha kuwa makini, mbunifu katika kukabiliana nao basi hii ndio huwa njia ya kuvunjika uhusiano husika. Ugomvi wa kihisia una kawaida ya kujiumba zaidi kadiri mhusika unavyohisi kukosewa na kushindwa kuamini unyenyekevu wa mtuhumiwa dhidi yake.

Hakuna mahusiano ambayo wahusika hawagombani. Kila mahusiano kuna matatizo na shida za hapa na pale. Ila mahusiano yanayovunjika kwa sababu ya wahusika kugombana ni yale wahusika walikurupuka katika migogoro yao.

Eti mtu kagombana na mpenzi wake badala ya kusaka suluhu, yeye anakimbilia katika mitandao ya kijamii kulaani mapenzi ama jinsia ya mhusika. Hii ni hatari kwa mahusiano yako.

Pia hata kama ukikosewa jichunge usiongee sana hata ukasema mengine yasiyokuwapo. Wapo waliogombana na wapenzi wao badala ya kushikilia katika tatizo husika wakasema mengi, wakajikuta wanateleza na kusema mengine yanayoleta hisia tofauti kwa wapenzi wao.

Unakuta mtu kagombana na mpenzi wake kwa sababu anahisi anamsaliti. Sasa badala ya kukaa hapo hapo katika ugomvi husika juu ya usaliti wa mwenzake, anajikuta anaropoka na kusema mengine ambayo hayahitajiki.

Katika ugomvi mmoja, mhusika alikuwa akigombana na mwenzake akihisi anasalitiwa. Wakati akiwasilisha hisia zake za kuumizwa, akajikuta anasema kwamba ndiyo maana hata yeye huwa anafikiria kumsaliti mwenzake kutokana na kuwa hamuelewi. Akaenda mbali zaidi na kusema kuwa eti mwenzake yupo yupo tu ndiyo maana huwa anafikiria hata yeye kumsaliti. “Ungejua kuna watu wengi wa maana wananitaka wala usingefanya ujinga huo. Mimi kuwa na wewe ni kama nakusaidia tu ila unaleta ujinga.”

Maneno kama haya yanamfanya mwenzako akufikirie katika namna tofauti. Hata baada ya mgogoro husika kwisha ila atabaki na maswali mengi katika kichwa chake.

Ataanza kujihoji kuwa kumbe mambo yote ambayo huwa unamwambia kuwa yeye kwako ni bora na mzuri sana ni uongo. Atawaza ni mangapi mengine umemdanganya. Atawaza mengi na mwishowe atajihisi hayuko eneo salama sana katika hali yake ya furaha ya nafsi.

Mtu akifika katika hatua hii jua mahusiano husika tayari yanakuwa yamepoteza ladha. Kuwa makini katika kupambana na changamoto zako katika uhusiano. Jifunze namna ya kumaliza mgogoro wa mahusiano yako kabla hujafika mbali zaidi. Hata mwenzako akukosee vipi penda kuwa na fikra chanya. Fikra za kuamini bado kuna nafasi ya kurekebisha kila kitu na mambo kuwa bora tena kama ilivyowahi kuwa awali.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU