TFF IHIFADHI VEMA KUMBUKUMBU ZA WACHEZAJI

TFF IHIFADHI VEMA KUMBUKUMBU ZA WACHEZAJI

310
0
KUSHIRIKI

MICHUANO ya Ligi Kuu Tanzania Bara, imeanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki iliyopita ikiashiria kuanza kwa msimu mpya wa 2017/18, ambao utazishirikisha timu 16 zinazowania kulibeba taji linaloshikiliwa na Yanga.

Kabla ya ligi hiyo kuanza, klabu zilikuwa katika mapumziko, ni matumaini yetu zimepumzika kiasi cha kutosha na pili zimekuwa na muda wa kutosha kujiandaa na ligi hiyo kubwa nchini ambayo ndiyo chimbuko la timu yetu ya Taifa ya Tanzania.

Hii inatupa matumaini kwamba, ligi ya msimu huu itakuwa nzuri kwa kuwa inashirikisha timu ambazo zimejiandaa kufanya vizuri ili kupata bingwa halali.

Hata hivyo, ikumbukwe kwamba hayo yote ni matumaini tu, lakini ukweli na uhalisia wa kila kitu utaanza kuonekana baada ya timu zitakapoanza rasmi harakati za kuliwania taji la ubingwa.

Sisi BINGWA tunapenda kuwakumbusha wahusika wote hasa viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), kutekeleza yanayowapasa kadiri iwezekanavyo ili wasiwe sababu ya kuwakwaza wachezaji na klabu zao.

Ni wazi kwamba, TFF wanafahamu fika wana wajibu wa kusimamia kanuni zote za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ili ligi hiyo iweze kuwa bora.

Mbali na kuwakumbusha kusimamia michuano hiyo ambayo ni mikubwa hapa nchini, tunawaomba pia TFF kusimamia na kutunza kumbukumbu za matukio yote yatakayojiri katika michezo yote.

OmbiĀ  letu hilo linatokana na kwamba, imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kuwapo kwa mkanganyiko wa kumbukumbu za matukio katika michezo hiyo hususani kadi ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wachezaji, baada ya kuonesha vitendo vya utovu wa nidhamu kama ilivyojitokeza msimu uliopita katika rufaa iliyokatwa na Simba dhidi ya mchezaji wa Kagera Sugar, Mohamedi Fakhi.

Tuna imani kama TFF ingekuwa imesimamia vema kumbukumbu za mchezo huo, utata usingekuwapo hivyo tuna imani viongozi wa shirikisho hilo watalisimamia suala hilo kwa umakini na weledi wa hali ya juu ili lisitokee tena msimu huu.

Waamuzi nao ni vyema wakatambua kwamba ili ushindani katika ligi uwe na maana, ni lazima wachezeshe kwa kuzingatia sheria 17 za soka tofauti na hivyo muda ambao klabu zimetumia kujiandaa unaweza usiwe na maana yoyote.

Kundi jingine lenye umuhimu wa kipekee katika kuifanya ligi iwe bora na yenye ushindani ni wachezaji, wana wajibu wa kujituma pale makocha wanapowapa fursa ya kuzichezea timu zao.

Ni muhimu wachezaji kuelewa kwamba uchezaji wa kiwango cha juu hata kama ukiwa katika timu inayoshuka daraja bado utaonekana na hiyo itakuwa fursa nzuri ya mchezaji huyo kujiuza na kuhitajika kwenye timu ya taifa.

Ikumbukwe kwamba, ligi hii itaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha Azam, hivyo kuwapa fursa wachezaji kuonekana sehemu mbalimbali.

Hiyo ni nafasi ya kipekee kwa wachezaji kujiuza na ili soko lao liweze kuwa zuri ni lazima wafanye bidii katika kila mechi watakazocheza.

Tunachotaka kuona ni wachezaji wa Tanzania wanatoka nje baada ya kuonekana wakionyesha uwezo wao kwenye Ligi Kuu Bara, jambo ambalo pia litakuwa na maana katika timu ya taifa.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU