HADITHI: NILISHAKUFA

HADITHI: NILISHAKUFA

490
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia

LAKINI yeye alinitazama mara moja na kurudisha sura yake kwa mwanaume wake. Alinichukulia kama watu wengine waliokuwa mle ndani ya klabu ambao hawana shida yoyote na yeye. Mapigo ya moyo wangu yalianza kunisumbua yakisema kuwa yanamhitaji yule msichana. Nilitokea kumpenda ghafla kupita maelezo.

Kule upande wa shoo Halid alishangaa kuona muda mrefu umepita mimi nikiwa bado sijarudi. Alitazama huku na kule akijiuliza nilikuwa nimekwenda wapi baada ya kutoka chooni. Ilibidi aache kuwatazama wanabendi wa Bana Motema na kuamua kutoka pale eneo la kusimama na kwenda moja kwa moja chooni.

SASA ENDELEA

Mimi nikiwa nimekaa pale nilimuona akitoka eneo la jukwaa na kuelekea chooni, ambako hakunikuta. Aliporudi alinikuta nimekaa kwenye meza moja ya peke yangu. Aliporusha macho yake upande wa mbele, alimkuta yule msichana mrembo.

Halid alitikisa kichwa kunisikitikia kisha akanifuata  hadi pale mezani.

“Ndugu yangu naona umebadili upepo. Huna hamu kabisa ya burudani,” aliongea Halid huku akimtazama yule msichana.

“Kwani vipi mimi nimepumzika tu hapa nilijisikia kupata moja baridi,” nilimjibu nikiwa na sura ya uongo maana ukweli wote ulikuwa wazi.

Tayari Halid alijua kuwa nimempenda yule msichana. Alinishawishi kurudi karibu na eneo la kucheza muziki ili tukafurahie sauti za wanabendi, lakini mimi nilimjibu kuwa ninabaki pale pale. Yeye aliamua kuinuka na kurudi kwenye burudani ya bendi akiniacha mimi nikiendelea kumuwaza yule msichana mrembo kuliko wote mle ndani.

Hakika uzuri wake uliendelea kunichanganya kila dakika. Sikufurahia kabisa shoo za muziki. Watu karibu wote mle ndani, walikuwa wakishangilia na kufuatisha vibao vya bendi ya Bana Motema, wakiimba pamoja nao. Halid aliendelea kula raha ya maisha kwa burudani ile kabambe.

Mawazo yangu yalikuwa ni kwa yule mrembo tu. Nilitamani aniangalie kwa mara ya nyingine ili apate kugundua kitu. Nilitamani ajue kuwa nilikuwa nikihitaji kusema naye. Akili yangu haikumfikiria kabisa yule mwanaume aliyekuwa naye. Nilimuona kama watu wengine mle ndani sikujali kama alikuwa ni mwanaume mwenye pesa zake.

Baadaye kidogo yule msichana aliinuka. Muda huo sasa  nililiona  na umbo lake. Hakika aliumbika pasipo mfano. Alizidi kuniweka kwenye jela ya mapenzi yenye mateso makali. Nilimeza mate mara nyingi kadiri yalivyokuja.

Msichana aliinuka na kumuaga mwanaume wake, kuwa alikuwa anakwenda msalani. Kama chizi nami nilijikuta najinyanyua kwenye kiti na kuelekea chooni.

Hakuna aliyenigundua kuwa nilikuwa namfuata yule msichana. Nilitembea haraka kwenda eneo la choo lililokuwa na vyoo vya kiume na vya kike. Nilipofika kwenye korido nilisimama ili kumsubiria maana alikuwa amekwishakuingia. Baada ya kama dakika kama 12 hivi, alitoka. Macho yangu yaligongana na macho yake. Alinitazama huku akitembea kuja eneo nililopo. Nilizidi kupata shida maana uzuri wake ulinifanya nitetemeke. Aliponikaribia nilijitoa muhanga kwa kumsalimia.

“Habari yako sista?” niliongea huku nikijishtukia.

Alinishangaa kwa sababu eneo lile lilikuwa si rafiki sana kwa salamu. Ukizingatia na jinsi nilivyomsalimia kwa kujishtukia, alichelewa kidogo kuitikia. Alinitazama kuanzia miguuni hadi kichwani kisha akaitikia.

“Nzuri tu,” alijibu kwa sauti nyororo iliyonifanya nijione nakufa.

Alisimama kidogo karibu yangu akijua labda nilikuwa na neno jingine la kumwambia. Lakini alishangaa kuona nashikwa na kigugumizi kikali. Harufu nzuri ya marashi yake ya kizungu yalinifanyaa nilione lile eneo la vyoo kama paradiso.

Baada ya kuona siongei jambo lolote, alianza kupiga hatua akitaka kuondoka.

“Samahani na..na..omba,” niliongea huku nikimuogopa vilivyo.

Aliposikia samahani ya kigugumizi, aligeuka na kunitazama tena kwa macho yale yale yaliokuwa mithili ya risasi.

“Unasemaje?” aliniuliza.

Nilipiga hatua kumsogelea huku nikitafuta neno lolote la kujitetea, maana alinitazama kwa makini akisubiri nitamwambia jambo gani la maana. Nilipomkaribia nilimwambia.

“Nimependa tufahamiane. Mi naitwa Fredy sijui mwenzangu unaitwa nani?” nilimuliza huku nikimpa mkono.

Alinitazama kuanzia chini hadi juu, huku mimi nikiwa nimeugandisha mkono wangu vile vile.

“Naitwa Paulina,” alinijibu bila kunipa mkono.

Akageuka na kutaka kuondoka kabla hajafika mbali alinigeukia.

“Halafu siku nyingine ukitaka kufahamiana na mtu sio unataka mfahamiane maeneo ya chooni, kuwa na akili sawa?” aliongea hivyo na kuondoka mbele yangu.

Nilibaki nimesimama kama nimepigwa na mvua ya mawe. Nilibaki kulimezea mate umbo lake zuri pindi alipokuwa akiondoka. Marashi yake mazuri yalianza kupotea ile harufu ya eneo lile la choo ilianza kurudi taratibu. Nilijisemea kuwa kweli duniani watu wanafaidi. Nikatulia na kujiuliza.

“Itakuwaje siku ambayo nitakuwa hanimuni na mrembo kama yule?”

Nami niliondoka lile eneo na kurudi ukumbini ambako burudani ya Bana Motema ilikuwa ikiendelea kuwanyanyua mashabiki. Nilirudi kukaa pale pale, nilifurahi kulijua jina la yule mrembo. Huku nikichukia kuona amerudi kukaa na yule tajiri. Jina la Paulina lilinikaa sana kichwani, niliona kama alikuwa amenithamini sana kwa kuniambia jina lake. Japo alikuwa ameondoka kwa kunitukana.

Niliendelea kumtazama nisiishiwe hamu. Nilitamani yule mwanaume tajiri aliyekuwa amekaa naye aondoke ili mimi nikakae naye nianze harakati zangu za kumsaka. Jambo lililokuwa likiniumiza zaidi ni jinsi yule mwanaume alivyokuwa akimpiga mabusu huku akimnywesha mara kwa mara kinywaji. Niliumia sana utafikiri Paulina alikuwa mpenzi wangu au mke wangu wa ndoa. Burudani iliendelea kupambana moto watu waliendelea kucheza. Rafiki yangu Halid aliendelea kuburudika. Mimi sikuwa na hamu ya kufuatilia burudani kwa bendi hiyo kutoka Zaire. Ingawa wakati tunatoka nyumbani mimi na Halid, tulikuwa tumepania kucheza na kuruka na bendi hiyo, lakini uzuri wa Paulina ulinifanya nione shoo ya Wanazaire hao kuwa ni ya kawaida.

Nikiwa naendelea kumkodolea macho, Paulina aligeuka kunitazama. Moyo wangu ulilipuka tena. Nilitamani aone pia na moyo wangu maana nilitokea kumpenda sana mrembo huyu. Aliniangalia kisha alimgeukia tena yule mwanaume wake na kuendelea  kuongea naye, wakicheka huku wakigeuka mara chache kutazama burudani kule jukwani.

Baadaye yule mwanaume aliinuka kwenye kiti na kumpa mkono Paulina.  Waliondoka pale kwenye meza pamoja na wale wanaume waliojazia misuli wakielekea kwenye mlango wa kutokea  nje ya ukumbi. Niliishia kumtazama Paulina kwa huzuni kubwa nikitamani kumfuata ili kumueleza hisia zangu juu yake.

Nilijikuta natamani kumweleza kuwa nampenda bila kujali kama alikuwa ameolewa. Akili yangu haikufikiria hivyo kabisa. Niliona kuwa Paulina alikuwa ameumbwa kwa ajili yangu.

Nikiwa naendelea kumtazama Paulina pindi alipokuwa akitoka na mwanaume wake, nilishtuka baada ya kushikwa kwa nguvu na Halid. Halid alikuwa akihema.

“Aise! Bana Motema hawafai muda wote wanaturusha tu. Siku ya leo nimeifurahia sana,” aliongea Halid.

Mimi niliishia tu kumuunga mkono. Lakini mawazo yote yalikuwa kwa mrembo Paulina.  Hata hivyo, Halid alijua kabisa kuwa nilikuwa mbali na jambo analolisema.

“Fredy Fredy acha hizo bwana yule msichana sio saizi yako. Hebu waza mengine usimfikirie kabisa,” aliongea Halid kauli iliyonichukiza kwa kiasi fulani.

Sikumjibu lolote nilielekea kukaa kwenye kiti. Nikiendelea kuwa mtumwa wa hisia za mapenzi dhidi ya Paulina.

“Hebu twende tukacheze bwana unakosaje burudani kama ile?” aliongea Halid huku akivuta mkono.

“We nenda tu nitakuja,” nilijibu huku nikikataa kuvutwa.

Halid aliniacha na kurudi eneo la kucheza. Hakutaka kuendelea kunisumbua maana alishajua kuwa tayari nilishakuwa nimetekwa na mapenzi. Aliendelea kucheza na kufurahia vibao vya Bana Motema huku mimi nikiwa kwenye kipindi kigumu cha kumfikiria mrembo Paulina.

Saa saba usiku bendi zote zilimaliza kutoa burudani. Kilichokuwa kimebaki ni kuruka disko, kucheza nyimbo za akina James Broun, Roy Keison, Dolly Parton na wengineo kutoka Marekani. Baadaye nilimfuata Halid na kumtaka tuondoke kurudi nyumbani. Halid alinikatalia akisema ni mapema sana. Baada ya kumsihi sana, aliamua kukubaliana na uamuzi wangu.

Tulitoka nje ya ukumbi wa Freesize na kurudi nyumbani. Ila Halid hakupenda kwa jinsi nilivyokuwa siku hiyo. Kutokana na usiku kuwa mkubwa, tulipanda magari ya Dakatwende mawili.

Tuliachana na Halid yeye akienda kwake na mimi nikienda kwangu. Mtaa niliokuwa naishi mimi ulikuwa karibu na mtaa wa Halid.

Nini kitafuatia usikose kesho

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU