KWANINI MWANDANI WAKO AKUONE WEWE NI BORA ZAIDI?

KWANINI MWANDANI WAKO AKUONE WEWE NI BORA ZAIDI?

664
0
KUSHIRIKI

ASILI ya binadamu ni kupenda kuwa na kitu bora. Tunaishi katika dunia na kufanya kila tunachoweza kwa sababu ya kutafuta kuwa bora.

Ili mpenzi wako ajihisi amani na awe na jeuri ya kujivunia kuwa na wewe ni lazima uwe bora. Bila kujidanganya, jiulize kama wewe ni bora.

Angalia tabia yako, maneno na matendo yako, je, wewe ni bora kwake? U mbunifu wa kiwango stahili kumfanya mwandani wako ajihisi yuko na mtu bora?

Maisha ya mapenzi yamejaa ushawishi na vituko vya kila aina. Mpenzi wako huko mtaani anaambiwa mambo mengi na rafiki zake, anaona wengi mbele yake na anashawishiwa na vingi. Je, wewe ni  mbora kwake hata kumfanya akuone wa thamani mbali na vingi na wengi anaowaona huko nje?

Si kila anayesaliti ni malaya. Si kila mwanaume anayetoka nje ya ndoa ni mwendekeza tamaa. Wako wengi wenye kusaliti na kutoka nje kwa sababu ya matendo ya wandani wao. Je, matendo na maneno yako ni sahihi hata kumfanya mwenzako ajihisi hofu kutaka kukusaliti?

Kuna baadhi ya wasichana wana kauli za hovyo sana kwa wandani wao. Wanapenda ushindani, si wastaarabu na kitu kidogo ndani ya nyumba yao hukikuza. Wewe mwanamke uko vipi ili mume wako ajione fahari kuwa na wewe?

Mwanaume hataki kuishi na mwanamke mpinzani. Anataka kuwa na mtu mstaarabu, mwenye kubembeleza na msikivu. Mwanamke kutaka ligi na mume ndani yanyumba ni kichocheo cha mwanaume kuangalia nje.

Maisha ya ndoa hujengwa na mwanamke mstaarabu na mwanaume makini. Mwanamke mpenda kelele, jeuri huwa si chaguo la wanaume. Wanaume wengi wanasaliti ndoa zao kwa sababu ya wanawake wa aina hii. Nani anataka kuwa na mwanamke pasua kichwa? Hakuna.

Halikadhalika mwanamke anahitaji mwanaume mwenye kujielewa. Mwanaume mwenye upeo wa kuangalia mambo ya mbele na kusimamia kwa nguvu na utimamu ustawi wa familia yake.

Hakuna mwanamke makini mwenye kutaka mwanaume ambaye yupo yupo tu. mwanaume mwenye kuendekeza kukaa maskani na marafiki hata katika mambo ya hovyo. Mwanamke anahitaji mwanaume mwenye upeo wa mambo. Mwanaume ambaye ataweza kumuongoza yeye kufikia ubora wa familia bora.

Wanaume wengi wanaweka mianya ya wao kusalitiwa kwa sababu ya tabia zao. Unakuta mwanaume mlevi na yuko hovyo hovyo tu. Mwanume anaendesha mambo yake kisiri siri hata kumtia hofu mwanamke wake.

Mwanamke hatakiwi kufanywa kama msaidizi wa kazi. Anatakiwa kufanywa kama mtu mwenye mamlaka na mwenye kuthaminiwa kwa kiwango stahili. Ukiwa msiri sana kwake unamtia wasi wasi.

Atawaza mengi na mwisho anaweza kudhani kuna mtu mwingine ambaye una ajenda naye za kimahusiano. Hali ikifikia hivi na yeye ataanza kuwaza tofauti. Wakati mwingine binadamu ni kiumbe mwenye kupenda visasi tofauti na mnyama mwingine.

Kama mwanaume, jiangalia kama una sifa za kumfanya mwandani wako akuangalie wewe katika jicho la ubora na hadhi. Una sifa za kumfanya mke wako ajivunie kuwa na wewe mbali na mapungufu kadhaa uliyo nayo?

Ili mahusiano ya mapenzi yaweze kuwa bora, ni jukumu la wapendanao kila mmoja kutafuta kuwa bora kwa mwenzie.

Mwanamke inabidi atimize majukumu yake yote kwa mwenzake na ahakikishe namna alivyo anakuwa burudani na muhimu kwa mwenzake.

Mwanaume pia inabidi atimize majukumu yake yote kwa usahihi huku pia akiwa mtu mwenye hadhi ya kuitwa kichwa cha familia, kwa namna yake ya kufikiri, jinsi yake ya kuamua na vile anavyokabiliana na changamoto za mwenzake.

ramadhanimasenga@yahoo.com

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU