MCGREGOR KUMBE ALIVUNJA REKODI YA PACQUIAO KWA MAYWEATHER

MCGREGOR KUMBE ALIVUNJA REKODI YA PACQUIAO KWA MAYWEATHER

364
0
KUSHIRIKI

LAS VEGAS, Marekani

JUZI ulimwengu wa masumbwi ulishuhudia pambano kali ambalo liliwakutanisha mafahari wawili, Floyd Mayweather na Conor McGregor.

Pambano hilo ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi, lilimalizika kwa Mayweather kuibuka na ushindi wa TKO baada ya kumsimamisha mpinzani wake katika raundi ya 10.

Hata hivyo, licha ya Mayweather kupata ushindi huo, lakini kumbe cha moto alikiona kutokana na makonde mengi aliyoyapata kutoka kwa  McGregor.

Kwa mujibu wa taarifa za mwandishi wa masuala ya masumbwi, Mike Chiapetta, raia huyo wa Ireland alirusha makonde 111  yaliyotua mwilini mwa Mmarekani huyo ambaye hajawahi kupigwa kati ya 430 aliyorusha.

Idadi hiyo inatajwa kuwa ni kubwa ikilinganishwa na aliyorusha na kutua mwilini  mwa Manny Pacquiao, katika pambano lililofanyika mwaka 2015.

Si hilo tu pekee kama Pacquiao alivyomtwanga  Mayweather makonde 89, lakini McGregor alijaribu kurusha makonde  mengi ambayo ni moja zaidi dhidi ya Pacquiao ambaye alirusha  429.

Pia katika upande wa kupangua, McGregor anaonekana kuwa na uwiano mzuri kwani aliweza kupangua makonde kwa asilimia 26  ikilinganishwa na asilimia 19 aliyopangua Mfilipino huyo.

Kitu pekee ambacho Pacquiao alimzidi McGregor, ni kushindwa kwa pointi 116-112 ikilinganishwa na McGregor ambaye alipigwa kwa TKO.

Kiasi walichokinga

Baada ya pambano hilo ambalo lilipigwa kwenye Ukumbi wa T-Mobile Arena, Mayweather alijiondokea na hundi ya dola milioni 100 na huku Conor McGregor akiwa amejiwekea kibindoni kitita cha dola milioni  30.

Mbali na mkwanja huo, asilimia nyingine ambayo ilitokana na udhamini wa kurusha pambano hilo ilishuhudiwa Mayweather akilamba mkwanja wa pauni milioni 350 na hii ikiwa ni mara ya pili kwa bondia huyo kulipwa kiasi kikubwa baada ya kile cha pauni milioni  250 alichopewa wakati alipopambana na  Pacquiao.

Kwa upande wa McGregor ambaye ni bondia wa ngumi za mapigano mchanganyiko aliwahi kulipwa fedha nyingi ambazo ni dola milioni tatu, lakini kinara huyo ameweza kuvunja rekodi hiyo ambapo kupitia hati miliki hiyo ya kurusha matangazo ameweza kujikusanyia dola milioni 100.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU