KWA MAJANGA HAYA, WENGER ANATOKAJE MSIMU HUU?

KWA MAJANGA HAYA, WENGER ANATOKAJE MSIMU HUU?

504
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

MAPUMZIKO ya kupisha mechi mbalimbali za kimataifa yamekuja katika wakati mzuri sana kwa klabu ya Arsenal.

Unajua kwanini? Baada ya kile kichapo cha mabao 4-0 walichokipata wikiendi iliyopita dhidi ya Liverpool, ni wazi huu ni wakati sahihi wa kocha wa Gunners, Arsene Wenger, kuirudisha timu yake katika hali nzuri kabla ya kurudi tena kwenye hekaheka za ligi.

Hadi sasa, Arsenal wameruhusu nyavu zao zitikiswe mara nane ndani ya mechi tatu tu za awali. Huku ikipoteza mechi mbili kati ya hizo, sawa na nusu ya mechi zote walizopoteza Tottenham msimu uliopita.

Lakini kuna vitu ambavyo kocha huyo anatakiwa kukaa chini na kuvifanyia mabadiliko ili Arsenal iamke kutoka usingizini, unavifahamu? Hivi hapa vitu vitano vya Wenger kuvifanyia kazi.

Uongozi

Arsenal inaonekana wazi kukosa yule mtu wa kuwafanya wachezaji waingie uwanjani wakiwa na ari ya kusaka ushindi. Mwanzo alikuwepo Arsene Wenger, ila kwa sasa huyo mtu hayupo.

Wenger ni kama amechoka hivi. Na kama hajachoka na anataka kuendelea basi aboreshe namna ya kuwapa morali mastaa wake ambao wanatajwa kuwa ni bora zaidi ya wale ‘Invicibles’ waliotwaa taji bila kufungwa miaka takribani 13 iliyopita.

Huenda nahodha wa timu, Per Mertesacker, akawa mbadala wake kama alivyofanya kwenye fainali ya Kombe la FA kwani hakuna mchezaji mwingine yeyote mwenye uwezo wa kufanya hivyo uwanjani.

Upangaji kikosi

Kama kuna eneo ambalo Wenger huwashangaza wengi ni upangaji wa kikosi chake hasa kwenye mechi muhimu, hili ni eneo ambalo Mfaransa huyo hana budi kulifanyia kazi.

Juzi dhidi ya Liverpool, aliamua tu kumwanzisha benchi nyota aliyevunja rekodi ya klabu ya usajili, Alexandre Lacazette. Pia na Sead Kolasinac, ambaye alianza kuonesha kulizoea haraka soka la England.

Halafu akampanga Rob Holding kama beki wa kati apambane na Sadio Mane! Wakati huo huo, Gabriel alishaondoka na Shkodran Mustafi hatima yake ilikuwa ikining’inia kwenye kuti kavu.

Ugenini mbona shida?

Arsenal pia inatakiwa kuboresha kiwango chao pindi wanapocheza mechi za ugenini. Hadi kufikia sasa wameshacheza mechi 21 za Ligi Kuu England dhidi ya Manchester United, Manchester City, Chelsea, Tottenham na Liverpool tangu mwanzoni mwa msimu wa 2013-14.

Wakishinda mechi mbili kati ya hizo, tangu mwaka 2015 dhidi ya City hawajashinda mechi yoyote Etihad.

Katika hizo mechi, walipoteza 13, vikiwemo vichapo vya 6-0 kwa Chelsea, wiki tano baada ya kupokea kichapo cha mabao 5-1 dhidi ya Liverpool.

Alhamisi

Msimu huu klabu ya Arsenal itakutana na kitu kigeni baada ya muda mrefu sana.

Washika mitutu hao wa London walishazoea kucheza mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya, aidha Jumanne au Jumatano. Lakini msimu huu watacheza mechi za Ligi ya Europa katika siku ya Alhamisi.

Wenger atalazimika kujipanga vyema kwa ajili ya kucheza mechi Alhamisi na Jumapili, kwani kiwango safi watakachokionesha kwenye michuano hiyo na kutwaa taji lake kitawasaidia kuingia Ligi ya Mabingwa Ulaya kirahisi iwapo tu watashindwa kumaliza ndani ya ‘top four’ msimu huu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU