NILISHAKUFA

NILISHAKUFA

659
0
KUSHIRIKI

Ilipoishia

Tulikula nyama ya mbuzi kwa dakika kama 45 hivi. Lakini muda wote huo sikumwona mrembo Paulina zaidi ya kuwaona wanawake wengine mle ndani. Moyo uliendelea kuniuma utadhani Paulina alikuwa mke wangu.

Kiti nilichokuwa nimekikalia nilihisi cha moto. Nilihangaika kwa siri kama kuku anayetaka kutaga.

 “Fredy ukiuendekeza huo moyo wako, hautafanya mambo mengine ya msingi. Kwanini usiache kumfikiria yule malaya?” aliongea Halid kauli iliyonichukiza.

 “Kwanini unamuita Paulina malaya?” nilimuuliza nikiwa nina ndita tatu kwenye paji langu la uso.

SASA ENDELEA

“Anastahili kuitwa jina hilo,” alijibu Halid.

“Huo ni udhalilishaji dhidi ya wanawake Halid si vizuri unajuaje kama malaya?”

“Wewe una miezi saba tu tokea uingie katika mji huu. Unamjua Paulina kuliko mimi?”

“Pamoja na hayo, lakini huwezi jua umfikiriaye kumbe sivyo alivyo. Wewe unaweza ukamwona na mwanaume huyu kesho yule, ukajua kuwa ni mabwana zake kumbe ni marafiki zake tu.”

“Eti eeh?”

“Ndio, mbona mimi nilipomwona na kufanikiwa kuongea naye maneno machache, sikuona hayo uyasemayo juu yake?”

“Ki ukweli ndugu yangu, wewe tayari ushakwama kwenye shimo na kutoka huwezi yaani hata mimi unanipinga?” Aliuliza Halid akionekana kukata tamaa ya kuendelea kunishauri.

“Sikupingi Halid ila ninasimamia kile nachokijua mimi. Mapenzi yanaweza kumbadilisha mtu na kumfanya kuwa mtu bora. Ninaamini endapo Paulina antakuwa mpenzi wangu nitafanya niwezalo kuweza kumbadalisha.”

“Una nini wewe cha kuweza kumbadilisha Paulina?”

“Niache mimi na moyo wangu najua nini cha kufanya.”

“Ungekuwa na pesa ningeamini unaweza lakini huna. Huwezi kumbadilisha mwanamke yule ambaye muda wote anataka kukaa kwenye sanduku la pesa. Hivi hufikirii mara moja tu. Kusoma huwezi hata picha huioni Fredy?”

“Mapenzi hayajengwi kwa pesa Halid. Niamini kuwa nitaweza kumbadilisha Paulina,” nilimjibu kwa kujiamini.

Halid alikasirika, akasimama kwenye meza na kuelekea upande wa jukwaa ambako bendi ya Chekecheke ilikuwa ikianza kutoa burudani. Aliniacha peke yangu nikiendelea kumalizia ile kilo moja ya nyama ya mbuzi.

Saa nyingi zilipita bila kumwona msichana Paulina mle ndani. Moyo wangu uliendelea kuhangaika, usitake kutulia kabisa. Wasichana na wanawake wengine wengi, waliendelea kumiminika ndani ya klabu hiyo. Lakini mtu ninayemtaka sikuona dalili za yeye kuja.

Baadhi ya wasichana walikuwa wakinitamani kwa jinsi nilivyokuwa nimependeza. Nilionekana kama mtu mwenye pesa kumbe nilikuwa ni mtu wa  maisha ya chini.

Baadhi ya wasichana walikuwa wakija pale mezani na kuomba kujumuika na mimi, lakini niliwajibu kuwa mpenzi wangu alikuwa amekwenda uwani. Sikuhitaji kukaa na msichana yeyote kwa kuwa moyo wangu ulishakuwa umetekwa na mrembo Paulina.

Baada ya masaa mawili kupita, ikiwa ni saa tano usiku, nikiwa nimekata kabisa tamaa ya kumwona Paulina siku hiyo, ghafla nilihisi harufu nzuri ya marashi ambayo pua yangu ilikuwa ikiyafahamu.

Moyo wangu ulidunda kidogo, pua yangu iliendelea kuivuta harufu ile ili kujua ilikuwa ikitokea wapi. Upesi niliamua kugeuka nyuma ambako sikuyaamini macho yangu. Nilimwona Paulina akiwa amekaa kwenye meza iliyokuwa ya tatu kutokea kwenye meza niliyokuwa nimekaa mimi. Moyo wangu ulishtuka paaaaaa!! Viungo vyangu vilianza kutetemeka woga mkubwa ulianza kunijia huku nafsi yangu ikifurahi kumwona.

Hakika Paulina alikuwa amependeza tena zaidi ya siku ile. Nilimwona kama ni malaika. Nilibaki nameza mate pasipo kujizuia. Moyoni nilijisemea kuwa wacha niendelee kuwa mtumwa wa mapenzi maana Paulina siwezi kumuacha kumfikiria. Nilijiuliza kwa uzuri ule kweli ninaweza kuyasikiliza maneno ya rafiki yangu Halid ya kutaka niache kumpenda mrembo yule, hataa nililipinga sana suala hilo.

Kila kitu ambacho Halid alikuwa akinishauri siku zote tokea nilipoingia  katika mji huo mkuu, nilikuwa nikimsikiliza na kumwelewa. Lakini kwa suala la Paulina, nilikataa kata kata kumwelewa.

Siku hiyo Paulina alikuwa peke yake. Maana nilikuwa nimeangaza huku na kule kumtafuta yule mwanaume wake, lakini sikumwona. Nilifurahi sana ingawa sikujua kama mwanaume wake angekuja baadaye kidogo. Moyo wangu uliendelea kukimbia mbio za mita 100 kwa sekunde tano. Nilihama kiti nilichokuwa nimekaa na kukaa kile alichokuwa amekaa Halid ili nipate kumtazama vizuri Paulina.

Paulina aliagiza kinywaji cha kizungu kiitwacho Golddrink, ambacho bei yake ilikuwa ni shilingi 600 bei ambayo ni kubwa kuliko bei ya kiingilio cha kuingia kwenye klabu hiyo. Baada ya mhudumu kumletea, aliendelea kunywa taratibu.

Nilitamani aniangalie lakini yeye alikuwa mbali na mawazo yake. Nilimkazia macho sikutaka kugeuka upande wowote nikihitaji ajue kuwa nilikuwa nikimtazama.

Wanaume wengi walikuwa wakienda kwake na kuomba kukaa kwenye kiti kilichokuwa kwenye meza yake, lakini aliwakataza akiwaambia kuwa kiti hicho kilikuwa na mtu wake anayekuja.

Mimi nilijua kuwa mwanaume anayemsubiria, alikuwa ni yule tajiri anayependa kuvaa suti nyeupe. Sikupenda mwanaume yule aje nilimchukia sana nikiamini atakuwa kikwazo cha mimi kueleza hisia zangu kwa Paulina siku hiyo.

Moyo wangu ulianza kujishauri kuhusu kwenda kukaa kwenye kile kiti ambacho Paulina alishakuwa amemkataza mwanaume yeyote kukaa. Nilishauri sana na kwa muda mrefu.

Moyo wangu ulikuwa ukiongeza nguvu ya kuushauri mwili wangu lakini akili yangu yenye maamuzi juu ya mwili wangu ilikuwa ikiogopa kuamua hivyo.

Niliendelea kuhangaika huku marashi ya bei ghari ya mrembo Paulina yakizidi kunikumbusha siku ile uwani. Ghafla niliamua kuinuka. Nilipiga hatua za taratibu kuelekea pale alipokuwa ameketi Paulina huku akili yangu ikitafuta maneno mazuri ya kianzio ya kumweleza.

Bila kuomba kukaa nilipofika nilikaa.

“Habari Paulina,” nilimsalimia huku viungo vyangu vikitetemeka kwa siri.

“Samahani hicho kiti kina mtu,” aliongea Paulina.

“Mbona sijamwona, lakini mimi mwenyewe si mtu?” Niliuliza nikitabasamu kwa woga.

“Usilete maneno ya mtaani nishakwambia kuna mtu anakuja kukaa kwenye hicho kiti.”

“Sawa haina shida akifika nitaondoka,” nilimjibu kwa ujasiri wa woga.

“Unahitaji matatizo?” aliuliza.

“Siogopi lolote Paulina kwa kuwa mimi sijaja kuleta matatizo.”

“Kwanza umelijuaje jina langu?” aliuliza Paulina.

“Msichana mrembo kama wewe. Siwezi kukosa kulijua jina lako,” niliongea safari hii nikijiamini kupita kawaida.

“Sawa ni nani alikwambia jina langu?”

“Wewe mwenyewe uliniambia jina lako, umesahau?”

“Usiongopee lini tumewahi kukutana mimi na wewe?”

“Jumapili iliyopita kule uwani.”

“Kumbe wewe?” aliongea Paulina akinikumbuka.

“Ndio naitwa Fredy,” nilimjibu kwa tabasamu nikifurahi kuona amenikumbuka.

“Fredy uliyenisimamisha chooni uliniudhi sana siku ile. Kwanza nilifanya makosa kukwambia jina langu.”

“Kwanini unasema hivyo Paulina?”

“Utanisimamishaje mimi chooni na kutaka kuongea na mimi?”

“Sasa Paulina ulitaka nije pale ulipokuwa umeketi na yule mwanaume nije kukusalimia, siogopi kupigwa?”

“Kwa hiyo leo ulivyokaa kwenye kiti chake huogopi kupigwa?” aliniuliza Paulina swali lililokuwa gumu kidogo kulijibu.

“Kwa kuwa sijamwona siogopi labda akija,” nilimjibu huku nikitazama pembeni na baadaye kumgeukia.

Hakika moyo wangu ulikuwa umetengeneza ngome kubwa sana ya Paulina, ngome isiyoweza kuvunjika kirahisi. Kitendo cha kuongea naye maneno mawili matatu tu, tayari nilijiona kama ninastahili kuwa mpenzi wake. Nilihisi raha isiyo kawaida.

“Kwa hiyo ulikuwa na shida gani?” aliniuliza Paulina.

“Si lazima niwe nina shida ndio nije kukaa na wewe. Mimi nimekuona peke yako katika hali ya upweke nikaona si vema nikasogea kukuliwaza.”

“Naomba uondoke mpenzi wangu asije akakukuta,” aliongea Paulina kauli iliyoniumiza kwa siri.

“Sikiliza Paulina, naomba nikuweke wazi sina haja ya kuficha maana hata nikificha, mwisho wake siuoni. Ninaomba muda wa kukaa na wewe kuzungumza,” niliongea mimi nikiwa tayari nimejivika silaha ya ujasiri usoni.

“Sina muda wa kuongea na wewe kakaangu,” aliongea Paulina kwa makini maneno yaliyoniumiza.

“Tafadhali sana Paulina, ninahitaji kuongea na wewe naomba unipe nafasi na kama haitapatikana muda huu nitafutie muda mwingine.”

“Bila shaka unataka uniambia masuala ya mapenzi?” aliniuliza Paulina kauli iliyonimaliza nguvu.

Nilibaki nimetoa macho nisione jibu la kumpa.

“Ndio najua unataka uniambie kuwa umetokea kunipenda. Hakuna jingine zaidi ya hilo.”

“Ni kweli Paulina.”

“Haya nakupa muda wa kuongea yote uliyopanga kuniambia, fanya upesi.”

Baada ya Paulina kusema hivyo, nilijipanga kutoka ndani ya moyo wangu. Tayari kwa kuanza kurusha makombora.

Nini kitafuatia? Usikose kesho.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU