UNAOGOPA ASIKUACHE? ITAMBUE DHAMIRA YAKE

UNAOGOPA ASIKUACHE? ITAMBUE DHAMIRA YAKE

436
0
KUSHIRIKI

HAKUNA anayependa kuachwa na mtu ampendaye kwa dhati. Mtu yeyote anayehisi suala hilo hujikuta akiwa mnyonge, mwenye pupa ya kutaka kuokoa penzi lake na wakati mwingine kuchanganyikiwa kabisa.

Kuwa na mtu unayempenda ni zaidi ya starehe ya kawaida. Hakuna aliye radhi kuikosa.

Ila mbali na ukweli huo, wengi wanaachwa na wale wawapendao. Katika jicho la haraka unaweza kudhani inafaa tuwaonee huruma, ila ukweli si huo. Baadhi yao inabidi wajipongeze kwa kuachwa na wale wanaowapenda. Nimekuchanganya kidogo siyo? Tulia. Utanielewa tu.

Katika maisha wakati mwingine ni bora mtu atoke kidogo katika mahusiano na flani ndiyo apate amani na utulivu wa akili.

Ila wengine inabidi waingie katika mahusiano ili wapate raha na kuondokana na upweke walionao. Hali hiyo inatokea kutokana na aina ya mtu uliyenaye katika maisha.

Kuna wengine kila siku katika maisha yao sura zao zinapambwa na tabasamu za furaha na amani kutokana na yale wanayofanyiwa na wapenzi wao.

Ila kwa wengine ni mmmh…!!!! Kila siku visa, karaha na maudhi. Ni aghalabu sana kumkuta akifurahia mapenzi yake na mwenzake. Yeye kila siku ni mawazo tu. Kila siku na kuumizwa tu. Alafu na haya eti tunayaita pia ni mahusiano ya mapenzi. Kuna mapenzi hapa!

Kuna mateso na utumwa tu. Mapenzi ni pale kila mmoja anapofurahia uwepo na hali ya mwenzake. Haya tuyaite vipi mapenzi? Ikiwa mmoja anamhangaikia mwenzake ampende na mwingine hana habari? Hapana.

Ila japo kuna idadi kubwa ya watu waliopo katika aina hii ya mapenzi, mapenzi ya kuumia kila siku. Ila ni wachache sana baina yao wanataka kutoka katika mahusiano na wahusika. Wengi wao kila siku wanaomba wasiachwe kwa maana wao suala la kuacha halipo.

Ndiyo maana mbali na mateso na karaha zingine wenyewe hata wazo hilo hawana. Ndoto zao ni kuwa ipo siku wenzao watabadilika na kuwa vile watakavyo wao.

Sikatai uvumilivu katika mapenzi ni muhimu. Tena sana. Ila hata siku moja sitakaa nikushauri uvumilie mateso, dharau na kutooneshwa kuthaminiwa  na mtu asiyeonesha kujali hata kidogo.

Vitu hivyo ni dalili ya kutopendwa. Sasa kwanini nikushauri uanzishe mahusiano na mtu asiyekupenda. Ni vyema ukaondoka na kutuliza akili yako sehemu nyingine. Akiona thamani yako atakutafuta.

Ndiyo, najua si rahisi hata kidogo kutoa uamuzi wa kuachana na umpendaye kwa dhati na yakini ya nafsi. Ila furaha yako ni muhimu karibu kwa kila kitu unachofanya katika maisha yako.

Bila kuwa na amani katika moyo wako huwezi kufanya kazi kwa bidii, huwezi kusoma vizuri, huwezi ‘kuenjoy’ hata kusikia au kula kitu kizuri. Sasa kwanini uwe na mtu ambaye ni chanzo cha wewe kuwa katika hali hii. Mapenzi si hayo ndugu.

Yachunguze vizuri mahusiano uliyopo huenda unatumika tu ndiyo maana thamani yako haionekani. Unamwambia nakupenda anakujibu sawa. Unamletea zawadi hata kusema ahsante hasemi badala yake ndiyo kwaza anaanza kuitoa kasoro tena kwa maneno ya dharau na nyodo. Unamtumia ‘sms’ ndefu yeye anajibu “K”! Maana yake nini?

Eti bado tuseme tu uko katika mahusiano? Hapana. Anayependwa hayuko kama wewe. Anayejaliwa hafanani na wewe. Anayethaminiwa hakaribiani na wewe kwa lolote. Ila anayetumikia mapenzi anafanana na wewe. Uko na furaha katika mapenzi ya namna hiyo. Mapenzi jina.

Wakati wenzako wakifaidi upamoja wao, wewe ndiyo kwanza unajutia mapenzi. Kila siku tunakusikia eti mapenzi balaa, mapenzi mateso, mara mapenzi ni utumwa. Wala mapenzi hayako hivyo. Ila kuna watu wako hivyo. Mmojawapo ni huyo uliyenaye. Anakupa mateso na mabalaa.

Katika hali ya utulivu jiulize nini kitatokea baadaye katika mahusiano yako hayo ikiwa kila siku ni majuto na maumvivu. Kwanini usitake kujipanga na kuangalia mustakabali mwingine wa maisha yako kimahusiano? Wengi katika hili mnashindwa.

Japo mnaona mnateseka katika mahusiano yenu mnajitahidi kadiri muwezavyo kuonesha eti mko katika furaha. Mbali na hilo mnatumia kila mbinu na jitihada kuhakikisha hamuwapotezi hao wapenzi wenu, ingawa wao wanaonesha dhahiri kutotamani kuendelea kuwa katika mahusiano na nyinyi.

Yote hii ni kutokana na ile dhana kuwa nitampata wapi kama huyu? Cheki alivyokuwa mzuri, angalia mali zake kila mtu anamsifia. Hayo si maisha sasa.

Kwanini uendelee kuwa mtumwa eti kisa huwezi kumpata anayefanana au anayemzidi. Nani anayejua ya kesho? Ulijua kama utakutana na mtu wa aina yake? Sikia.

Ili mapezi yawe faraja na yakupe amani ni lazima mhusika akupe sababu ya kumpenda na kumjali. Matendo ya dharau, kashfa na tabia zingine za kukera ni ishara ya kuwa hakuhitaji katika maisha yake. Anayekuhitaji atakunyenyekea, kukujali na kukusikiliza. Tofauti na hapo, jua hauko na mtu sahihi katika maisha.

Wengine mko radhi kufanya mambo hata msiyokuwa na uwezo nao eti kuwafanya wakina flani wafurahi ili wasiwaache, mkiomba hiki mnatoa, akitaka kile utahangaika ili ukipate.

Kisa? usipokubali utaachwa! Katu huwezi kufurahia maisha ya kimahusiano katika aina hiyo ya mapenzi. Kila siku wewe itakuwa ni kubinyika.

Katika hali hiyo sitashangaa mwenzako kuwa na furaha na amani huku wewe ukikonda na kuanza kupoteza dira hata katika mambo yako ya kimaendeleo.

Hauko kwa mtu sahihi. Wewe ni kama bozo wake tu. Anakwambia kile anachojisikia hata bila kufikiria na wewe pia unafanya katika mtindo ule ule. Mtindo wa bila kufikiria.

Kukubali kuumia na kujitesa kwa ajili ya kuhofia kuachwa ni dalili ya kutojiamini. Kwa mwanya huo unampa mpenzi wako jeuri na mamlaka ya kuendelea kukutesa na kukudharau vile anavyojisikia. Si unahofia utaachwa bwana!

Atazidi kukufanyia vitimbi kwa kuwa anajua huna ujanja kwake. Ni kama kakufuga vile. Eti kakwambia anataka kwenda disko umekubali, jana kakwambia anataka gauni jipya umekubali.

Yote unayafanya kumfurahisha huku ukijua unaharibu bajeti yako ya msingi. Ila kwa kuwa unaogopa kuachwa umeona acha tu ufanye. Hali hiyo mpaka lini?

Unadhani utaendelea kulifuga penzi la mtu asiyekuwa na huruma na wewe mpaka wapi? Maisha si hayo. Kupigania penzi hakuko hivyo.

Huko ni kusagika kwa ajili ya kile unachokiita penzi. Ambalo kwangu naliita utumwa. Kupigania penzi ni pale mnapopendana na mtu alafu kukatokea kutoelewana baina yenu. Sasa hapo ukitumia maarifa na akili katika kuliweka sawa penzi lako utaonekana wa maana.

Na si kwa huyo ambaye akikuona na kitu kipya ndiyo unafaa. Mapenzi yake yameegemea katika vitu zaidi. Sasa hayo mapenzi biashara?

Mpenzi anataka kila siku mshinde katika kumbi za burudani mkiburudika. Hapendi kukusikia unaeda kazini wala unatoa misaada kwa ndugu yeye ni matanuzi tu.

Ukimpa hela analalamika ni ndogo. Akisikia una matatizo hata kukupa pole ni shida. Ila kitu kikitokea kwake hata kisiwe tatizo basi atakifanya kiwe tatizo ili apate chochote kwako. Na wewe unatoa bila kuuliza japo unaumia. Eti unaogopa kuachwa, wakati unaumia. Sasa si bora kuwa bila mpenzi kuliko mpenzi wa aina hii? Maana japo uponaye ila huna sababu ya kusema una mpenzi?

Mateso gani ya moyo unahofia kuyapata ikiwa japo bado upo  naye ila cha moto unakiona. Kuwa na msimamo kisha amua kuwa na yule akupaye furaha na faraja katika maisha yako.

Kuachana na asiyekupenda ni sawa na  kukubaliwa na yule unayempenda akakupenda. Huwa ni faraja na raha sana. Yangu kwa leo nimemaliza.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU