IWE MARA YA MWISHO KUPANGUA RATIBA LIGI KUU BARA

IWE MARA YA MWISHO KUPANGUA RATIBA LIGI KUU BARA

602
0
KUSHIRIKI

 

NA ZAINAB IDDY

IKIWA ni raundi ya kwanza tu imechezwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/18, tayari suala la kupangua ratiba limeonekana kuchukua nafasi.

Tofauti na ilivyokuwa awali, mechi za mzunguko wa pili zimesogezwa mbele kwa kile kilichotajwa kupisha mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars dhidi ya Botswana, ambayo iko kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa).

Kwa kuwa mwanzoni ratiba ilionyesha kuwa mechi za raundi ya pili zitachezwa katikati ya wiki, tayari baadhi ya timu zilikuwa zimeshaanza mipango ya kusafari kuwafuata wapinzani wao.

Lakini, Shirikisho la Soka nchini (TFF) limeamua kuzipeleka mbele hadi mwisho wa wiki hii, jambo linaloonekana kuwavuruga viongozi wa timu husika na hata kuwaacha midomo wazi wadau wa soka.

Hili ni jambo linalokera na donda sugu katika soka la Tanzania, kwani kiuhalisia inafahamika kabla ya kupangwa kwa ratiba ya ligi hiyo ni  lazima yaangaliwe matukio mengine muhimu yanayoweza kutokea kipindi ambacho ligi inaendelea, hasa kalenda ya Fifa na ile ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Lengo la kuangalia matukio mengine ni kutaka kuhakikisha hakuna mwingiliano wa tukio moja na ligi lakini pia kuondoa dhana ya upangaji wa matokeo.

Ni jambo la ajabu na aibu kwa Bodi ya Ligi ambayo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia mashindano hayo makubwa Tanzania.

Ni wazi imeonyesha udhaifu mkubwa mbele ya macho ya wadau wa soka, imethibitisha ni jinsi gani haiko makini katika utendaji kazi wake.

Kwa upande mwingine, sitaki kuamini kuwa kusogezwa mbele kwa mara ya pili kwa michezo iliyokuwa ianze Jumatano ijayo imetokana na maombi ya Simba kuelekea mechi yao dhidi ya Azam FC.

Zipo taarifa zinazoelezwa na baadhi ya viongozi wa Simba kuwa wao ndio walioomba mchezo wao dhidi ya Azam usogezwe mbele kwa kile kilichodaiwa kutokuwapo kwa wachezaji wake wawili ambao ni beki Jjuuko Murshid na mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi.

Wachezaji hao wa Simba kwa sasa wako na timu yao ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ inayowania tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Urusi.

Uganda watashuka dimbani kesho kumenyana na Misri katika mchezo wa marudiano, baada ya ule wa awali wa Agosti 31 ambapo Uganda walishinda bao 1-0 mjini Kampala, bao lililofungwa na Okwi.

Kama kuna ukweli katika hilo ni sababu dhaifu na inayoweza kutafsiriwa kuibeba timu moja, licha ya kwamba mechi zote zilitakiwa kuchezwa katikati ya wiki.

 

Sitaki kuizungumzia sana Simba kwa kuwa Bodi ya Ligi ilikuwa na mamlaka ya kulitupilia mbali ombi hilo na kuliacha lile ya mechi ya kimataifa ambayo nao halina maana kwa kuwa kalenda ya Fifa hutoka mapema.

Hata hivyo, naamini suala la kuja kupangua tena ratiba ya ligi halitajirudia tena, ikizingatiwa kuwa TFF inaendeshwa na viongozi wenye weledi mkubwa, wenye kujua majukumu yao na kuyatekeleza kwa ufanisi.

Ni vema Watanzania wakaona ratiba inapanguliwa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo kama vile majanga ya asili yakiwemo mabadiliko ya hali ya hewa kwa maana ya mvua kubwa, kimbunga au mengineyo.

Kwa maana hiyo basi, kwa sasa yaliyopita si ndwele tugange yajayo, hivyo TFF kupitia kwa bodi yake ya ligi, Watanzania hawatarajii kuona suala la kupanguliwa kwa mara ya tatu kwa ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara likijitokeza tena.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU