MAMBO HAYA YALIIPA USHINDI TAIFA STARS

MAMBO HAYA YALIIPA USHINDI TAIFA STARS

464
0
KUSHIRIKI

NA MARTIN MAZUGWA

KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kimeendelea kuwakosha wapenzi wa soka nchini baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Botswana, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam juzi.

Shukrani zimwendee winga mwenye kasi, Simon Msuva ambaye alipachika mabao mawili na kuihakikishia ushindi timu ya Taifa katika mechi hiyo ambayo kocha wa timu hiyo, Salum Mayanga ameutumia mchezo huo kukipima kikosi chake kabla ya kwenda kuwavaa Lesotho, katika mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Kikosi cha Stars kimeendelea kufanya vyema katika michezo yake ya hivi karibuni chini ya Mayanga ambapo amepata ushindi dhidi ya Botswana mara mbili na Burundi, huku akitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Lesotho mchezo wa kufuzu fainali za Afcon, huku pia kocha huyo akikiongoza kikosi cha Tanzania kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya Cosafa 2017 nchini Afrika Kusini ambapo ilishiriki kama timu mwalikwa.

Mayanga  ambaye alichukua mikoba ya kuinoa Stars kutoka kwenye mikono ya kocha, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ ambaye hakuwa na matokeo mazuri.

Haya ni baadhi ya mambo yaliyosaidia kikosi cha Taifa Stars kutoka kifua mbele dhidi ya Botswana ‘Zebras’ katika mchezo huo wa juzi.

Nidhamu ya hali ya juu

Moja kati ya vitu alivyofanikiwa kwa asilimia kubwa kocha Mayanga ni kutengeneza kikosi chenye nidhamu ya hali ya juu ambayo imekuwa silaha yake kubwa, ni nadra sana kuona Stars wakimaliza, pungufu hii imedhihirika katika mchezo dhidi ya Botswana ambapo ndani ya dakika 90 hakuna mchezaji wa Stars aliyepata kadi yoyote licha ya kucheza madhambi mara 18 huku wakichezewa mara 21.

Umiliki wa mpira

Ilikuwa ni siku ya aina yake ambapo kikosi cha Tanzania kilionyesha uwezo wa hali ya juu, huku safu ya viungo chini ya Himid Mao, Hamis Abdallah, Muzamiru Yassin, Said Ndemla na Rafael Daud, ilikuwa mwiba kwa Botswana ambao walikuwa wakihaha sehemu ya kati kutafuta mipira kiasi kwamba hadi dakika 90 zinamalizika, Tanzania ilikuwa ikiongoza kwa kumiliki mpira kwa asilimia 53 dhidi ya 47 za wapinzani wao.

Ubora wa wakongwe

Ukubwa dawa, uwezo ulioonyeshwa na wakongwe Erasto Nyoni aliyekuwa upande wa beki ya kulia pamoja na Kelvin Yondani aliyekuwa mlinzi wa kati, uliongeza uimara wa safu ya ulinzi ya Stars katika mchezo huo, jambo lililowafanya mashabiki kuwashangilia vilivyo mabeki wa timu hiyo, hasa kila walipoondosha hatari langoni mwao.

Mseto mzuri wa kikosi

Kikosi cha Stars kilichoitwa katika mchezo dhidi ya Botswana, kimekuwa na mchanganyiko mzuri wa wachezaji ikiwahusisha ‘wakongwe’ wenye umri mkubwa wa kati pamoja na vijana ambao wamechanganywa kuanzia katika safu ya ulinzi hadi ushambuliaji ambayo imekuwa silaha kwa Mayanga.

Nassry Aziz aliyeitwa Stars kwa mara ya kwanza kutoka katika kituo cha kulelea vipaji cha Aspire Academy na Ramadhan Kabwili anayekipiga katika klabu ya Yanga ambao wote ni nyota wenye umri chini ya miaka 17, hawakupata nafasi ya kucheza, lakini walikuwa kwenye benchi angalau kuona kaka zao wanafanya nini kitendo kilichowasaidia kuwapa uzoefu.

Ubora wa Manula, Msuva

Ilikuwa siku nzuri zaidi kwa nyota wawili, mlinda mlango namba moja wa kikosi hicho, Aishi Manula  aliyefanya kazi ya ziada kwa kuokoa michomo mitatu ya wazi ambayo kama si uimara wake, Botswana wangemaliza mchezo wakiwa mbele ya Stars, lakini pia  kazi nzuri iliyofanywa na winga wa zamani wa Yanga , Simon Msuva, ilikuwa ya kipekee na kudhihirisha kuwa nyota huyo kwa sasa ameiva kwani amekuwa akifanya makubwa tangu alipotua nchini Morocco anakocheza soka la kulipwa.

Ingizo jipya lawaacha midomo wazi mashabiki

Nyota aliyeitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Stars, Hamis Abdallah anayecheza Ligi Kuu nchini Kenya  katika kikosi cha Sony Sugar, aliwaacha midomo wazi mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo kutokana na ubora wa hali ya juu aliouonyesha kwa kuituliza timu pale inaposhambuliwa, lakini pia akiwa ni fundi wa kuanzisha mashambulizi.

Kutokana na ubora huo, mashabiki walikuwa wakihoji nyota huyo alikuwa wapi kipindi chote kutokana na uwezo wake wa hali ya juu aliouonyesha katika mchezo huo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU