MMEMWELEWA KWELI SIMON MSUVA?

MMEMWELEWA KWELI SIMON MSUVA?

670
0
KUSHIRIKI

 

NA OSCAR OSCAR

TUNAPASWA kuamka mahali tulipolala na kumwelewa mshambuliaji wa Taifa Stars, Simon Msuva. Pamoja na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili katika mismu mitatu ya hivi karibuni, nimemuona akiwa mpya.

Msuva hajamaliza hata miezi mitatu tangu atimkie nchini Morocco anakokipiga na Klabu ya El Jadida, lakini tayari ameonekana kubadilika. Anaonekana tofauti na wenzake aliowaacha hapa nyumbani. Si kwa sababu ya kufunga magoli mawili kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Bostwana juzi, ila namna alivyocheza mechi yote na hususan anapokuwa anafanya maamuzi ya kufunga.

Mshambuliaji huyu wa zamani wa Yanga hajaanza kufunga leo lakini aina ya umaliziaji wake kwenye mchezo dhidi ya Botswana una kitu cha ziada. Sikumuona Msuva yule wa mbio nyingi. Sikumuona Msuva yule mwenye kucheza na jukwaa. Nilimuona Msuva mwenye utulivu mkubwa na mwenye kucheka na nyavu tu za timu pinzani. Msuva anayejua awe wapi na kwa muda gani. Hapo ndiyo hajamaliza hata nusu msimu nchini Morocco, sipati picha endapo angekuwa huko tangu miaka miwili iliyopita.

Mmemwelewa kweli Simon Msuva? Bado nina mashaka makubwa kwa wadau wa soka Tanzania kama tumemwelewa vizuri Msuva. Ukiachilia mbali magoli yake mawili, Msuva anatueleza kwamba wachezaji wetu wanaweza kucheza tu kwenye mataifa ya Afrika yaliyopiga hatua na soka letu likabadilika na Stars ikawa rahisi kufundishika.

Hiki ndicho kikubwa nilichokiona kwa Msuva. Kama tutafanikiwa Muzamiru Yassini akajiunga na Al Merreikh ya Sudan, Ibrahim Ajibu akaelekea zake DR Congo kujiunga na wababe wa Afrika, TP Mazembe, taratibu kazi ya kocha Salum Mayanga itaanza kuwa rahisi. Kama Shizza Kichuya atapata timu Misri huku Aishi Manula akielekea zake nchini Afrika Kusini, muda si mrefu tunaweza kuanza kusogea.

Achana na magoli ya Msuva pale taifa dhidi ya Botswana, huyu mtu tayari ana kitu cha ziada kwa wachezaji wetu kujifunza. Kipindi hiki ambacho ligi yetu bado haina ubora wa kutosha, Mama Afrika anatosha kutuvusha. Ni vema kuwa na ndoto za kwenda kucheza soka Ulaya na kwingineko walikoendelea lakini kwa Taifa letu, njia nzuri na rahisi ni kupitia kwenye klabu kongwe na bora Afrika.

Njia pekee ya kuwa na Taifa Stars imara kwa kipindi hiki ni wachezaji wetu kutoka nje ya mipaka. Hata ukimtazama Abdi Banda alivyocheza na Kelvin Yondani unaona utulivu wa hali ya juu. Hawa vijana wetu wakicheza zaidi ya misimu miwili nje hasa kwenye ligi zenye ushindani zaidi kuliko yetu, tutaona utofauti mkubwa.

Aina ya Himid Mao si vijana wa kufurahia kuendelea kuwaona nchini. Inasikitisha wakati mwingine kumuona Manula bado yuko Tanzania. Kwenda nje hasa kwenye ligi zenye ushindani si kwamba itatufanya tuwe na timu bora ya Taifa lakini hata maisha ya wachezaji wetu yatabadilika mno kwa sababu ligi bora Afrika zinalipa pia zaidi tofauti na Bongo.

Soka ni tofauti na muziki, hata ukiwa na umri wa miaka 60 bado unaweza kuimba. Soka mchezo unaohitaji nguvu zaidi, miaka 10 mpaka 15 inahitaji mchezaji awe ameshavuna pesa za kutosha na kujitengenezea uwekezaji utakaomfanya aishi maisha yake yote bila kusumbua watu. Wachezaji wetu wanahitaji kutupia nafasi zao vizuri kwa manufaa yao pia ya baadaye.

Mmemwelewa kweli Msuva? Tunapaswa kupiga hatau moja mbele. Huu ndiyo muda kwa kina Geoffrey Mwashiuya, Emmanuel Martin kutoka Tanzania. Kama hili linaweza kugeuka kuwa agenda ya kitaifa, tunaweza kusogea. Mtibwa Sugar imekuwa moja ya klabu zinazouza sana wachezaji Simba na Yanga. Kama watabadili upepo na kuanza kuwauza wachezaji wao nje ya mipaka, watapiga hatua kwanza wao na kisha watakuwa wamelisaidia Taifa.

Azam FC wamekuwa mstari wa mbele katika kusimamia soka la vijana, sasa wanapaswa kwenda mbele zaidi na kuwa sambamba na hao wachezaji nje ya mipaka. Hii itawasaidia Azam wenyewe lakini itasaidia pia Taifa. Msuva ameonekana kubadilika si tu kwa sababu amefunga ila uchezaji wake. Anapaswa kutumika kama chachu kwa wenzie waliobaki kutoka kwenye usingizi mzito.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU