TAIFA STARS SAFI, LAKINI…

TAIFA STARS SAFI, LAKINI…

363
0
KUSHIRIKI

 

TIMU ya Taifa Stars juzi ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Botswana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Kocha Salum Mayanga aliingia akiwa na nyota wake wote wanne wanaocheza soka nje ya Tanzania ambao ni  Mbwana Samatta, Simon Msuva, Farid Mussa na Abdi Banda.

Mchezo huo ulikuwa ni wa pili kwa Stars kukutana na  Botswana  katika kipindi cha  miezi minne iliyopita, hivyo wapinzani wao walikuwa wamejiandaa  ili kulipiza kisasi lakini  wakashindwa.

Kutokana na ushindi huo, BINGWA tunaungana na wadau wote wapenda soka ndani na nje ya nchi  kuipongeza timu hiyo kwa ushindi huo.

Pongezi  zetu hizo zinatokana na kwamba pengine ushindi huo utaongeza hamasa kwa mashabiki wa soka kuwa wanajitokeza kwa wingi uwanjani ili kushuhudia timu yao ikicheza, baada ya awali kukatishwa tamaa na matokeo mabaya  ambayo walikuwa wakiyashuhudia.

Hii ni kutokana na kwamba Taifa Stars mara nyingi imekuwa ikifanya vibaya katika michezo yake ya kimataifa ikiwamo hiyo ya kirafiki, jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa mashabiki wengi wa soka nchini.

Lakini  sasa pengine huenda viongozi na wachezaji wanaweza kuwa wamelitambua hilo na kuamua kutuliza kiu yao  kwa kuiandaa timu mapema ili kuondokana na uteja ambao ulikuwa umekiandama kikosi hicho.

Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo BINGWA tunashauri  ushindi huo uwe ni mwendelezo wa kushinda  katika michezo mingine ijayo, vinginevyo hautakuwa na faida yoyote.

Hivyo ni wakati mwafaka kwa sasa viongozi wa Shirikisho la Soka nchini TFF kuhakikisha wanapanga mikakati mbadala ili Watanzania waendelee kuwa na imani na timu yao.

Mikakati hiyo ni kuhakikisha timu inapata maandalizi ya mapema na kila mahitaji yanayotakiwa  ili kuwafanya wachezaji kuwa na moyo wa kujituma wanapokuwa uwanjani, tofauti na kipindi cha nyuma ambapo yalikuwa yakifanyika maandalizi ya kukurupuka.

Mbali na viongozi, pia hiki ni kipindi kwa wachezaji kujitunza ili kulinda viwango vyao kama  tulivyoviona katika mchezo huo walionekana kuwa tofauti, ukilinganisha na mechi zilizopita hivi karibuni dhidi ya Rwanda.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU