UNAKUMBUKA!! SIMBA ILIVYOTWAA UBINGWA BAADA YA MIAKA MITATU 1994

UNAKUMBUKA!! SIMBA ILIVYOTWAA UBINGWA BAADA YA MIAKA MITATU 1994

737
0
KUSHIRIKI

NA HENRY PAUL
TIMU ya Simba maarufu kama Wekundu wa Msimbazi, baada ya kuhangaika kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, hatimaye mwaka 1994 ilitwaa ubingwa wa soka Tanzania Bara baada ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuifunga klabu ya Pan African mabao 3-1.
Mchezo huo ambao uliiwezesha timu ya Simba kutwaa ubingwa huo, ulikuwa ni mkali na wa kusisimua wakati wote wa dakika 90, uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru), Jumamosi, Septemba 24, 1994.
Kabla ya Simba kutwaa ubingwa huo ambao ulikuwa mikononi mwa wapinzani wao wa jadi Yanga kwa miaka mitatu mfululizo, baada ya kucheza mechi hiyo ya mwisho ilifikisha pointi 47 huku wapinzani wao wakuu Yanga wakishika nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 42 baada ya mechi yake ya mwisho kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Pamba ya Mwanza.
Ilikuwa ni vifijo na shangwe kwa mashabiki wa Simba wakati aliyekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni, Profesa Philimon Sarungi, alipomkabidhi nahodha wa Simba, Edward Chumila, kombe jipya la ubingwa wa soka Tanzania Bara.
Kombe la zamani la ubingwa wa soka Tanzania Bara lilichukuliwa moja kwa moja na klabu ya Yanga kutokana na kulitwaa taji hilo mara tatu mfululizo.
Mchezo huo kati ya Pan African na Simba ulianza kwa kasi huku, Pan African wakilisakama lango la wapinzani wao kwa mashambulizi makali ambapo katika dakika ya 13 walifanikiwa kutikisa vyavu za Simba kwa bao lililofungwa na Daudi Ilunda.
Bao hilo la Pan African lilipatikana baada ya Ilunda kuunganisha krosi kutoka kwa Peter Lupokela aliyeambaa na mpira katika winga ya kushoto kabla ya kupiga krosi hiyo.
Simba baada ya kufungwa bao hilo ambapo awali walikianza kipindi hicho cha kwanza kama vile walikuwa wakifanya mazoezi, walicharuka na kuanza kuelekeza mashambulizi makali langoni mwa timu ya Pan African wakiwa na lengo la kutaka kusawazisha.
Mashambulizi hayo yalizaa matunda, kwani katika dakika ya 28 ya kipindi hicho cha kwanza walifanya shambulio moja la nguvu langoni mwa timu ya Pan African na kufanikiwa kusawazisha bao ambalo lilifungwa na mshambuliaji, David Mihambo.
Mihambo alisawazisha bao hilo baada ya kuunganisha krosi safi iliyochongwa na beki aliyekuwa akicheza kwa ‘jihad’ siku hiyo, George Masatu, kutoka winga ya kushoto.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza cha mchezo zinamalizika, timu zilienda mapumziko matokeo yakiwa ni sare ya kufungana bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu zote zikitafuta bao la ushindi kwa kufanya mashambulizi makali langoni kwa mpinzani wake, huku mabeki wa timu zote wakionekana kuwa imara katika kudhibiti mashambulizi hayo.
Mashambulizi ya Simba yalizaa matunda, kwani katika dakika ya 64 ya kipindi hicho cha pili walifanya shambulio moja la nguvu langoni mwa timu ya Pan African na kufanikiwa kupata bao la pili ambalo lilifungwa na mshambuliaji, Juma Amiri.
Bao hilo lilipatikana baada ya Juma Amiri aliyekuwa amepanda mbele kupokea pasi kutoka kwa kiungo mkabaji, Abdul Mashine, aliyekuwa anagongeana vizuri na winga wa kushoto, Nteze John.
Katika dakika ya 32 mshambuliaji Nteze John alifunga kitabu cha mabao kwa kufunga bao zuri baada ya kugongeana pasi vizuri na Athumani China ambaye alikimbia kwa kasi huku akiwalamba chenga mabeki wa Pan African kabla ya kumpasia tena mfungaji aliyemvuta kipa na kuujaza mpira upande wa kushoto mwa goli.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Simba walitoka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakiwa vifua mbele kwa kuwafunga Pan African mabao 3-1 na kwa ushindi huo klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi ilitwaa taji la ubingwa wa soka Tanzania Bara kwa mwaka huo wa 1994.
Kikosi cha Simba kiliwakilishwa na kipa; Mohamed Mwameja, Kasongo Athumani, Rashid Abdallah, Mustapha Hoza, George Masatu, Abdul Mashine, Masoud Shabani, Juma Amir, David Mihambo/Maduwa Zuberi, Edward Chumila/Madaraka Seleiman na Nteze John.
Kikosi cha Pan African kiliwakilishwa na kipa Patrick Mwangata, Nurdin Kasabalala, Hanzuruni Hamisi, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, Reuben Mgaza, Habib Kondo, Peter Lupokela, Shabani Ramadhani, Thomas Mashala, Furahisha Sapi na Daudi Ilunda/China Keya.
Mwisho:

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU