HAKUNA MZURI KULIKO WOTE, JIWEKE BORA KWA ULIYE NAYE

HAKUNA MZURI KULIKO WOTE, JIWEKE BORA KWA ULIYE NAYE

558
0
KUSHIRIKI

 

MAHUSIANO mengi ya vijana yanakumbwa na migogoro na mikasa kila siku. Kijana katika mapenzi anataka mwenza mtulivu, makini, msomi, tajiri na mwenye kumjali kwa kila kitu.

Anataka mwenza mwaminifu, ajiweke kwake tu na amtii kwa kila kitu. Ila bahati mbaya sana kila anayekutana naye anaona anakosa kitu.

Kama akiwa tajiri na maarufu, basi anakosa unyenyekevu na kujali. Akiwa mwenye kujali na msikivu, anakuwa lofa na asiyempa maisha anayotaka.

Kwa sababu hii, kijana anajikuta kila siku akihama mahusiano kwa lengo la kutafuta mahali ambapo atapata hitaji lake. Nani hataki kuwa na mtu mwenye vigezo anavyotaka?

Vijana wengi wana mawazo na fikra zisizokuwa halisi (illusion) kuhusiana na mahusiano ya mapenzi ndiyo maana kila siku wanahangaika.

Kuwa na mtu mtulivu katika mahusiano ni kitu halisi na kinaweza kabisa kutimia. Il kuwa na mtu mwaminifu, mwenye kukufurahisha kila muda, tajiri, msomi na mwerevu kwa kiwango cha juu ni ndoto ngumu kutimia. Utanielewa.

Katika tathmini kadhaa ambazo nimefanya kwa kina juu ya ubora wa mahusiano, kuna mengi nimegundua. Moja na la msingi ni kuwa mahusiano bora kabisa ni yale yanayojengwa katika misingi halisi ya upendo na maelewano.

Yaani wahusika wapendane  kwa dhati na kwa mwitikio wa hisia zao waridhie kuingia katika mahusiano.

Mahusiano ya aina hii hufanya wahusika wawaone wenzao ni watu bora na wenye thamani kuliko wengine wote.

Kama mtu akiamua kuingia katika mapenzi kwa sababu ya mali na vitu (materialistic love), mahusiano haya yanaweza kufurahisha kwa kipindi kichache ila baadaye ni lazima yataboa.

Ni kawaida kwa binadamu kubabaika na vitu vipya. Ila kwa kuwa mbabaiko huu hujengwa kitamaa zaidi basi upya huu wa mali na pesa hukaa kwa muda na kisha hufubaa (novelty wears off).

Na kutokana na hali hii, mtu aliyekuwa na mtu huyu kwa sababu ya mali zake huanza kuona mapungufu yake kwa sababu mwanzo hakuweza kuyaona kutokana na akili yake kuwa imefunikwa na pesa ambazo ndiyo alidhani ni kila kitu kwake.

Kabla hujawa na mtu, jiulize unakuwa naye kwa sababu gani? Mapenzi yanayoanzishwa kwa sababu ya kitu fulani (Conditional love) huwa na umri mfupi kutokana  vitu kuna kipindi hupoteza maana katika maisha.

Vijana wengi hawana amani katika mahusiano yao na kujikuta kila siku wanahama kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa sababu msingi ya uanzishaji wao wa mahusiano si thabiti.

Huwezi kuwa na amani na mtu kama umeanzisha uhusiano naye kwa sababu ya cheo au mwonekano pekee. Wenye vyeo wako wangapi? Wenye mwonekano mizuri wako wangapi?

Sababu sahihi ya kuanzisha uhusiano inatakiwa kuwa upendo wa dhati( Pure love). Katika upendo wa dhati kila kitu cha mwenzako kitaleta raha na hamu. Wanaopendana husaidiana, hufurahiana, humisiana na kutamaniana.

Mahusiano yaliodumu kwa muda mrefu na kuleta raha, si kwa sababu yanahusisha wahusika wazuri sana ama wana akili sana. hapana kabisa. Yamedumu na kuleta msisimko kwa sababu wahusika wanapendana kwa dhati.

Kwa upendo huo kila muda wanakuwa wanatamaniana, wanaheshimiana na kila mmoja huona hatari kumpoteza  mwenzake.

Usihangaike kutaka kujua ni kwanini wakina fulani mbali na kuwa katika mahusiano kwa muda mrefu ila bado wanapendana. Jibu ni rahisi na jepesi sana.

Wanapendana kwa dhati bila nguvu ya chochote kingine ila hisia tu. Unaishi vipi katika uhusiano wako?

Ili kudumu katika uhusiano wako inabidi uwe makini sana katika msingi wa uanzishwaji wake.

Kama ukikurupuka kuanzisha naye uhusiano kwa sababu nyepesi, kama vile mwonekano na mali basi ujue unajiweka katika hatari ya kuishi katika maisha ya unyonge, huzuni kwa muda mrefu wa maisha yako.

Kiu halisi ya binadamu ni furaha ya ndani ya nafsi (inner joy) si laghai ya mambo ya nje. Hata kama utapata gari, pesa na majumba ila kama hakuna furaha ya ndani ya nafsi yako huwezi kujivunia kuwa na vitu vya namna hiyo.

Mara ngapi umeona watu walioolewa na matajiri wanaanzisha uhusiano na watu wa hadhi ya chini? Mara ngapi umeona wanaume waliooa wanawake waitwao mashuhuri na wenye mvuto lakini bado wanahangaika na wanawake wanaoonekana hawana hadhi? Unajua sababu?

Unaweza kuambiwa sababu nyingi sana ila moja na ya msingi ni kuwa wanatafuta ‘inner peace and joy’. Jiangalie wewe. Ni kwanini unataka kuanzisha mahusiano?

Hata starehe ya kufanya ngono huleta raha maradufu ikiwa utashiriki kitendo hicho na mtu umpendaye na anayekupenda kwa dhati. Hilo limethibitishwa na tathmini kadhaa.

Usihangaike kumtafuta mtu mzuri sana, mwenye mali nyingi, mwenye kukujali na kukupenda na mwenye kukufanya kufurahia mahusiano yako. mtu huyo hayupo.

Ila yupo mtu ambaye mnaweza kupendana naye hata kuona mengine hayana uzito mkubwa katika maisha yako ila upendo na uwepo wake.

Usibabaishwe na fikra za mazingira. Mtu muhimu na wa thamani katika maisha yako ni yule mtakayependana na kuelewana naye. Mahusiano bora yako hivyo. Mahusiano yatakayokupa amani na furaha yako hiyo pia.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU