SIMBA WAPELEKE MAONI KAMATI YA KINA NDUMBARO

SIMBA WAPELEKE MAONI KAMATI YA KINA NDUMBARO

946
0
KUSHIRIKI

NA EZEKIEL TENDWA

MWISHONI mwa wiki iliyopita klabu ya Simba, ilitangaza Kamati Maalumu itakayokuwa na kazi moja kubwa ya kumtafuta mzabuni, ambaye atanunua hisa ya 51% za timu hiyo katika harakati zao za uendeshaji mpya wa klabu hiyo.

Kamati hiyo ambayo inatarajiwa kukutana leo ili kuweka mambo yao sawa, inaundwa na wajumbe watano chini ya mwenyekiti wake Jaji Mstaafu, Thomas Mihayo pamoja na wajumbe wanne ambao ni Wakili msomi Damas Ndumbaro, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu, Yussuf Majjid Nassor na Abdulrazak Badru ambaye ni Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania.

Ili kuhakikisha kamati hiyo inafanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa, imepewa siku 45, bila shaka kwa sababu waliochaguliwa ni watu wenye weledi mkubwa na heshima katika jamii, wataifanyia Simba kazi nzuri kama wenyewe wanavyotarajia.

Uongozi wa wekundu hao wa Msimbazi, uliamua kuunda kamati hiyo ili kufanya kile ambacho wametumwa na wanachama wao ambao kwa uwingi wao, waliamua timu hiyo iendeshwe kisasa kama zinavyofanya baadhi ya timu ulimwenguni ikiwamo Arsenal.

Wanachama hao kwa uwingi wao Agosti 20, mwaka huu wakiwa katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, walinyoosha mikono yao kuashiria kukubali hicho kinachokwenda kufanyika na ni mwanachama mmoja tu kati ya 1,216, aliyepiga kura ya hapana hiyo ikimaanisha wengi wape.

Binafsi niseme kwamba mpaka hapo walipofikia Simba, ni hatua kubwa sana ambayo siku si nyingi watafikia ile nchi ya ahadi ambayo wenyewe wanaitaka, kwani ndio waliopitisha kwa kauli moja kutoka kwenye mfumo waliokuwa na kuingia huu wa hisa.

Nilishawahi kuandika na leo narudia tena kusema kwamba, mfumo huu wa hisa ndio ambao unaifaidisha timu kubwa kama Arsenal na endapo Simba watautumia vizuri ni wazi watajikuta wanapiga hatua kubwa ya kimaendeleo na kuzikuta timu zenye majina makubwa barani Afrika kama TP Mazembe ya Congo.

Ni wazi kwamba aliyewashtua Simba kuhusu mfumo huu ni mwanachama wao maarufu, Mohamed Dewji ‘Mo’, ambaye aliweka wazi kwamba anataka kuchukua 50% kwa shilingi bilioni 20, hiyo ikimaanisha kwamba katika huo mchakato wa kuwatafuta wazabuni, hata mfanyabiashara huyo atakuwa mmoja wao.

Kamati hiyo haijaundwa kwa sababu ya Mo peke yake, la hasha! Ni kwa yeyote ambaye anahisi anaweza kuwekeza fedha zake kwenye klabu hiyo, ndiyo maana wakaambiwa jukumu lao ni kutafuta wawekezaji.

Kutokana na kauli hiyo ya uongozi kwamba kamati hiyo inatafuta wawekezaji watakaoweka hisa ya 50%, binafsi nadhani ni wakati mwafaka kwa kila anayehisi anaweza kujitutumua, ajitokeze kwenye kamati hiyo ya kuweka hoja zake mezani ili isije ikatokea yeyote kulalamika mchakato haukuwa wa wazi.

Kilichonifurahisha katika mchakato huu ni huo uwazi uliotangazwa, licha ya kwamba Mo alishaweka wazi mapema lakini wameamua kutangaza kwa wengine wenye nia hiyo, japo inawezekana kuna baadhi ya mapungufu ambayo hayazuii mambo hayo kuendelea mbele.

Mo yeye alishaweka wazi kwamba akifanikiwa kupenya moja ya mambo atakayoyafanya ni kuhakikisha Simba inakuwa na uwanja wake kuliko kila siku kutegemea wa kukodi licha ya ukubwa walionao lakini pia kuwa na academy ya nguvu ya kukuza vipaji vya vijana.

Nadhani hata akitokea mwingine akafanikiwa kupenya, bila shaka ataifikisha Simba pale ambapo wapenzi, wanachama, pamoja na mashabiki wanapataka na hii italiondoa kabisa lile kundi ambalo mara zote limekuwa likiinyonya klabu hiyo.

Niwashauri pia wale ambao walikuwa na sababu zao za kupinga mchakato mzima wa kuelekea kwenye mabadiliko, binafsi naheshimu kile walichokuwa wakikipigania kwani kila mmoja ana mawazo yake, lakini kwa sababu jambo hili limepita, ni wakati wao kuungana na wenzao kusapoti hiki kinachofanyika.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU