WALIKATAA OFA NONO KISA WANAZIPENDA TIMU ZAO

WALIKATAA OFA NONO KISA WANAZIPENDA TIMU ZAO

516
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

KATIKA soko la usajili lililopita, yapo yaliyokuwa gumzo hasa filamu ya Barcelona na Philipe Coutinho, PSG na Neymar na hata ile iliyomhusisha kinda Kylian Mbappe na timu vigogo.

Mbrazil Neymar alifanikiwa kutimkia Ufaransa kujiunga na mabosi wa jijini Paris, PSG, ambapo pia wamemchukua Mbappe mwenye umri wa miaka 18, huku Coutinho akifeli katika mpango wake wa kulazimisha kuondoka Anfield.

Kwa upande mwingine, hawa ni wachezaji waliowahi kupata ofa nono kutoka kwa klabu vigogo lakini wakagoma kuviacha vikosi vyao.

Alan Shearer (Newcastle)

Miaka 20 iliyopita, Shearer aliiwezesha Blackburn kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England huku akikitetea kiatu cha mfungaji bora. Mafanikio hayo yakawavuta Manchester United iliyokuwa chini ya ‘babu’ Alex Ferguson.

Hata hivyo, Shearer alikataa kutua Old Trafford na hatimaye kwenda Newcastle ambako katika msimu wake wa kwanza alibeba kiatu cha mfungaji bora ingawa timu yake ilishika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Man United.

Baadaye, Barcelona walimtaka Mwingereza huyo lakini pia aliwachomolea na hatimaye kumalizia soka lake St James’ Park.

Alessandro Del Piero (Juventus)

Mwaka 2006, Juve walishushwa daraja wakitajwa kujihusisha katika upangaji matokeo. Licha ya kukimbiwa na mastaa Zlatan Ibrahimovic, Patrick Vieira na Fabio Cannavaro, Del Piero alibaki na Juve akiwa na Pavel Nedved na Gianluigi Buffon.

Mabao yake yaliiwezesha Juve kurejea Serie A, lakini haikuchukua ubingwa kwa misimu minne iliyofuata. Hata hivyo, kilichofuata ni timu hiyo kuchukua taji lake la kwanza katika msimu wa 2011-12 ikiwa chini ya kocha Antonio Conte.

Francesco Totti (Roma)

Kwa miaka 25 aliyokaa Roma, Totti alitakiwa na klabu vigogo barani Ulaya lakini msimamo wake ulikuwa ni kubaki klabuni hapo.

Mpaka anastaafu, Muitalia huyo ndiye mchezaji anayeshika nafasi ya pili kwa upachikaji mabao katika historia ya Serie A.

Steven Gerrard (Liverpool)

Baada ya Liver kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, kulikuwa na tetesi kwamba Gerrard angeondoka.

Klabu zilizokuwa zikimtolea macho kwa kipindi hicho ni Chelsea iliyokuwa ikinolewa na Jose Mourinho. Hata hivyo, Gerrard aliitupilia mbali ofa hiyo na kuamua kubaki Anfield kwa miaka mingine zaidi.

Jamie Vardy (Leicester)

Arsenal walimtaka mpachikaji mabao huyo kwa pauni milioni 20 mwaka jana, baada ya mabao yake 24 na kuipa Leicester ubingwa wa Ligi Kuu England.

Licha ya kuwa alifikia uamuzi wa kuwatafutia watoto wake shule mjini London, Vardy aliachana na mpango huo.

Marek Hamsik (Napoli)

Miaka mitano iliyopita, wakala Mino Raiola alitaka kumng’oa Hamsik pale Napoli.  Ni kipindi ambacho nahodha huyo msaidizi wa Napoli alikuwa akiwaniwa na Bayern Munich, Juventus na klabu nyingine za Ligi Kuu England.

Hata hivyo, Hamsik aligoma kuiacha Napoli na badala yake kuongeza mkataba mpya na wakali hao wa Serie A.

Diego Godin (Atletico Madrid)

Mwaka 2015, kocha Manuel Pellegrini alimtaka pale Manchester City lakini haikuwa rahisi kama alivyofikiria.

Mbali na Man City, pia Godin amewahi kuahidiwa mshahara mzuri Chelsea lakini alisimamia uamuzi wake wa kutoiacha Atletico.

Pavel Nedved (Juventus)

Ni staa mwingine aliyetakiwa na vigogo barani Ulaya, lakini aliamua kubaki Juventus. Mwaka 2009, kocha Jose Mourinho, aliyekuwa Inter Milan alimhitaji Nedved, ambapo ilielezwa kuwa alimwahidi mambo mengi ikiwamo nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.

Kilichomzuia Nedved kuiacha Juve ni kwamba angejiunga na wapinzani wao Inter, jambo ambalo hakutaka litokee.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU