BUSWITA AANZA TAMBO

BUSWITA AANZA TAMBO

1414
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

MCHEZAJI aliyekua na utata wa kusaini katika klabu mbili za Simba na Yanga, Pius Buswita, ametamba akisema kesho ataanza kazi iliyompeleka kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Buswita alijiunga na Yanga katika kipindi cha dirisha la usajili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mbao FC aliyoitumikia kwa mafanikio msimu uliopita.

Licha ya jina lake kuwa katika orodha ya wachezaji waliosajiliwa na Yanga msimu huu, lakini hakuweza kuitumikia timu yake mpya katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Lipuli FC, kutokana na kufungiwa mwaka mmoja kutojihusisha na soka ndani na nje.

Mchezaji huyo alijikuta akiingia kwenye adhabu hiyo baada ya kuingia mkataba na klabu mbili tofauti katika msimu mmoja wa Ligi Kuu kwa maana ya Simba na Yanga, hivyo kutakiwa kuilipa Simba kiasi cha Sh milioni 10 ili aweze kufutiwa adhabu hiyo.

Akizungumza na BINGWA, Buswita alisema ana matarajio makubwa ya kucheza mechi ya pili baina ya timu yake mpya na Njombe Mji baada ya suala lake kumalizika.

“Suala langu limeshamalizika hivyo sina shaka nitapangwa katika mchezo wetu unaokuja, kwani ninashauku ya kuona ninafanya kile kilichonileta Yanga.

“Awali, nilikuwa naumia kuona wenzangu wanacheza huku mimi nikiwa naishia kufanya mazoezi, lakini hivi sasa ninaamani kwani  kesi yangu haipo tena baada ya mabosi zangu Yanga kuamua kulimaliza ili mimi niendelee kucheza hivyo kwa mara ya kwanza Jumapili nitaanza kazi rasmi,” alisema.

BINGWA lina taarifa kuwa tayari uongozi wa Yanga umeshaingiza kiasi cha fedha alichokuwa akidaiwa Buswita na Simba benki na kupeleka stakabadhi ya malipo TFF, huku wakikubaliana ili mchezaji wao aweze kucheza lakini pia wakikubaliana na mchezaji mwenyewe kuwa watakuwa wakikata kiasi hicho cha fedha kwenye malipo yake ya mshahara kila mwezi.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU